Navigate / search

Vijue Vikwazo Vinavyozuia Kufanikiwa Kwako.

businessmanrollingstone-32avrs4foyzjjhtpg5emtm

Ili uweze kufanikiwa katika malengo yako ni lazima kila wakati utumie muda kujikagua kuona kama kweli uko katika muelekeo wa mafanikio ama kuna mambo ambayo yanakuzuia kuendelea mbele.Ukishayagundua unatakiwa kuyazingatia kwa haraka sana bila kuchelewa.Mambo yanayochelewesha mafanikio yamegawanyika katika makundi makubwa mawili-Moja ni yale ambaye yanatokana na wengine na pili ni yale ambayo yanatokana na wewe mwenyewe.

Watu wengi sana wanapokuwa wamekwama katika maisha huarakia kuangalia mambo yale ambayo yanatokana na wengine na husahau kabisa kushughulika na mambo ambayo husababishwa na wao wenyewe.Leo ningependa tungalie kwa undani mambo mawili ambayo hutokana na sisi wenyewe na yamekuwa yanachangia sana kuchelewesha ama kukwamisha kufikia malengo tuliyonayo katika maisha yetu.Unapofanikiwa kuyajua mambo haya basi unakuwa umepiga hatua kubwa sana kuelekea katika kuvishinda vikwazo ambavyo vimewakwakmisha watu wengi sana.

Kikwazo cha kwanza ni ile hali ya kushindwa kukamilisha mambo unayoanza kuyafanya.Kuna watu wengi sana wamejikuta  ni watu wa kuanza na kurudi nyuma kila wakati kwa sababu ni wazuri katika kuanza lakini sio wazuri kabisa katika kukamilisha mambo ambayo wameyaanza kuyafanya.Kuna watu kila ukikutana nao wao huwa wanakuwa na simulizi ya jambo jipya ambalo wamelianza katika maisha yao lakini hakuna siku huwa wanaweza kukamilisha hadi mwisho.

Mara nyingi ukipata hamasa ya mafanikio hasa baada ya kusikia habari za mtu fulani ama kusoma unaweza kujikuta unapata nguvu za ghafla sana za kuanza kufanya jambo hilo.Mara nyingi mtu anaweza kuja na kuanza kukushirikisha kuhusu wazo fulani la biashara ama fursa fulani na ghafla bila kufikiria mara mbili unajikuta tayari umeshajiingiza katika kuanza kufanya.Hata hivyo baada ya muda unajikuta kuwa haukuwa umejiandaa kisaikolojia,kifedha na hata kimaarifa.Hii ndio husababisha watu wanapokuwa na nia ya kufuga unashangaa wanaishia kujenga banda tu,wengine wanaanza kulima wanaishia kusafisha eneo tu hawaendelei,wengine wananunua bidhaa na wanakaa nazo tu hadi zinaharibika hawajaanza kuziuza,wengine wanaanza kusoma kitabu kabla hakijaisha wanaanza kingine ambacho nacho hawakimalizi n.k

Tabia ya kuanza jambo na kutomaliza hadi mwisho imewapotezea pesa watu wengi sana na kuwakatisha tamaa ya kuendelea mbele.Ili uwe mtu ambaye unafanikiwa ni lazima uwe na maamuzi thabiti kuwa jambo ambalo umeamua kulianza basi utalifikisha hadi mwisho na upate mafanikio yake.

Ili uweze kuwa mtu ambaye hauishii njiani ni lazima uamue kuwa kwa kila jambo ambalo unaamua kulifanya katika maisha yako ulisimamie hadi mwisho na ulikamilishe na kulimaliza.Ili uweze kuwa na uwezo huu kuna mambo kadhaa ya kuzingatia katika maisha yako.

Unatakiwa kwanza kujiuliza mara mbilimbili-“hivi ni kweli nimeamua kuanza kufanya jambo hili na niko tayari kulipa gharama zote ambazo zinatakiwa?”.Kila jambo ambalo unaamua kulifanya katika maisha yako huwa linaambatana na gharama fulani ambazo ili ufanikiwe ni lazima uwe tayari kuzilipa.Watu wengi sana huwa wanaangalia upande wa faida kubwa wanayoelekea kuipata bila kuangalia ukubwa wa gharama ambayo wanatakiwa kulipa.Kabla haujaanza kulima,kabla haujaamua kujiajiri,kabla haujaamua kuanza ujenzi,mradi mpya n.k kwanza jiulize-Hivi ni gharama gani zinaambatana na jambo hili?Ukishazijua jihoji kama uko tayari kuzilipa.Mfanyabiashara maarufu wa marekani bwana Lewis Hunt alipoulizwa siri kubwa ya mafanikio yake ni ipi,alisema-“Ni uwezo wa kuwa tayari kulipa gharama yote inayohitajika ili kupata kile ambacho unataka”.Watu wengi sana huwa wanakwama kuelekea katika mafanikio yao kwa sababu mara baada ya kuanza kufanya jambo fulani wanakuja kugundua kuwa hawakujua kwa uhalisia gharama ya kweli ambayo inaambatana na kile wanachokitafuta.

Hebu jichunguze leo katika maisha yako-Ni mambo gani ulishawahi kuyaanza na ukashindwa kuyamaliza?Ni biashara gani uliwahi kuianza na ukaishia njiani?n.k-Hebu jiulize kama uliwahi kuhesabu gharama halisi kabla haujaanza ama ulivutiwa na stori za mafanikio uliyoambiwa.Ukiwa mkweli utagundua kuwa mambo mengi sana ambayo umeshindwa kuyakamilisha na umeishia njiani ni kwa sababu haukupata muda mzuri wa kujua gharama ya kifedha,muda,nguvu inayohitajika ili uweze kufanikiwa.Kuanzia leo usianze jambo bila kwanza kuhesabu gharama unayotakiwa kulipa na kisha dhamiria kuwa utailipa bila kushindwa.

Kitu cha pili cha kukusaidia kuwa na uwezo wa kumalizia jambo ulilolianza ni  kujua sababu iliyokusukuma kufanya jambo hilo .Kwenye mafanikio ukishajua sababu ya kufanya kitu basi namna ya kufanya itapatikana tu.Watu wengi sana wanaishia njiani kutokana na ukweli kuwa sababu ambazo zinawasukuma kufanya jambo fulani huwa ni sababu dhaifu ambazo haziwezi kuwatia nguvu wakiwa katika changamoto.

Watu wengi sana huwa wanaishia njiani kwa sababu kilichowasukuma kuanza kufanya kitu fulani ni kwa sababu waliona tu mwingine amefanikiwa.Hivyo wanajikuta wanaanza vitu ambavyo hawana hamasa navyo wala hawana ujuzi unaotakiwa ili waweze kufanikiwa katika kile ambacho wanakifanya.Kuna watu wengi sana nimeshawahi kukutana nao ambao baada ya kuona kuna mtu amefanya bisahara fulani ama kilimo fulani wanachukua pesa,tena wengine ni ya mkopo na wanaenda kufanya,mwishowe wanajikuta wamefeli vibaya sana mara tu wanapoanza na hujikuta hawawezi tena kuendelea mbele.

Kikwazo kingine ambacho kimewafanya wengi wachelewe kufikia malengo yao kwa haraka ni hali ya kila wakati kutafuta sababu ya kukufanya usifanye unachotakiwa.Kwenye safari ya mafanikio ni kuwa,kila wakati utakapoamua kutafuta sababu ya kwa nini hauwezi kufanikiwa basi lazima utaipata.kwa mfano leo nikikukuliza,kwa nini haujafanikiwa kufikia malengo yako kwa mwaka huu?UKitaka kujua kuwa wewe ni mtu utakayechelewa kufanikiwa basi utakuwa ni mtu wa kuorodhesha visingizio tu.Utakuta mtu anasema sina mtaji wa kutosha,ila kuna watu kama wao wanafanikiwa,utakuta mwingine anasema uchumi mbaya,lakini kwenye huohuo uchumI kuna watu wanapanua biashara,utakuta mwingine anasema hafanikiwa kwa sababu hajasoma lakini kuna watu pia hawajoma na wamefanikiwa sana.Usikubali kujizuia kufikia malengo yako.

Vikwazo hivi vyote viko ndani yako.Amua kuvishinda kuanzia leo.

Endelea kutembelea www.JoelNanauka.com/www.Mentorship.co.tz kujifunza zaidi.

See You At The Top

@JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website