Navigate / search

Utafiti wa CHUO Kikuu cha Harvard: Mambo 3 Yanayoleta Mafanikio

Harvard University celebrates Commencement 2014. Spectators watch from the steps of Widener Library. Stephanie Mitchell/Harvard Staff Photographer

Ili kufikia kilele cha ndoto yako na kufanikisha malengo yako yote,ni lazima uwe mtu ambaye kila wakati uko katika hamasa ya kuchukua hatua kuelekea katika lengo kubwa ulilonalo maishani.Kati ya sababu zinazowasababisha watu wengi sana washindwe kufikia malengo yao makubwa ni ile hali ya kuwa leo wako na hamasa kubwa ya kufanya kitu kisha kesho unakuta hamasa imepungua,kesho kutwa wanaanza tena kisha siku inayofuata wamepunguza kasi tena.

Kama wewe ni mtu ambaye hamasa yako ya kufanya jambo inayumbayumba na iko kama homa za vipindi-Leo uko juu kesho uko chini basi itakuchukua muda mrefu sana kufanikiwa.Kuna watu wengi ambao wakikutana na kitu kidogo tu basi huwa wanashindwa kabisa kuendelea kufuatilia ndoto zao.Wengine wakiambiwa neno la kukatisha tamaa na mtu,wengine wakikataliwa kitu,wengine wakiudhiwa jambo fulani n.k basi hutumia hisia zao za hasira ama kuudhika kwa kuacha kufanya jambo ambalo walishaamua tangia mwanzo kuelekea katika mafanikio yao.

Profesa Teresa Amabile wa kitivo cha biashara cha chuo kikuu cha Harvard,aliwahi kufanya utafiti juu ya mambo ambayo huwafanya wale wanaofanikiwa kuwa na uwezo wa kupiga hatua kila wakati bila kukata tamaa hata wakati wengine wote wanaonekana kuvunjika moyo kuendelea kuchukua hatua katika kuelekea kutimiza malengo yao.Utafiti huu ulifanyika kwa miaka mingi na ulipelekea kuandikwa kwa kitabu cha kanuni ya kuendelea mbele(The Progress Principle).

Katika utafiti huu aliwahusisha watu takribani 238 ambao walikuwa wamefanikiwa sana katika nyanja zao.Na akawachunguza kwa muda wa siku takribani 12,000 kwa kila siku kuwasiliana nao na kujua ni mambo gani wamefanya na pia kujua ni mambo gani waliyatumia kuwatia hamasa katika kuelekea kufanikisha malengo yao.Katika watu aliowahoji walikkuwepo mameneja takribani 26 kutoka katika makampuni makubwa sana ya kimataifa.
Utafiti huu ulikuja na matokeo kadhaa ambayo kama na wewe utayajua basi yatakusaidia sana kuhakikisha kuwa unafanikiwa na unapiga hatua kubwa katika kutimiza malengo yako kabla mwaka huu haujaisha.
Moja,ilionyesha kuwa watu wanaofanikiwa ni wale ambao huwa wanajua bila shaka kuwa wanataka nini katika maishba yao.Ni rahisi sana kukutana na watu wanaotamani kufanikiwa ,lakini ni ngumu sana kukutana na watu ambao kwa umahsusi wanajua haswaa wanachotaka.Kuna watu wengi sana ukiwauliza watakuambia wanataka kuwa matajiri lakini kwa kiwango gani,hawajui.Wengine watakuambia wanataka kuwa wafanyabiashara wakubwa ila ukiwauliza unataka kuwa unauza nini na unataka kuwa tajiri wa kiasi gani,hawajui-Wengine watakuambia wanataka kubadilisha jamii au Taifa lao ila ukiwauliza kwa namna gani,hawajui kabisa.

Mafanikio ni matokeo ya kujua bila kuwa na shaka lile jambo ambalo unataka kufanikiwa kwalo.Leo hebu jiulize,hivi mafanikio unayoyazungumzia unayajua kwa ufasaha ama unazungumza kwa ujumla.Nimeshakutana na watu wengi sana ambao ukiwauliza kwa nini hawaishi ndoto yao watakuambia sina mtaji,ila ukijaribu kuwauliza kwa undani wanataka kufanya nini utashangaa kuwa hawako mahsusi kabisa katika kila wanachotaka kufanikiwa.Wengi wamekwama sio kwa sababu hakuna watu wanaotaka kuwasaidia ama hakuna mtaji,bali kwa sababu bado hawajajua kwa hakika wanachokitafuta katika maisha ni nini.Je,wewe unajua unachokitafuta?

Tukikuamsha kutoka usingizini unaweza kutuambia kwa sentensi moja unataka mafanikio ya namna gani?Kama jibu lako ni hapana basi ujue haujajiunga katika safari ya mafanikio.Kitaalamu malengo yako yanatakiwa yawe kama vile unatoa oda kiwandani,kiasi kwamba kama mzalishaji wa kiwandani akiyasoma basi alete kitu sawasawa na kile ulichoagiza-Je,kwa malengo ulinayo yanakidhi kiwango hiki?Kama hapana,wala usiwe na haraka ya kukimbilia kufanya,tengeneza malengo mahsusi kuhusu mwelekeo wako.

Jambo la pili ambalo liligundulika katika utafiti huu ni kuwa watu wanaofanikiwa ni wale ambao huwa wanatiwa moyo na kila mafanikio madogo wanayoyapata huku wakiamini mafanikio makubwa yatakuja pia.Huwezi kuwa mtu ambaye huna shukrani kwa kidogo ulichonacho halafu ukategemea kupata kikubwa,hiyo haiwezekani.Utafiti uligundua kuwa watu ambao kila hatua ndogo wanayoipiga huwa wanaifurahia na kujaa na shukrani huwa wanapiga hatua kwa kasi sana.

Hii inamaanisha watu hawa kila siku wanapoamka asubuhi huangalia kile walichonacho na kuanza kushukuru kuwa wanacho na sio kuanza kuangalia wasichonacho na kuanza kunun’gunika.Wakati wewe unalalamika huna gari la kutembelea kuna mtu hana nauli ya daladala,wakati wewe unalalamika hakuna anayekujali,kuna mtu tangu azaliwe hawajui wazazi wake kwa sababu walimtupa na akaokotwa jalalani na tangia hapo anaishi kituo cha watoto yatima,wakati wewe unalalamika una viatu pea moja kuna mtu alizaliwa hana miguu kabisa,wakati wewe unalalamika mshahara mdogo kuna mtu hajui leo atakula nini na jana amekula mlo mmoja tu.

Kwa hali yoyote ile uliyonayo jifunze kuwa mtu wa shukrani,mwambie Mungu-“Nashukuru kwa hapa nilipo na hivi nilivyo,najua kuna watu wenye hali mbaya kuliko yangu.Ingawa bado sijafika ninakokwenda ila bado nina matumaini ya kufanikiwa”.Amua kuwa mtu ambaye unaona jema katika kila baya,mtu ambaye unaona tumaini katika kila kinachokatisha tamaa.Leo,anza siku yako kwa shukrani.Jikague na usiangalie usivyonavyo,hebu angalia ulivyonavyo na mshukuru Mungu kwa hali yako huku ukifanya bidii katika kufikia malengo makubwa.Leo,utashangaa jinsi ambavyo utajawa na nguvu za kuchukua hatua zaidi.Kumbuka siku zote malalmiko huwa hayawezi kubadilisha hali yako.Unapokuwa mtu wa shukrani unaruhusu ubongo wako kufanya kazi kwa kasi na kuwa na ubunifu zaidi.

Jambo la tatu waliloligundua ni kuwa watu wanaofanikiwa ni wale ambao katika kila changamoto wanayopitia huwa wanaamua kuangalia malengo makubwa na hawako tayari kukatishwa tamaa na kushindwa kudogokudogo.Utafiti uligundua kuwa hata wale waliofanikiwa sana huwa wanapitia nyakati za kukatisha tamaa na huwa wanajikuta wako chini kabisa.Tofauti yao ni kuwa kila wakati wakijikuta katika hali hiyo ya kukatisha tamaa huwa wanaweka macho yao katika ndoto yao kubwa ambayo ndiyo huwatia nguvu zaidi kusonga mbele.Je,unayo picha kubwa ya ndoto yako?Kama unayo basi kila wakati ukikutana na hali ya kukatisha tamaa,weka macho yako katika picha kubwa.Leo usikubali jambo lolote lile likukatishe tamaa ya kusonga mbele.Amua kuwa utachukua hatua kuelekea katika malengo yako.

Kumbuka kuwa ndoto yako inawezekana.
Endelea kutembelea www.JoelNanauka.com/www.mentorship.co.tz ili kujifunza zaidi.
See You At The Top.
©JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website