Navigate / search

Usiishi Kwa Kufurahisha Wengine

Siku moja mwimbaji maarufu wa uingereza Ed Sheeran aliambiwa aeleze siri za mafanikio ambazo zimemfanya afikie kilele cha mafanikio yake.Alieleza mambo kadhaa lakini akiwa anahitimisha akasema haya yote hayatakuwa na maana kama hamtajua jambo kubwa ambalo huwa linawafanya watu wafeli katika maisha yao,nalo ni-Kujaribu kumfurahisha kila mtu.Huu ni ukweli ambao haupingiki,na kuna watu wengi sana wamekwama katika mtego huu na wameshindwa kabisa kujinasua.

Kuna watu ambao wana ndoto kubwa sana na wana uwezo mkubwa wa kuzifanya ndoto hizo zifanikiwe lakini wanashindwa kwa sababu ya tabia ya kutaka kumfurahisha kila mtu katika maisha yao.Tabia ya kutaka kumfurahisha kila mtu katika maisha yako inakufanya uwe mtu ambaye hauishi maisha yako halisi bali unakuwa unaishi maisha ya  wengine.Kiufupi ni kuwa ule uhalisia wako unapotea kabisa na unajikuta unaishi maisha ya watu wengine.

Jambo baya sana kuhusiana na hali hii ni kuwa,unapokuwa mtu unayeishi kwa kuwafurahisha wengine unaweza ukajikuta unajifariji kuwa hayo ndiyo maisha na hakuna namna unaweza kuishi maisha ya tofauti,jambo ambalo sio kweli kabisa.Ili kujigundua kama wewe ni mtu ambaye unaishi ili kuwafurahisha wengine,kuna mambo kadhaa ambayo unaweza kujichunguza ili kuona kama unayo.

Jambo la kwanza ni kujitathmini kama una uwezo wa kusema hapana.Siku ambayo Steve Job aliulizwa maana ya kuwa na focus(mtazamo usiyoyumbishwa) maana yake nini,alijibu bila wasiwasi kuwa ni uwezo wa kusema HAPANA.Kama wewe ni mtu ambaye sio rahisi kusema hapana katika maisha yako basi ujue kwa asilimia kubwa unaishi maisha ya kuwafurahisha wengine na hautafika mbali sana.

Katika ulimwengu tunaoishi kuna mambo mengi sana ambayo yanapigania muda wetu na kati ya hayo,kwa asilimia kubwa ni yale ambayo hayana mchango wowote katika kutusaidia kufikia kilele cha mafanikio tunayoyatafuta.Ili tuweze kufikia malengo yetu basi ni lazima tuwe na uwezo wa kusema hapana kwa baadhi ya mambo yanayotaka kuchukua muda wetu na tunaona kabisa hayana umuhimu kwetu.

Ukweli ni kuwa hauwezi kuwa katika kila group la watsapp,hauwezi kuhudhuria kila sherehe,hauwezi kuwa kwenye kila kamati,hauwezi kuwa katika kila kikundi cha vicoba,hauwezi kuangalia kila kipindi cha TV,hauwezi kusoma kila kitu kwenye fb-Lazima ujifunze kusema hapana kwa baadhi ya mambo.

Hapana ya kwanza unayohitaji kuisema ni kujiambia wewe mwenyewe.Kila wakati akili yako inapokuambia kufanya jambo fulani ambalo unaona kabisa halitakuwa na mchango katika mafanikio yako ya baadaye,jifunze kujiwekea uwezo wa kujiambia hapana wewe mwenyewe.Ukiwa mtu ambaye kila akili yako inachotaka basi unatii,inamaanisha hauna nidhamu ya mafanikio na utachelewa kufika unakokwenda.Hii ndio maana kuna watu ni wanene sio kwa sababu ya vinasaba bali kwa sababu kila akili yao inachowaambia kula basi wanakula tu,kuna wengine wanapoteza pesa hovyo kwa sababu kila ambacho akili yao inawaambia kununua wananunua na baadaye wanagundua kuwa hawakihitaji kabisa.Nidhamu ya kwanza ya mafanikio unayohiitaji ni uwezo wako wa kujiambia hapana wewe mwenyewe.

Hapana ya pili ni ile ambayo unatakiwa kumwambia mtu mwingine ambaye anakutaka kufanya jambo fulani.Watanzania wengi tumekulia katika mazingira ya kuambiwa kusema hapana ni kiburi ama kukosa adabu,kwa sababu hiyo tumejikuta kila wakati tunakubaliana na kila kitu ambacho tunatakiwa tukifanye hata kama hatukipendi ama hatukubaliani nacho.Ili ufanikiwe ni lazima ujenge uwezo wa kusema hapana kwa baadhi ya mambo ambayo unaona fika hayakusaidii.Kama umeshawahi kuwa karibu na mtu ambaye amefanikiwa sana utakubaliana na mimi kuwa hawezi kukubali kila mwaliko anaopewa.Hii haimaanishi kuwa anajidai,bali inafundisha kuwa huwezi kumkubalia kila mtu kila kitu halafu ukategemea uwe mtu mwenye mafanikio.Kila unachoombwa kufanya lazima ujiulzie kama kina umuhimu katika maisha yako ama la.Siku zote ukiona ni jambo linaloharibu hatima yako,usiogope kusema hapana kwa upendo na huku ukitabasamu.

Jambo la pili unalotakiwa kujichunguza ili kuona kama wewe ni mtu ambaye unafanya mambo kwa kufurahisha watu ni kila wakati kujiuliza watu watasemaje ukifanya au ukisema jambo fulani.Kuna watu ni wafungwa wa maoni ya watu katika maisha yao-Kila wakati huwa wanaendeshwa na maoni ya watu kuliko malengo yao

Kuna watu wakianza kuchagua nguo ya kuvaa wanaanza kuwaza hivi john atasemaje?na yule mlinzi je?halafu nimekumbuka na Dorcas akiniona sijui atasemaje leo?-Hawa ni watu ambao wanaendesha maisha yao kwa kutegemea maoni ya watu wengine na kwa sababu hiyo hujikuta furaha yao imekamatwa na yale wengine wanayosema.

Hii inamaanisha kila wanachofanya na kila ambacho hawafanyi hutokana na huendeshwa na maoni ya watu wengine wanachosema kuhusiana na maisha yao.Watu wa namna hii wameogopa kuchukua maamuzi kuhusu mahusiano yao kwa sababu ya kuogopa watu watasema nini,wameogopa kuchukua hatua kuhusu kazi zao kwa sababu ya kuogopa watu watasema nini-Kiufupi wameendelea kubakia katika maumivu ya muda mrefu kwa sababu ya hofu ya maneno ya watu juu ya kile ambacho wataamua kufanya.

Kama kweli umedhamiria kufanikiwa basi unatakiwa usiwe muoga wa maneno ya watu,kama kweli umedhamiria kufika mbali kimaisha basi inatakiwa uwe jasiri wa kusimamia mambo ambayo unayaamini.

Kati ya watu ambao lazima ukabiliane nao kwa maneno ya kukatisha tamaa ni watu wako wa karibu.Wengine watakuwa marafiki,watu uliosoma nao hata wazazi wako pia-Kiufupi watu wanaokujua kwa karibu zaidi ndio ambao siku zote huongoza kuwa na maneno ya kukatisha tamaa zaidi kuhusiana na wewe kufikia malengo yako.Lazima ujiandae kwa hili.

Maneno ya mwanafalsafa maarufu Aristotle aliwahi kusema-Kama hupendi kusikia maneno ya kukatishwa tamaa na kukosolewa basi usiseme kitu,usifanye kitu na usiwe mtu yeyote wa maana-Hii inamaanisha kila unapoona unaambiwa maneno ya kukosolewa ama kukatishwa tamaa,inamaanisha uko kwenye kupiga hatua.

Kitabu cha TIMIZA MALENGO YAKO kimeelezea mbinu 60 ambazo watu waliofanikiwa wanazitumia kufikia kilele cha mafanikio yao.Unaweza kuwasiliana nasi kupitia namba 0655 720197 na tutakuelekeza kwa wakala wetu katika mkoa uliopo ama kama uko Dar Es Salaam na unahitaji kuletewa hadi pale ulipo uanweza kuwasiliana nasi kupitia 0712 224282

See You At The Top

 

 

 

Leave a comment

name*

email* (not published)

website