Navigate / search

Unaijua Hatua Ya Kwanza Ili Kuishi Maisha Unayoyataka?

Je uko tayari kulaumiwa?Je uko tayari kuonekana wa ajabu?Je,uko tayari kuonekana sio wa kawaida?
Haya ni maswali ambayo nakuuliza wewe ambaye unasema kwa mwaka huu ni lazima utimize malengo ambayo umejiwekea katika maisha yako.Unachotakiwa kujua ni kuwa illi kupata kitu ambacho haujawahi kukipata katika maisha yako,ni lazima uchukue hatua ambazo haujawahi kuzichukua katika maisha yako.Ili kufanikiwa katika jambo ambalo hujawahi kufanikiwa katika maisha yako ni lazima ufanye maamuzi ambayo haujawahi kuyafanya hapo kabla.Ili kuwa tofauti na wengine ni lazima uwe na mwelekeo ambao wengine hawana kabisa.
Leo ningependa kukumbusha kuwa unayo kila sababu ya kuamua kufanya maamuzi yasiyo ya kawaida katika maisha yako ili upate mwelekeo ambao sio wa kawaida.Kuna watu wengi sana ambao kitu pekee kinachowachelewesha kupiga hatua ni uoga wa kufanya maamuzi,na kitu cha kwanza ambacho huwa wanafikiria inapofika suala la kufanya maamuzi ni swali la-“Hivi watu watafikiriaje?Hivi watu watanionaje?:”
Kuna mambo mengi sana utashindwa kuyafikia katika maisha yako kama wewe utakuwa ni mtu wa aina hii kila siku za maisha yako.Kuna mambo kadhaa unatakiwa kuyafahamu:
Moja ni kuwa maisha yako ni wajibu wako mwenyewe na hakuna mtu ambaye ana wajibika zaidi yako.Hii inamaanisha kuwa hakuna mtu ambaye anawaza juu ya kuboresha maisha yako zaidi ya wewe mwenyewe.Kuna watu huwa wanaishi kama vile kuna mtu mwingine ambaye anawaza na kuwajibika kwa maisha yao,huwa wanasahau kuwa kama wao wenyewe wasipofanya maamuzi muhimu kuhusu maisha yao basi hakuna mtu ambaye ataweza kuwasaidia kufanya maamuzi hayo katika maisha yao.Hata siku moja usifikiri kwamba kuna mtu anawajibia kukufanyia maamuzi kuhusiana na maisha yako.
Mbili ni kuwa kadiri unavyochelewa kufanya maamuzi ya kubadilisha mwelekeo wa maisha yako mara baada ya kugundua kuwa hauko kwenye mwelekeo sahihi ndivyo utakavyozidi kuzama katika shimo la matatizo uliyonayo.Katika suala la mafanikio kuna aina ya kufikiri inaitwa “Zero Based Thinking” ambayo huwa inasema,kama ningekuwa najua hiki ninachojua sasa muda uliopita je nigefanya maamuzi yale?Kam jibu lako ni sio basi inamana kuwa unatakiwa kutafuta njia ya kubadilisha maamuzi yako kwa haraka kadiri unavyoweza.
Watu ambao huwa wanafanikiwa ni wale ambao huwa wanafanya maamuzi kwa haraka kila wanapogundua kuwa wamekosea bila kujali kuwa wengine watasema nini na bila kuogopa kuanza kufanya kitu kipya.Kwa upande mwingine watu ambao huwa wanachelewa sana kufanikiwa ni wale ambao hata baada ya kugundua kuwa wamekosea basi hupenda kung’ang;’ania maamuzi yao ili mradi tu waonekane wana msimamo wa maisha bila kujali kuwa mwisho wa siku wao ndio watakaoumia.
Leo jaribu kutafakari na jiulize-Kuna maeneo gani ambayo natakiwa kubadilisha maisha yangu na kupata mwelekeo mpya?Ukishagundua basi weka mikakati ya jinsi ya kufanya.Kama unahitaji ushauri wa kitaalamu tafadhali tuwasiliane kupitia 0655720197na utapewa utaratibu maalumu.
See You At The Top
@JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website