Navigate / search

Umekuja Duniani Kufanya Nini?:Mambo 4 Ya Kuyafahamu kuhusu Kusudi Lako La Kuzaliwa

 

beach-838803_960_720

Utafiti ambao uliwahi kufanywa na taasisi ya moyo ya marekani(American Heart Association) uligundua kuwa watu wengi hupata magonjwa ya moyo na kufariki siku ya jumatatu asubuhi.Hii ni kwa sababu baada ya mapumziko ya weekend wanajikuta wanatakiwa kulazimika kwenda kufanya kazi ambazo wanazichukia na ambazo kama wangekuwa na namna nyingine wangeacha kabisa kuzifanya.Pengine hata leo unaposoma Makala hii,upo katika hali ya kufanya kitu ambacho hukipendi na unajilazimisha tu kufanya na pengine ungetamani kufanya kile unachokipenda ila hauwezi.

Kati ya Maswali makubwa sana ambayo watu wengi wamekuwa wanajiuliza ni swali la nimeumbwa kufanya nini.Ukweli ni kuwa hakuna namna unaweza kufurahia maisha bila kuwa unaishi katika lile kusudi lako halisi la wewe kuja duniani.Kwa upande mwingine huwa ni vigumu sana kwa mtu kufanikiwa kama haiishi katika kusudi lake.

Umeshawahi kujiuliza kwa nini samaki akitoka nje ya maji anakufa?Kwa sababu kusudi lake linamtaka aishi kwenye maji.Hakuna haja ya kumfundisha samaki kuogelea mara anapozaliwa,anajikuta tu uwezo wa kuogelea uko ndani yake.Pamoja na nguvu zote alizonazo papa,ukimtoa nje ya maji hawezi kufanya lolote,ndivyo ilivyo-Unapoishi nje ya kusudi uliloumbiwa unajikuta unashindwa kila unachojaribu.

Kuishi nje ya kusudi lako ni kujitengenezea mazingira ya kushindwa maishani na kukosa furaha na utajikuta matatizo yafuatayo yanakuandama:
Kwanza utatumia nguvu kubwa sana kufanikiwa katika unachofanya.Ni kama vile simba akiamua kuogelea,anaweza kujitahidi lakini atatumia nguvu kubwa sana na atafanya kwa shida kwa sababu hakuumbwa kwa ajili hiyo.Watu ambao wako katika maeneo ambayo hawakuzaliwa kufanya wanachofanya utakuta nguvu anayotumia na matokeo wanayopata havifanani.Hebu chunguza maisha yako leo.Linganisha nguvu unayotumia na matokeo unayoyapoata,linganisha muda unaotumia na matokeo unayoyapata-Je,vinafanana ama ndio simba anajaribu kuogelea?

Kumbuka kuwa watu wengi hawafeli kwa sababu hawana vipaji ama uwezo la hasha,watu wengi wanafeli kwa sababu wanafanya mambo na wako sehemu ambazo ukweli ni kwamba hawajaumbwa kuwa hapo.Kama vile ambavyo samaki ameumbiwa uwezo wa kuogelea ndani yake nawe pia kuna uwezo wa kipekee ambao umeumbiwa ili ufanikiwe katika eneo lako.

Pili utakuwa ni mtu wa kuanza na kuishia njiani.Kiufupi ni kuwa kama unafanya kitu ambacho sio sehemu ya kile uliletwa duniani kukifanya,hautakuwa na nguvu ya kukifanya kwa muda mrefu.Kwa sababu hiyo utakuwa ni mtu wa kuanza kufanya vitu na kuishia njiani na hakuna siku utafanikiwa kwa asilimia 100.Kwa sababu hii utajikuta ni mtu wa kuanza upya kila wakati,Jichunguze-Wewe ni mtu wa kuanza upya kila wakati?Hii ni dalili kuwa bado haujajua kusudi lako halisi.

Tatu ni kuwa unakosa kuwa na Hamasa(motivation).Mtu aliye kwenye kusudi lake huwa ni mtu mwenye hamasa ya kufanya kitu alichokusudia bila kukata tamaa.Mara nyingi ili kufanikiwa katika malengo yako utakutana na mambo na nyakati za kukatisha tamaa maishani.Kitu pekee kitakachokufanya ufanikiwe ni ule uhakika kuwa unachofanya ni kitu ulilchoumbwa kufanya.Kuna watu wako makazini leo lakini ukiangalia wanavyofanya kazi utagundua kuwa hawana motivation kabisa,kuna watu wameanzisha biashara zao lakini hawana hamasa kabisa na wanachofanya ,matokeo yake wanakuwa wa kawaida sana hawafanikiwi.Je,una hamasa na jambo unalofanya.

Nne ni kwamba kama ungepata njia nyingine ya kupata pesa usingeendelea kufanya unachofanya leo.Kiufupi ni kuwa unafanya unachofanya si kwa sababu unakipenda bali kwa sababu ndio chanzo cha pesa kwako.Kama katika mawazo yako kuna kitu kingine unatamani kufanya Zaidi ya kile unachofanya leo maana yake ni kuwa bado hauiishi ndoto yako.

Kitu kikubwa nilichojifunza katika maisha yangu ni kuwa kadiri unavyoligundua kusudi lako mapema ndivyo unavyoweza pia kufanikiwa kwa haraka na pia hautaweza kuwa na furaha ya kudumu bila kuishi ukifanya kile ulichoumbwa kufanya.Lakini ni muhimu kujua kuwa hakuna kuchelewa katika kuligundua kusudi lako,bila kujali umri ulionao unaweza kuamua leo kufanya juhudi kuvumbua kusudi lako.Mafanikio yako yamefichwa katika uwezo wa kuligundua na kuliishi kusudi la maisha yako.

Kumbuka kuwa hakuna mtu ambaye ameumbwa bila kusudi lolote,kumbuka kuwa hakuna mtu ambaye kusudi lake ni dogo-Kila mtu ana nafasi ya kufika juu ya kilele.Kama vile ambavyo ndege huwa haziwezi kugongana angani kila moja ina fursa ya kupaa juu sana,ndivyo ilivyo kwa wanadamu kila mmoja ana fursa ya kupaa juu kileleni.

Makala zijazo nitakuelekeza namna ya kulivumbua kusudi lako na jinsi ya kutoka hapo ulipo hadi kuanza kuiishi ndoto yako ila unaweza pia kuwasiliana na mratibu wa malezi ya ndoto/mentorship program kwa nambari 0655 720 197 ili uweze kununua DVD inayofundisha kuhusu namna ya kuigundua ndoto yako ama CDs zingine za namna ya kutoa hotuba nzuri,jinsi ya kufaulu mitihani yako kwa kiwango cha juu,namna ya kuwa bora mara 10 katika unachofanya,jinsi ya kuiishi ndoto yako,namna ya kufikia kilele cha mafanikio n.k.

Kumbuka kuwa kila jumamosi ya mwisho wa mwezi kunakuwa na mafunzo ya kukusaidia kufikia ndoto yako.Mafunzo haya hufanyika Dar Es Salaam katika Jengo la GEPF ghorofa ya 4 na hufanyika bure.Mafunzo haya pia yataanza kufanyika mikoani hivi karibuni.Usiache kuhudhuria,na kwa maelezo Zaidi unaweza kutumia namba hiyo hapo juu kuulizia.
Kumbuka kuwa unaweza kupata mafunzo ya kila siku kupitia ukurasa wangu wa facebook(JoelNanauka) na instagram(joel_nanauka)unaweza kuufungua na kulike na usiache kualika na wenzako pia.

Kumbuka kuwa Hatua ya kwanza ya mafanikio ya ndoto Yako huanza na
kuligundua kusudi lako.

Ndoto Yako Inawezekana.

See You At The Top

Leave a comment

name*

email* (not published)

website