Navigate / search

UKIWA TAYARI KUFANYA JAMBO HILI MOJA BASI NDOTO YAKO LAZIMA IFANIKIWE.

Dream-Big1

Kila mtu anataka kufanikiwa,kila mtu anataka kufikia kilele cha ndoto yake,kila mtu anataka kufika hatima yake lakini je kila mtu anajua anatakiwa kufanya nini ili kuhakikisha malengo yake yanafanikiwa?

Siku moja watu walikuwa wanamsifia sana Michelangelo kuhusiana na mchoro ambao alikuwa ameuchora kwenye dari la ndani la kanisa(Sistine Chapel) na kuona kama ni kitu cha ajabu sana kuweza kufanyika.Siku alipoulizwa kuwa mbona mchoro huo umewashangaza wengi?Aliwajibu kuwa-“Kama wangejua gharama niliyoingia ili kuweza kukamilisha mchoro huu basi wasingeshangaa sana”.Jibu lake lilizidi kuongeza maswali kwa aliyekuwa anamuhoji pale alipomuuliza tena,gharama anayoizungumzia ni ipi,ndipo Michelangelo aliposema “Nilitumia miaka 4 kila siku nilikuwa nimelalia mgongo ili niweze kuchora kwenye dari hili unalloliona leo”.

Kitu kikubwa sana unachokihitaji ili kufanikiwa katika ndoto yako ni kujua aina ya gharama unayotakiwa kuilipa na uwe tayari kuilipa bila kuwa na shaka yoyote.Kocha wa Michael Jordan,Steve Alford alipoulizwa kuhusu mafanikio ya Jordan kwenye mpira wa kikapu alisema-“Sishangai kumuona anafanikiwa kwani akiwa katika timu ya olimpiki alikuwa ananishangaza sana,alikuwa wa kwanza kufika uwanjani na nilipokuwa nimemaliza program za mazoezi za siku hiyo wakati wengine walikuwa wanaondoka yeye,aliendelea kubakia na kufanya mazoezi yake binafsi pale uwanjani”

Wakati unaendelea kufuatilia ndoto yako kwa bidii kuna swali moja ambalo hautakiwi kulikwepa.Kadiri utakavyoweza kulijibu swali hili kwa ufasha basi ujue ndivyo utakavyoweza kufanikiwa haraka-Swali lenyewe ni hili-“Kuna gharama gani natakiwa kuilipa ili nifanikiwe katika lengo hili nililonalo?”Kwenye kila ndoto kuna gharama,je ya kwako unaijua?

Kama unataka kufanikiwa kifedha unahitjai kuwa tayari kulipa gharama ya kujifunza elimu ya kifedha(financial intelligence),nunua vitabu hudhuria semina pia-Lakini pia unahitaji kujifunza kuwa makini na matumizi yako na kujitahidi kila wakati kutotumia zaidi ya vile unavyoingiza.Ni lazima pia uwe tayari kujinyima kununua vitu unavyovipenda kwa muda fulani ili uweze kujenga msingi imara wa baadaye.Kama kweli unahitaji kufanikiwa kwenye ndoto yako utahitaji kuwa tayari kugharamia kununua vitu vinavyojenga ndoto yako zaidi kuliko vinavyokuburudisha.Utahitaji kutumia muda wako mwingi Zaidi katika kujifunza kuliko katika kujifurahisha,utahitaji kusoma wakati wengine wanaangalia tamthilia,utahitaji kusoma kitabu wakati wengine wanasoma magazeti ya udaku,utahitaji kusoma Makala ndefu kama hii badala ya kusoma hadithi za kuchekesha,utahitaji kuamka mapema zaidi kuanza siku yako kuliko wenzako wote,utahitaji kuwa na nidhamu ya kutumia muda wako-Kiufupi kama kweli unataka kufanikiwa ni lazima uwe mtu tofauti kabisa na ulivyo sasa.

Namna ulivyo leo ndio imekufanya uwe na mafanikio ya kiwango ulichonacho leo,kama kweli unataka kufanikiwa kwa kiwango kingine ni lazima uamue kuwa mtu wa aina nyingine kabisa katika maisha yako.Kulingana na mtaalamu wa michezo anayeandikia Gazeti la USA Today,John Troup anasema mwanamichezo yoyote ambaye anajiandaa kwa michezo ya olimpiki huwa anafanya mazoezi kwa masaa 4 kila siku kwa siku 310 kabla hajaenda katika mashindano na huwa wanaamka mapema kiasi kwamba ifikapo saa 1 kamili asubuhi basi wanakuwa wameshamaliza mazoezi yote(Wakati wengine ndio wanakuwa wanaamka).
Leo nataka ufanye kitu cha muhimu kuhusu ndoto yako-Hebu jiulize ni gharama gani natakiwa kuilipa ili kuifanya ndoto yangu iweze kukamilika.Hebu jaribu kuorodhesha mambo yote ambayo ndio gharama unazotakiwa kulipa na anza mara moja kuzilipa.Gharama za ndoto yako ni kama bidhaa dukani,kadiri unavyoweza kuilipa mapema ndivyo kadiri utakavyoipata mapema.
Kila siku usisahau maneno ambayo Paul Bryant alisema-“It’s not the will to win that matters-Everyone has that.It’s the will to prepare to win that Matters”( Cha muhimu zaidi kwenye kuifanikisha ndoto yako sio utayari wa kutaka kufanikiwa,bali utayari wako wa kujiandaa na kulipa gharama za mafanikio”.Tafadhali jiulize na upate jibu wa aina ya gharama uanzotakiwa kuzilipa na uanze kuzilipa mara moja.

Kumbuka Kuwa ndoto yako Inawezekana,
Endelea kutembelea www.JoelNanauka.Com ili kujifunza zaidi.
See You At The Top

Leave a comment

name*

email* (not published)

website