Navigate / search

UKICHUKUA HATUA HII BASI UJUE UNAKARIBIA KUFANIKIWA.

joel

Mara nyingi kwenye maisha unahitaji kuwa tayari kuchukua hatua  moja kubwa(leap step) ambayo inaweza kuwa ndio chanzo cha mafanikio yako na itakufungulia mwanzo mpya katika maisha yako kuanzia hapo.Mike Kelley alifanikiwa kusoma kwa muda wa mwaka mmoja tu katika shahada yake ya kwanza na baada ya hapo alishindwa kabisa kuendelea na masomo yake chuoni.Kwa sababu ya kukosa elimu ya kutosha Mike alijikuta anauza bidhaa za urembo katika kisiwa cha Hawaii nje ya hoteli ya Maui,Hawaii.

Kwa muda mrefu akiwa anaendelea na biashara yake alijaribu sana kupata tenda kubwakubwa toka kwa makampuni na mahoteli mbalimbali yaliyokuwa maeneo ya karibu lakini hakufanikiwa kwa sababu kulikuwa tayari kuna wafanyabiashara ambao walikuwa wamebobea na walikuwa wanawauzia mahoteli hayo makubwa kwa miaka mingi sana.Ili aendelee kufanya biashara yake vizuri Mike alikuwa anapenda sana kusoma majarida ya kumjenga kibiashara na kumasaidia kujua kinachoendelea katika eneo lake la biashara.Siku moja katika kusomasoma aligundua kuwa hoteli kubwa ya Maui ilikuwa imepata meneja mpya.Hapo akaona hiyo ndiyo fursa ya kupata mkataba.

Badala ya kumsubiri meneja mpya aje aripoti hotelini Mike alijigharamia na akasafiri kwa ndege hadi Colorado na akaenda kumtafuta huyo meneja huku akiwa na maelezo,vipeperushi na baadhi ya  bidhaa anazoziuza.Alipofika na kufanikiwa kukutana naye alimpongeza na kisha alimweleza kuhusu biashara yake na kumwambia angefurahi kumuona atakapokuja kuripoti katika kazi yake mpya.Baada ya meneja kuripoti Hawaii ni kama vile alimsahau kabisa Mike lakini siku moja Mike alishangaa akapigiwa simu na akafanikiwa kupewa mkataba ambao unamwingizia mamilioni ya pesa kila mwaka.Kwa sasa Mike anamiliki kampuni kubwa sana yenye wafanyakazi zaidi ya 175 na anaingiza zaidi ya dola milioni 5 kwa mwaka.

Hii ni siri mojawapo ya mafanikio katika maisha yetu ya kila siku,ni lazima uamue kuchukua hatua ambayo siyo ya kawaida.Mike alikuwa na hofu alipofikiria kuhusu kukutana na meneja mpya,alijiona bado ni mfanyabiashara mdogo,alihisi pengine angemkatalia lakini aliamua tu kwenda.Ili ufanikiwe ni lazima uchukue hatua hata pale unaposikia hofu(Feel the fear and do it anyway).Kuna mambo mengi tunayofikiri hayawezekani kumbe yanawezekana sana kama tukiamua tu kuchukua hatua fulani isiyo ya kawaida.

Ili uweze kufanikiwa ni lazima uamini kile Dr.Myles Munroe alichoambiwa pale alipokuwa anahofu ya kumtumia mtu kitabu chake ili amwandikie “foreword”(Maneno ya utangulizi) na akawaambiwa “Never say no to yourself before you have tried it”(Usijiambie haiwezekani kabla haujajaribu).Hivi ni mara ngapi umetamani kuchukua hatua fulani katika maisha yako au ulipata wazo kumwambia mtu fulani kitu lakini hata kabla haujajaribu ukajiambia-“hawezi kukubali,atanikatalia”.

Hivi kuna mambo mangapi ambayo leo ungekuwa umeshafanikiwa kama ungeamua kuchukua hatua bila kuogopa ama bila kufikiri kwamba ungekataliwa?Hata leo kuna vitu vingapi ambavyo unaogopa kuchukua hatua eti kwa hofu tu utakataliwa.Siku moja nilikutana na mtu analalamika ameongezewa kazi nyingi ofisini na hajaongezwa mshahara nilipomuuliza umeongea na bosi wako kuomba nyongeza akasema “Hapana,kwani hatakubali”.Nikamwambia nenda kajaribu ukiwa umeandika ongezeko la kazi zako na uwe na hoja za nguvu.Cha ajabu alipoenda bosi wake alishangaa sana kuona uzito wa kazi alizonazo kwa sasa tofauti na fikra alizokuwa nazo,akakubali siku hiyo hiyo akaandika barua ya nyongeza ya mshahara.
Kama unafanya biashara usiogope kumfuata mtu eti kwa hofu hatanunua,kama unataka mkopo usihofu kuomba eti kwa hofu ya kutokupewa,usiwaze kukataliwa kabla haujajaribu.

Watu wanaofanikiwa kutimiza ndoto zao ni wale ambao wanajaribu jambo lilelile ambalo huwa wanahofia halitafanikiwa.Leo,hebu jaribu kuorodhesha ni mambo gani ambayo unaona ni mawazo ambayo yanaweza kubadilisha maisha yako lakini kila ukitaka kuchukua hatua unapata hofu kuwa hautafanikiwa.Ukishafanikiwa tafadhali amua mara moja kuchukua hatua kama Mike.Usichoke kuendelea kujaribu kila wakati hata kama mara ya kwanza hautafanikiwa.Ila naomba uniahidi kuwa siku ukifanikiwa utaniambia na mimi pia nifurahi pamoja nawe.

Kumbuka Kuwa ndoto yako Inawezekana,
Endelea kutembelea www.JoelNanauka.Com ili kujifunza zaidi.
See You At The Top

Leave a comment

name*

email* (not published)

website