Navigate / search

Ufanye Nini Unapokosolewa

Moja ya maneno ambayo siwezi kuyasahau yaliyowahi kusemwa na mwanafalsafa maarufu Aristotle ni pale aliposema-“Kama hautaki kukosolewa,basi amua kutosema chochote,kutofanya chochote na usiwe mtu wa maana,ubaki kuwa wa kawaida”(If you want to avoid criticism,say nothing,do nothing and be nothing).Msemo huu niliufahamu wakati muafaka wa maisha yangu ambapo niliamua kuchukua hatua ambayo watu wengi walikuwa hawaelewi na waliikosoa.

Kitu ambacho nimejifunza kwenye maisha ni kuwa,hakuna namna unaweza kufanya kitu kikubwa ambacho hakijazoeleeka na kila mtu awe upande wako,HAIWEZEKANI.Namna pekee ya kila mtu kukuunga mkono ni pale ambapo utakuwa unafanya kama wao,unasema kama wao na unaishi kama wao.Mara tu utakapoanza kuishi tofauti na wao basi ujiandae kukabiliana na changamoto ya kupingwa.kukosolewa,kusemwa vibaya na hata wakati mwingine kutengwa kabisa.

Kwa sababu ya uoga huu kuna watu wengi sana ambao wanaugua ugonjwa wa “Neophobia”-Hofu ya kufanya kitu kipya kwenye maisha yao.Na wengi ambao wamekumbwa na ugonjwa huu ni kwa sababu ya uoga wa maneno ya watu hasa kuogopa kukosolewa katika kile wanachokifanya.Kuna mambo kadhaa ningependa uyafahamu:

Jambo la kwanza ni kuwa watu wengi sana walishakata tamaa na ndoto zao,na kwa sababu hiyo huwa wanaamini watu wengine pia hawatakiwi kutimiza ndoto zao.Kuna watu ambao maisha yao huwa yamejengwa katika falsafa ya “Msiba wa wengi sherehe”.Watu wa namna hii huwa hawako tayari kufeli peke yao,kwa kila wanaloweza watajitahidi kuhakikisha kuwa kuna watu wengi wanaofeli pamoja nao.Siku ukijaribu kuwashirikisha wazo lako watu wa namna hii utaona jinsi ambavyo watakukatisha tamaa na kukutolea mifano ya watu mbalimbali ambao walijaribu na walifeli.Nia yao kubwa haswa sio kukuepusha na kupata hasara bali huwa ni kuhakikisha kuwa kama wao walifeli basi na wewe unafeli pamoja nao.

Hii ndio maana ni muhimu sana kuzingatia unachukua ushauri wako kutoka kwa mtu wa nanma gani.Kuna watu ambao kwa sababu wao wamefeli basi wanaamini kuwa hakuna mtu mwingine anatakiwa kufanikiwa katika lile walilofeli ama katika jambo lingine lolote wanalofanya.Watu wa namna hii huwa wako haraka sana kuwakatisha tamaa wengine na kuwaonyesha kuwa hawawezi,kila ukikutana nao ni watu ambao watakuwa wako “Negative” mawazo yao huwa ni hasi siku zote na kwa sababu wengi wao huwa wameshakata tamaa huwa hawaamini kwenye jambo lolote lile,na kila ambalo utajaribu kuwaambia watakuambia kuwa haliwezekani kabisa.

Jambo la pili ambalo ni muhimu kulifahamu mapema ni kuwa,watu wengi huwa hawapendi watu walio tofauti.Kuna shauku ya kawaida sana duniani ambapo watu hupenda kila mtu afanane na wao na mara tu utakapoanza kufanya ama kuishi tofauti na wao wanaanza kukusema ama kuwa mbali na wewe.Kama unafanya kazi na uko ofisini ukianza kuwa “serious” na kazi yako na kuanza kuepuka stori za umbea zinazoendelea,utaanza kusikia wanasema unajidai.Ukiwa na rafiki zako na mlizoea kupoteza muda kwa kupiga stori tu zisizo na maana kila siku,utakapoanza kuwa bize na kujisomea ama kufanya mambo mengine ya maendeleo watasema unajidai.Kama ulizoea kutumia pesa kila siku jioni kununua bia,utakapoacha na kuanza kuweka akiba,wasipokuoana kijiweni wataanza kusema unajiona matawi.Kwa ufupi ni kuwa, watu huwa wanataka kutufanya vile tulivyo,na pale utakapoanza kuishi maisha kwa namna ya tofauti basi utashangaa jinsi ambavyo wataanza kukusema maneno mengi mabaya.

Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha kuwa umejiandaa kisaikolojia kuwa mtu wa tofauti.Hii inamaanisha kuwa kujiandaa kiakili kukabiliana na kila mtu ambaye atajaribu kuanza kukuambia maneno ya kukukatisha tamaa ama kukukosoa.

Ili ukabiliane na hali hii ni lazima uhakikishe kuwa una uwezo wa kusimama peke yako na kuendelea kufanya kile ambacho umekikusudia kwenye maisha hata kama kila mtu ameamua kuwa kinyume na wewe.Kitu ambacho kitakushangaza zaidi ni kuwa,mara nyingi watu ambao watakuwa wa kwanza kukukosoa na kukukatisha tamaa ni wale ambao wako karibu zaidi na wewe.Jambo hili huwa linawaumiza watu wengi sana,ila ni muhimu kukabiliana nalo ili uweze kushinda.

Siku zote kumbuka kuwa sio kila mtu ambaye anakuambia “tuko pamoja”,”sitakuacha”,”nitakusaidia” n.k atakuwepo na wewe mara zote.Kuna wakati unashangaa watu wa namna hii huwa ndio wa kwanza kuwa mbali na wewe unapoanza kufuatilia ndoto yako ama unapokuwa unapitia kwenye changamoto kubwa za maisha yako.

Fanya maamuzi,bila kujali watu wangapi wapo kinyume na wewe,na wangapi ambao wanakukosoa kusimamia kitu ambacho unakiamini kwenye maisha yako.

See You At The Top

@JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website