Navigate / search

Ufanye Nini Kuongeza Kiwango Chako Cha Mafanikio

Christophe Columbus aliwahi kusema “You You can never cross the ocean until you have the courage to lose sight of the shore”(Hauwezi kuvuka bahari kwenda upande wa pili hadi uwe na ujasiri wa kuacha kuangalia ufukwe).Hivi umeshawahi kujiuliza ni kwa nini kuna watu wengi sana ambao wameshindwa kupiga hatua kubwa katika maisha yao na ukiwaangalia wana uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo makubwa katika maisha yao?
Hata wewe inawezekana leo uko unafanya kitu ambacho kipo chini kabisa ya uwezo wako lakini umeendelea kufanya tu kwa sababu umehitimisha kuwa hakuna namna unaweza kufanikiwa kwa kiwango cha juu zaidi.Mwaka jana nilisoma ripoti ya Shirika la Kazi duniani(ILO) na moja ya tatizo ambalo walilisema linawakabili vijana wengi sana wa kitanzania kwa sasa ni kufanya kazi ambazo ziko chini ya uwezo wao(underemployement).Hii inamaanisha kuna watu wengi sana ambao wanakubali kufanya vitu ambavyo viko chini ya uwezo wao.
Maneno ya Columbus ni wito kwa kila mmoja wetu.Kwa tafsiri rahisi anachosema ni kuwa kuna watu wengi sana ambao wanatamani kuvuka bahari na kwenda kuona upande wa pili lakini kwa sababu wanavutiwa sana na ufukweni walipo sasa,basi huwa wanaona bora wabakie hapo.Ukweli ni kuwa kuna watu wengi sana ambao wataondoka duniani wakiwa na uwezo mkubwa ndani yao ambao hawajautumia kwa sababu tu ya kuridhika na mambo madogo waliyonayo.
Kuna sababu kubwa mbili zinazowafanya watu washindwe kuchukua hatua kutoka pale walipo ili waende kule wanakotaka:
Kwanza ni kuridhika na hali waliyonayo,hii inamaanisha kuwa kuna watu ambao ni kama wamesharidhika na hali ambayo waliyonayo na wanaona hakuna umuhimu wakutafuta kitu cha ziada katika maisha yao.Kuna watu wanaamini mshahara wanaolipwa ndio bora zaidi na hawawezi kulipwa mshahara mkubwa zaidi,kuna watu wanaamini biashara wanayofanya hawataweza kuikuza zaidi ya hapo,kuna watu wanaamini wao watakaa hivyohivyo bila kupata kazi nzuri,kuna watu wameshaamini na kukubali kwamba wao wa akili kidogo-Ukishalikubali tatizo ulilonalo hakuna namna unaweza kulitatua.
Njia ya kwanza ya kutatua tatizo ulilonalo ni kulichukia.Kama umefika hatua na ukaona tatizo linalokukabili umeshalikubali na unaliona kama ni sehemu ya maisha yako basi ujue hakuna namna utalitatua.Watu wengi hawapigi hatua kwa sababu wamesharidhika na pale walipo,vile walivyo na kile wanachopata na wanaona hakuna namna wanaweza kufanikiwa.Usiwe mmoja wapo-Ni kweli unatakiwa kushukuru kwa kiwango ulichopo sasa lakini hautakiwi ubweteke kama umeshafika tayari-Kumbuka kuna kiwango cha ju kinakusubiri.
Sababu ya pili ni kutokuwa tayari kupoteza walichonacho.Unachotakiwa kukumbuka ni kuwa hakuna namna unaweza kupata kitu kikubwa na kipya bila kupoteza hata kidogo kile ulichonacho.Ili uende sehemu nyingine ni lazima utoke hapo ulipo.Kuna watu wengi sana wanataka kupiga hatua ila hawako tayari kubadili marafiki,hawako tayari kubadili tabia zao n.k kwa ufupi wako tayari kubaki na kidogo walichonacho hata kama hakiwasaidii sana kuliko kujihatarisha kutafuta kikubwa wanachotaka.Usiwe mmoja wao.
Ili upate kitu kisicho cha kawaida ni lazima ufanye maamuzi yasiyo ya kawaida katika maisha yako.Leo,ifanye ni siku ambayo utayatafakari maisha yako na kuanza kuamua mwelekeo wa maisha yako.
See You At The Top
@JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website