Navigate / search

Ufanye Nini ili Kujitoa Katika Tatizo Linalokukabili

Unapokuwa katika mwelekeo wa kutaka kuiishi ndoto yako na kutimiza malengo uliyojiwekea katika maisha yako ni lazima ujiandae kukutana na changamoto kubwa  ambazo kuna wakati zitatishia uwezekano wa wewe kuendelea mbele.Watu wengi sana huwa wakijikuta katika hali za chini kabisa za maisha yao huwa ndio inakuwa mwisho wa wao kuendelea mbele na wanajikuta wamekwama kabisa.Ukifuatilia kila maisha ya mtu ambaye amefanikiwa,utagundua kuwa wote walipitia nyakati ambazo walikuwa chini sana ila kuna mambo ambayo waliyafanya na yakawasaidia kuweza kuinuka tena na kufanikiwa upya.

Akiwa na miaka 21 Steve Jobs alianzisha kampuni ya masuala ya teknolojia ya Apple na alipofikisha miaka 23,kampuni hii ilikuwa na thamani ya mamilioni ya dola za kimarekani.Baad aya hapo aliamua kumuajiri John Sculley ambaye alikuwa ni mzoefu sana katika kuendesha makampuni makubwa.Lakini baada ya miaka mitatu ijayo Steve Jobs alijikuta amefukuzwa kazi katika mazingira tata na akabakia bila kitu kabisa.

Mwaka 2005 wakati anahojiwa kuhusiana na jambo hili alisema “Sikuwa nimewahi kufikiria hapo kabla,lakini kufukuzwa kutoka Apple kampuni ambayo niliianzisha ndio lilikuwa jambo zuri sana kunitokea katika maisha yangu”.Baada ya kufukuzwa,Steve Jobsa alianzisha kampuni  yake nyingine iliyoitwa NeXT na baadaye kampuni hiyo ilinunuliwa na Apple na kisha Steve Jobs akajikuta yuko tena ni Mkurugenzi wa Apple.Na wote tunajua kuwa hadi anafariki alikuwa ni kati ya matajiri wakubwa marekani na duniani.

Huyu si mtu pekee wa kwanza kupitia hali ya namna hii ya kupoteza kila kitu,wako wengi walishawahi kupitia na hali hii haitaisha kwa kuwa ni sehemu ya safari ya kuelekea katika mafanikio ambayo kila mtu lazima apitie kabla hajafika katika kilele cha mafanikio.Nakumbuka mmoja wa wafanyabiashara wakubwa nchini marekani Bwana James Altucher ambaye aliwahi kumiliki kampuni ya Reset Inc,ilipofika mwaka 1998 ilibidi auze kila kitu chake ikiwemo na kampuni aliyoianzisha kwa bei nafuu sana ili aweze kujitoa katika changamoto zilizokuwa zinamkabili na akajikuta amepoteza kila kitu.Lakini baada ya miaka michache aliwez kurudi tena na kurudisha utajiri wake baada ya kuanzisha biashara nyingine.

Swali la msingi la kujiuliza hapa,hivi ni kwa  nini wengine wakianguka huwa hawawezi kuinuka na wengine wakianguka huweza kuinuka kwa haraka?Na  wakati mwingine unaweza ukakuta watu wawili wametokewa na kitu ambacho kinafanana kabisa ila mwingine anapata nguvu na anaanza upya na mwingine anajikuta ndio mwisho wake kabisa na hawezi kuendelea mbele zaidi.

Kwenye maisha yangu binafsi nimewahi kukutana na hali nyingi sana ambazo ukweli ni kuwa wakati nazipitia niliona kama ndio mwisho wa maisha yangu umefika,lakini baada ya muda fulani nilipopita na kushinda nilishukuru kuwa jambo hilo lilinitokea.Magumu mengi ambayo tunayapitia katika maisha yetu,huwa yanakuja kutumika kama daraja la kutusaidia kutoka katika hatua moja kwenda nyingine.Mara nyingi mambo magumu yanatusaidia kufikiri kwa namna ya tofauti na kuchukua hatua amabzo bila changamoto kubwa tusingeweza kuzichukua kabisa.Inawezekana hata leo unapitia changamoto fulani katika maisha yako na uko katika wakati ambao unajiuliza ufanye nini ili urudi tena kuendelea na kutimiza malengo yako.Kuna mambo matatu ambayo kila aliyejikuta ameanguka chini aliyazingatia na yakamsaidia kuinuka tena:

Hatua ya  kwanza ni kufanya uamuzi wa jambo gani ambalo unataka kulitazama katika kipindi cha namna hii.Watu ambao waliweza kuinuka baada ya kupitia changamoto za namna hii walifanya maamuzi ya kutazama katika kutafuta suluhisho ya tatizo linalowakabilia na sio kutafuta mabaye alisababisha tatizo.Huwa wanatumia muda wao mwingi katika kujiuliza-Nitatokaje hapa?Na wakishapata jibu huwa wanafanyia kazi kwa haraka bila kuchelewa.Baada ya Steve Jobs kufukuzwa kutoka katika kampuni yake,hakukaa chini na kuanza kujilaumu ama kumlaumu mtu,alichoamua kufanya ni kujiuliza afanye nini na akaamua kuanzisha kampuni yake binafsi na akaanza kazi mara moja.Kama leo uko kwenye wakati wa chini kabisa,jiulize-“Hivi kuna njia  gani za kutoka hapa?”-Ukishazipata,anza kuzifanyia kazi.Kadiri unavyotumia muda wako mwingi katika kutafakari wa kumlaumu na kujilaumu basi utachelewa kuinuka na kabla haujagundua utajikuta umebakia katika hali hiyo kwa muda mrefu Zaidi.Amua kutazama katika kutafuta suluhisho.

Jambo la pili ni tafsiri unayoiweka katika kile ambacho unapitia ama kimekutokea.Saikolojia ya mafanikio inasema,maisha yetu yalivyo yanatokana na asilimia 10 ya yale yanayotutokea na asilimia 90 ni kile tunachofanya baada ya kutafsiri yale yaliyotutokea.Hii ndio maana kuna wakati nilisikia mwanafunzi amefeli kidato cha nne amejinyonga kwa sababu tafsiri yake ni kuwa kufeli ndio mwisho wa maisha na hakuna kitu ambacho anaweza kufanya tena ili afanikiwe.Lakini kuna watu leo ni viongozi wakubwa na wengine wanamiliki makampuni makubwa waliwahi kufeli kidato cha nne na wakaamua kurudia mitihani na wakafaulu.Tafsiri unayoiweka juu ya kile kinachokutokea ndio hujulisha kama utafanikiwa tena ama la.Kuna watu wakipitia mambo magumu huwa wanatafsiri kuwa Mungu hawapendi,wamezaliwa ili wawe maskini ama wao ni watu wa mikosi na bahati mbaya tu,na kwa sababu hii hujikuta hawawezi kuinuka tena.Ili uweze kuinuka tena ni lazima utafsiir kuwa kila kinachotokea ni changamoto ya maisha ambayo unaweza kupata majibu yake.Hata hali inayokukabili leo unaweza kupata majibu yake pia.

Jambo la tatu ni uamuzi ambao unauchukua kuanzia sasa.Kumbuka kuwa hapo ulipo leo ni kwa sababu ya maamuzi ambayo uliwahi kuyafanya huko nyuma na namna pekee ya kutoka hapo ni kufanya maamuzi mengine ya kubadilisha hali yako ya sasa.Kati ya makosa ambayo watu huyafanya ni baada ya kujikuta wako kwenye changamoto ngumu za maisha huwa hawafanyi maamuzi,huamua kukaa tu na kusubiria mambo yabadilike yenyewe.Kwa hali ngumu yoyote ambayo unapitia-Jiulize leo ni uamuzi gani ambao ukiufanya utabadilisha hali yako ya sasa na uchukue uamuzi huo bila kuchelewa.

Kitabu cha TIMIZA MALENGO YAKO kimechambua mbinu mbalimbali ambazo watu waliofanikiwa wamekuwa wanazitumia ili kufikia kilele cha mafanikio.Unaweza kukipata katika mkoa wowote ulipo,wasiliana nasi kupitia 0655 720 197 na kwa walioko Dar es Salaam unaweza kukipata katika maduka ya vitabu ama ukaletewa pale ulipo kwa bei ileile kupitia namba 0762 224 282.

 

See You At The Top

@Joel Nanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website