Navigate / search

Tujikumbushe Kashfa ya Kagoda kuchota bilioni 40 BOT

bunge

UTATA unazidi kugubika ilipo na anayemiliki kampuni ya Kagoda Agricultural Limited (KAL) ambayo inatajwa kuchota kiasi cha Dola za Marekani 30,732,658.82 (zaidi ya Sh Bilioni 40) kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).Uchunguzi wa muda mrefu wa waandishi wa habari na hata wa makachero kuhusu mmiliki halisi wa kampuni hiyo na zilipo ofisi zake, unaelekea kugonga mwamba.

Kampuni hiyo ambayo kumbukumbu za Msajili wa Makampuni (BRELA) zinaonyesha kwamba ofisi zake zipo Kipawa Industrial Area Plot namba 87, Temeke, Dar es Salaam lakini eneo hilo lina makampuni tofauti jirani lakini na namba hiyo haionekani.

Badala yake wachunguzi wanakuta viwanja kuanzia Plot 77 na hata Plot 86 na Plot 88 katika eneo hilo maarufu la viwanda, lakini plot ilipo Kagoda haionekani popote hata kwa kutumia wataalamu wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

Katika hali isiyo ya kawaida, hata namba za simu na anuani zinagonga mwamba baada ya namba hizo kwa sasa kuwa na wamiliki tofauti lakini wamiliki wa awali wanafichwa ama hawaonekani katika kumbukumbu zozote rasmi mbali ya maneno ya mitaani.

Tayari waliotajwatajwa katika kuhusika na Kagoda wametoa matamko kwa watu mbalimbali na hadharani kwamba hawana uhusiano wowote na kampuni hiyo.

Hao ni pamoja na Mbunge wa Igunga Rostam Aziz ambaye alisambaza matangazo magazetini kiasi cha mwezi mmoja uliopita, akieleza kuwa Kagoda haikuwa kampuni yake.

Katika hatua nyingine, aliyesimamia na kufuatilia pesa za EPA ndani ya BoT na hatimaye kuchukua fedha za kampuni hiyo katika Benki ya CRDB Limited, tawi la Azikiwe, anajulikana waziwazi na wafanyakazi wa maeneo hayo, lakini kumbukumbu zake zinaelezwa kupotea ama kufichwa na wahusika kwa nia ya kuwasaidia watuhumiwa ama kwa sababu za kichunguzi.

Hata hivyo, inaelezwa kwamba wapelelezi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) walikwisha kuchukua nyaraka zote muhimu ikiwa ni pamoja na kadi ya benki iliyotumika kufungulia akaunti tawi la Azikiwe, ikiwa na picha na saini za wahusika wote muhimu kwa uhakiki zaidi.

Sakata la BoT, na zaidi akaunti ya EPA, limechukua sura mpya baada ya kuelezwa kwamba sasa mkakati wa Serikali ni kuhakikisha fedha zote kiasi cha shilingi bilioni 133 zinarejeshwa kabla ya kuchukuliwa hatua kwa wale waliofanya makosa ya kijinai katika kupata fedha hizo.

Imeelezwa katika hali ya kutatanisha kwamba tayari hata fedha kutoka kwa wamiliki wa Kagoda nazo zimekwishakuanza kurejeshwa japo kwa awamu, jambo linalodhihirisha kwamba Serikali inawafahamu kwa hakika kabisa wamiliki wa Kagoda na inawaficha ama inataka kuwalinda kwa sababu zilizodhahiri kwamba ni za kisiasa zaidi.

Katika uchunguzi wa awali wa mkaguzi wa nje, Samuel Sithole, kutoka kampuni ya kimataifa ya Deloitte & Touche yenye makao yake Afrika Kusini, alionya kuhusu matendo ya kihalifu ndani ya Kagoda kabla ya kuandikiwa barua na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji kwamba fedha hizo zilienda katika mambo “nyeti” ya kiusalama.

Hata hivyo, siku nne baada ya kuandika barua hiyo, Meghji alifuta barua hiyo akielezea kupotoshwa na aliyekua Gavana, Dk. Daudi Ballali, uamuzi ambao ulimgharimu kwa kiasi kikubwa mwanamama huyo ambaye sasa ameachwa nje ya Baraza la Mawaziri.

Hatua ya kuelekeza suala hilo la akaunti ya EPA katika kufidia zaidi inaelezwa kuwa ya makusudi ya kutaka kunusuru wahusika, lakini pia hata Serikali yenyewe na hasa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho taarifa zinaonyesha kwamba sehemu ya fedha hizo ziliingia katika uchaguzi wake.

Lakini wachunguzi wanasema hata kama hatimaye suala hilo litakuwa limefikia ukomo kwa wahusika kulipa fedha walizochota, bado mbele ya safari suala hilo itabidi liibuke tena.

Wanasema linaweza kuibuka kwa kuangalia nyaraka zilizoghushiwa kwa kuwa kosa la kughusi ni zito na lenye kubeba adhabu kubwa zaidi.

“Wanaahirisha tu tatizo. Hapa suala si wingi wa fedha wala nani aliyekwiba. Tatizo ni kwamba watu hawa walighushi nyaraka. Kwa vyovyote vile kughushi ni kosa zito na tutashangaa kama upelelezi hautaelekezwa katika eneo hilo”, anasema mtaalamu mmoja wa fedha ambaye hakutaka kutajwa.

Anaongeza: “Hawa watu walidanganya, wakaiba. Hii si kesi ya madai. Wanastahili kushitakiwa.

Kwanza ungetarajia wangechukuliwa hatua za kushitakiwa kwa sababu walighushi nyaraka. Hilo linalofanywa sasa la kutaka walipe tu fedha lingekuja baada ya hukumu ya suala la kughushi.”

“Dhahiri hii ni moja ya njia ya kutaka kuwalinda watu. Na kama inavyosemwa hawa watakuwa ni watu wakubwa. Sasa hii inaonekana kuwa kesi ya madai badala ya kuwa kesi ya jinai. Kwanza wengine tunaambiwa hata hayo madeni hayakununuliwa,” alisema.

Chanzo:Raia Mwema(February 27,2008)

Leave a comment

name*

email* (not published)

website