Navigate / search

Tanzania imeamua kuongeza maadui zaidi?

Nchi yetu imesifika kwa Muda mrefu sana katika kuwa na mahusiano mazuri na majirani na hata wasio majirani kwa jiografia bali wanaojulikana kama wadau wa maendeleo(Development Partners).Ingawa ni ukweli usiopingika kuwa urafiki huu na majirani zetu haujawahi kudhoofisha hata wakati mmoja uwezo wetu kama nchi kusimamia mambo ya msingi tunayoyaamini kuwa ni misingi yetu muhimu katika kutekeleza sera yetu ya mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa.

Kati ya mambo yanayoelezwa kuwa ni misingi ya sera yetu ya mambo ya nje ni kuendeleza ujirani mwema. Ni misimamo hii ndiyo ilitufanya tuwe wakosoaji wakubwa wa serikali ya kibaguzi ya Afrika kusini kiwango cha kukataa hata kuwa na mahusiano nao kibiashara.Na kwa kuuonyesha kuwa hatukuwa tunaichukia nchi bali tulikuwa tunapinga mfumo kandamizi,leo hii Afrika kusini ni mshirika wetu namba 3 katika uwekezaji Tanzania,makampuni yake yakiwekeza kiasi cha asilimia 31.2 ya uwekezaji wote wa moja kwa moja(Foreign Direct Investiment) hapa nchini.

Kwa muda mrefu tumekuwa tunalaani matendo maovu ya nje,na kwa uhalisia wa diplomasia yale tunayoyasimamia nje yanatakiwa yaakisi yale tunayoyasimamia ndani.Tulikuwa mstari wa mbele kulaani uingiliaji wa NATO katika nchi ya Libya na pia tulisimama kinyume na marekani tukaunga mkono wapalestina kuwa sehemu ya UNESCO.Misimamo hii katika jumuiya ya kimataiffa imetupa heshima kama nchi na pia imetufanya watanzania kuaminika katika majukumu mbalimbali ya kimataifa.Hii haishangazi kwani tuliona jinsi Dr.Asha Rose Migiro alivyotuwakilisha alipoteuliwa kuwa naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa,Mama Tibaijuka alipokuwa mkurugenzi wa UN-Habitat na hata Getrude Mongela alipokuwa rais wa bunge la Afrika.

Hata hivyo uhusiano na majirani zetu kijiografia kwa muda mrefu umekuwa ni mzuri ukiacha visa vichache.Vita kati yetu na Idd Amini inaweza ndio kusemwa kuwa ni dosari kubwa katika mahusiano yetu na majirani.Hata hivyo uhusiano wetu na Dr.Hasting Banda wa Malawi haukuwa mzuri na ni ukweli kuwa kumekuwa na misuguano ya kujirudia hasa kuhusu umiliki wa ziwa Nyasa linalojulikana kama ziwa Malawi kwa upande wa Malawi.Hivi karibuni baada ya Prof:Bingu wa Mutharika kutangazwa kuwa Rais wa Malawi nilitamani kujua zaidi sera yake kuhusu ziwa Nyasa,ndipo nilipokutana na habari iliyochapishwa na nyasa news mwaka jana August 3,2013 ikieleza kuwa kama angechaguliwa kuwa rais basi hakuna mjadala juu ya ziwa nyasa kwa kuwa ziwa hilo lote ni la Malawi na hakuna hata inchi moja ni ya Tanzania.Hapa ni kusema kuwa kwa ushindi wake tumeingia katika msuguano mwingine kam alivyokuwa mtngulizi wake Rais Joyce Banda.

Msuguano na majirani ama mataifa mengine ni jambo linaloweza kutokea ila namna tunavyojibu au aina ya mwitikio wetu ni jambo la msingi zaidi.Ningependa katika mtazamo wa leo tuangalie jinsi ambavyo tunajiingiza katika msuguano hatarishi kati yetu na “mdau wa maendeleo” uingereza na hasara yake katika juhudi zetu za kujenga uchumi wetu.

Ningeanza kwa kusema kuwa kwa sasa Tanzania tunajivunia kufuatilia utekelezaji wa sera yetu ya mambo ya nje ya diplomasia ya uchumi kama ilivyoundwa mwaka 2001.Katika aina hii ya diplomasia,faida za kiuchumi ni za muhimu zaidi kuliko faida nyingine yeyote ile.

Ugomvi wetu na Malawi kuhusu ziwa nyasa hivi karibuni haukuwa ugomvi na nchi hiyo peke yake,kulikuwa na nguvu ya ziada nyuma yake.Baada ya mwezi Oktoba 2011 serikali ya Malawi kutoa taarifa kuwa imetoa kibali cha utafiti wa mafuta kwa kampuni ya Surestream Petroleum ya uingereza hapo ndipo changamoto ilipoanza,hasa mara baada ya waziri wa Mambo ya nje Bwana Patrick Kabambe kutangaza kuwa ziwa lote ni la Malawi na hawataacha na shughuli ya utafutaji wa mafuta hata baada ya kupewa wito wa kufanya hivyo na Tanzania.Ukweli wa kwamba kampuni ya uingereza ndio yenye interest katika kufaya uchimbaji huo ni ukweli usiopingika kuwa serikali ya uingereza ilikuwa nyuma yake kuisaidia katika kupata tenda hiyo.Ni vyema kukumbuka kuwa katika diplomasia ya uchumi,serikali huwa bega kwa bega katika kusaidia makampuni yanayotokea katika nchi zao kufanikiwa kibiashara wanapokuwa katika nchi za kigeni.

Baada ya tamko la Malawi kazi ilibakia kwetu kueleza msimamo wetu kuhusiana na hili.Kamati ya bunge ya ulinzi,usalama na mambo ya nchi za nje kupitia mwenyekiti wake Mh.Edward Lowasa aliwahi kusema “kibidi kuingia vitani jeshi letu liko vizuri sana,na kama ilivyo ahadi yao(JWTZ) wako tayari kulinda mipaka ya nchi yetu hadi tone la mwisho.Tunasali sana tusifike hapo”.Hii ilikuwa baada ya kkufanya kikao na viongozi waandamizi wa jeshi kule Dodoma,sina hakika kama kliikuwa kikao maalumu cha kujadili ajenda ya ziwa nyasa ama la,lakini ho ndio ulitolewa kama msimamo wetu.

Hii haikuwa kauli ndogo na nyepesi.Ingawa sijui madhumuni yalikuwa nini naamini ilikuwa na madhara makubwa sana katika kuendeleza mtafaruku huu.Hata baada ya waziri wa mambo ya nje kuja kueleza nia yetu ya kusuluhisha mgogoro huu kidiplomasia,tayari kulikuwa na hali ya mvutano(tension) miongoni mwa seriakali hizi mbili.Je,kulikuwa kuna umuhimu wa kutamka utayari wa jeshi letu katika mgogoro huo?.Nijuavyo mimi katika uhusiano wa nchi,matumizi ya jeshi huwa ni chaguo la mwisho kabisa katika kutatua changamoto hasa pale tunapoona kil kitu kimeshindikana.Lakini hii inatuonyesha mwelekeo mpya wa namna tunavyohusiana na majirani zetu kwa kuamini katik matumizi ya nguvu na tuhuma.

Jazba za namna hii zilijitokeza hata katika majadiliano ya nafasi yetu kwenye jumuiya ya Afrika mashariki.Pale tulipoona ushirika wa walio tayari(Coalition of the willing) walipoanza kuwa na vikao na kutuacha solemba,mtakumbuka kauli za mawaziri wetu bungeni-Waziri Membe alisema tuko tayari kwa talaka,Mheshimiwa Sitta akasema sisi ndio tutakaotoa talaka kwani sisi ndio tumeoa.Na kuthibitisha hilo akasema kuwa sisi tunamiliki 52% ya eneo lote la jumuiya na tayari tumeanza na mazungumzo na Burundi kuimarisha uhusiano wetu.Kwa maneno mengine—Wametutenga nasi tumeamua kuwatenga–Ukifuatilia mazungumzo haya utagundu kuwa tulikuwa tunaendesha matamko ya lawama na shutuma kwa majirani zetu kuwa tunaonewa na kutengwa.Mwisho wa siku Rais Kikwete alilazimika kutumia hotuba yake ya bunge ili kuzima mvutano huu uliokuwa unaendelea kupamba moto.

Mambo haya yalitokea baada ya msuguano mkali unaoendelea kati yetu na nchi ya Rwanda,msuguano ulioanza baada ya Rais Kikwete kutoa ushauri kwa Rwanda kuwa waongee na waasi wa FDRL walioko DRC ili wamalize tofauti zao.Hali hii ilikolezwa tena Bungeni baada ya hotuba ya waziri Kivuli wa mambo ya nje kukumbushia jinsi waziri Membe alivyotamka kuhusu msaada wa Rwanda kwa Kikundi cha M23 na kuwa kiongozi wa FDLR Twigiramungu alikuja Tanzania na alihaidiwa kupew msaada wa Kuing’oa serikali ya Rwanda.Mara Moja waziri wa mambo ya nje ya Rwanda alijibu tuhuma za kuhusishwa na M23.Waziri Membe amekiri bungeni hivi karibuni kuwa uhusiano wetu na Rwanda unapitia wakati mgumu.

Hivi karibuni kama nchi tumejiingiza katika dimbwi lingine la siasa ya lawama kwa marafiki zetu.Mara hii tumevuka mipaka na kutua uingereza.Waziri wa Nishati na Madini Stephen Masele ameshusha lawama nzito kwa balozi wa uingereza hapa nchini Dianna Malrose.Kati ya lawama alizotoa ni pamoja na kusem kuw hivi karibuni Mkurugenzi wa UNDP duniani, Hellen Clark, alikuja Tanzania na kukutana na balozi huyu, kufuatia mazungumzo yake amekuwa akiishauri Marekani kutotoa fedha zake za MCC2 zinazojenga barabara mkoani Tanga.Na pia alieleza kuw inasikitisha na kuchukiza balozi wa taifa kama Uingereza akifanya vitendo kinyume cha maadili(kwa maneno mengine hafai kuwa balozi).Lawama zaidi alizielekeza na kusema kuwa anahusishwa kushawishi marafiki wa maendeleo wasitishe misaada ya kibajeti kwa Tanzania.

Kama vile haitoshi Waziri Masele aliendelea kusema kuwa ni aibu kwa serikali ya Waziri Mkuu, David Cameron kwa balozi wake kufanya uwakala wa Benki ya Standard Chartered, kuishawishi serikali ya Tanzania ikope fedha ili kulipa kampuni binafsi.Hizi ni lawama nzito na zinazohatarisha mahusiano kati yetu na nchi ya uingereza.

Na huu ni mwendelezo wa siasa za lawama na malalamiko ambazo tumeanza kuzikumbatia.Waziri masele hakuwa na sababu wala mamlaka ya kutoa tuhuma hizo mbele ya bunge hasa kwa kuzingatia kuwa ni jambo la kidiplomasia.Kwa utaratibu wa kawaida suala hili katika uzito huu lilikuwa linatakiwa lifikishwe kwa waziri wa mambo ya nje naye atajua namna ya kufikisha moja kwa moja au kumuhusisha Rais kadiri atakavyoona inafaa.

Na hili lilijidhihirisha wazi pale ambapo Ikulu kupitia Balozi Sefue Ombeni walikana kufahamu ttuhuma hizo na pia wizara walimtaka waziri huyo kufikisha tuhuma hizo rasmi wizarani.Ofisi hizi mbili zinajua umuhimu wa mdau huyu katika maendelo ya nchi yetu na hususani wizara ya Nishati na Madini ambapo uingereza ni wadu katika kusaidia mradi w umeme vijijini.

Uingereza ni Mdau mkubwa katika program za maendeleo kwa miaka takribani 35 kupitia kitengo chake cha maendeleo ya kimataifa DFID(Department for International Development).Katika ripoti ya mwisho ya uwekezaji ya TIC inaonyesha kuwa Uingereza ni kati ya wawekezaji wakubwa sana nchini(wengine ni Afriak ya Kusini na Canada) wanaotengeza asilimia 71.5 ya uwekezaji,hivyo ni muhimu sana kwetu.Kwa uzito huu,ni lazima ikulu imkane waziri Masele.

Swali kubwa la balozi lililowaudhi viongozi wetu ni pale balozi Malrose alipotaka uchunguzi juu ya pesa za akaunti maalumu ya Escrow ambako zilihamishwa shilingi bilioni mia mbili kinyume na utaratibu.Balozi huyu aliandika barua rasmi kwa serikali yetu kuonyesha kusikitishwa kwake na alipelekankala kwa nchi kadhaa za ulaya kuwajulisha masikitiko yake.Badala ya kupata majibu rasmi ya wizara,amejikuta anatupiwa lawama nzito tena ndani ya bunge ambakko asingeweza kujitetea.

Labda jambo la kujikumbusha ni kuwa ni nchii hii ya uingereza inayolaumiwa kuingilia mambo ya nchi yetu ndiyo ilitusaidia kupata chenji ya rada tuliyoitumia kununu vitabu mashuleni.Wakati sisi tumekaa kimy na rada imenunuliw kwa bilioni 29.5 badala ya bilioni 21,ni serikali ya uingereza ndio ilitusaidia kupata ziada ya pesa.Na hii ni kwa sababu kampuni iliyohusika na uuzaji w rada hiyo ni BAE Systems ya uigereza.Wakati wanafuatilia rushwa hii na kuturudishia chenji tulifurahi na hakun aliyelalamika kuwa tunaingiliwa uhuru wetu.Leo watu hao hao wnazungumza kusikitishwa kwo tunaanza kusema wananingilia uhuru wetu.

Kwa mtazamo wangu wanazo sababu mbili za kufuatilia mchakato wa fedha za Escrow.Moja ni kwa kama vile ambavyo BAE kampuni ya uingereza ilivyokuwa inabeba jina la nchi yao na wakataka kujisafisha kwa kurudisha ziada ya fedha ndivyo ambavyo Barclays ambako akaunti ya Escrow ipo inawahusu,wanataka isichafue taasisi zingine zenye asili ya kiingereza katika kusaidia makampuni yao kibishara nje ya nchi.Lakini pili,kama watu wanatusaidia fedha nyingi na miradi mingi halafu wanaona pesa zinachotwa kiholela tu,kwa nini wasihoji?Ni sawa na kusema wanachangia huku,wengine wanatoa huku,matokeo ya jumla yatakuwa ziro kabisa.

Kwa majirani zetu Malawi na Rwanda zote ni nchi zisizo na toleo la bahari(landlocked) hivyo zinatengeneza fursa kubwa kutumia bandari zetu kwa kuigizia mizigo yao,jambo linalotengeza ushuru kwetu.Hata kama tuantofautina nao katika mambo Fulani lakini kwa sababu za faida a kiuchumi inatulazimu kupunguza tofauti zetu na kuongeza ukaribu wetu.

Kwa upnde wa uingereza hawaitaji kutumia bandari zetu,ila tunawahitaji katika shughuli za maendeleo na uwekezaji.Ukweli ni kwamba kama hatutataki watuwajibishe tunapovurunda,basi tuwe wajasiri kukataa pia misaada mingine wanayotupa.Kujaribu kutumia lawama na siasa za vitisho haitasidia kuondoa nafasi yetu ya kuwajibika.

Kabla ya lawama na vitisho haijawa staili rasmi ya kuendesha mahusiano yetu na nchi nyingine ni vyema tukarudi katika msingi wa mahusiano yetu na marafiki zetu kwa kuonyesha uwezo wetu katika kusimamia yaliyo sawa na tunayoweza kujivunia.Tutumie nguvu za hoja katika kuboresha mahusiano yetu na sio kuyabomoa.

Leave a comment

name*

email* (not published)

website