Navigate / search

SIRI TATU TOKA KWA DEBBIE ZINAZOWEZA KUKUFANYA UTIMIZE MALENGO YAKO.

secret

Ili ufanikiwe unahitaji kuwa na mjumuiko wa sifa nyingi sana ambazo zote zinachangia kukusaidia kutimiza malengo yako.Hata hivyo kati ya sifa kuu unazotakiwa kuwa nazo,mojawapo ni ile ya uwezo wa kuiamini ndoto yako na kuamua kuvumilia kuifuatilia kwa muda mrefu hadi itakapofika kipindi ambacho umepata matokeo ambayo unayataka.Norman Vincent Peale aliwahi kusema,”It is always too soon to quit” (Kila wakati amua kutokata tamaa mapema).Kati ya sifa ambayo unatakiwa kuwa nayo katika maisha yako ni kuiamini ndoto yako katika wakati ambapo mazingira yanaonyesha unatakiwa usiiamini.

Debbie Macomber alipoamua kuwa mwandishi wa vitabu aliamua kununua “Typewriter”(machine ya kuchapa) na akaanza kuitumia nyumbani kwake.Alichokuwa anafanya kila siku asubuhi baada ya kuwapeleka watoto wake shuleni alikuwa anarudi na anaanza kuandika na mara baada ya kumaliza kula usiku kila mtu akienda kulala alikuwa anarudi sebuleni kuendelea na kuandika.Kwa muda wa miaka miwili na nusu,Debbie alifanya hivi bila kuchoka na anasema alikuwa anafurahia kila dakika aliyokuwa anaitumia kuandika.

Siku moja usiku mume wake akiwa amechoka baada kufanya kazi mchana kutwa aliamua kuongea na Debbie na kumwambia kwa sauti ya upendo kabisa-“Mpenzi umefanya kazi hii ya kuandika kwa miaka miwili na nusu sasa na hakuna matokeo yoyote uliyopata,ningependa kukushauri kuwa utafute kazi nyingine ya kufanya ambayo itaweza kukuingizia kipato kizuri ili tuweze kutunza watoto vizuri”.Debbie akamjibu mumewe na kumwambia-“Ahsante sana mume wangu kwa kujali hilo,ila unaweza kunipa muda kidogo zaidi niendelee kuifuatilia ndoto hii kwani ndio kitu ninachokipenda zaidi”.Mume wake akionyesha kutofurahishwa kabisa na majibu ya Debbie hakumjibu,aliondoka na kutangulia kulala.Baada ya muda Debbie alienda kulala naye lakini alikosa usingizi kabisa usiku kucha.Mume wake akihisi mkewe anajigeuza tu na amekosa usingizi,akaamua kuamka na kuwasha taa na akamwambia-“Debbie,nakubaliana na wewe,endelea kuifuatilia ndoto yako”.
Baada ya kupata ruhusa ya mume wake,Debbie aliendelea na utaratibu wake wa kuendelea kuandika na akaongeza masaa aliyokuwa anaandika na kusoma zaidi.

Bidii yake iilikuja kuanza kutoa matunda ilipofika kwenye mwaka wa 5 pale alipofanikiwa kupata kampuni ya kumsaidia kuchapisha kitabu chake cha kwanza.Baada ya kitabu chake cha kwanza kufanikiwa aliendelea kuandika vingine na hadi leo ana vitabu zaidi ya 100 ambavyo ameshaviandika na kati ya hivyo kuna vitatu ambavyo vimetengenezewa filamu zake.Kwa sababu ya mafanikio hayo,mume wake aliyeamua kumpa sapoti ya kutimiza ndoto yake,aliweza kustaafu ajira akiwa na miaka 50 na sasa wanaishi katika jumba la kifahari na watoto wao wamesoma katika vyuo bora kabisa duniani.

Hakuna ndoto ambayo huwa inafanikiwa kirahisi,hakuna lengo ambalo halihitaji uvumilivu na mara nyingi utahitaji kuiamini ndoto yako hata kipindi ambacho kila mazingira yanaonyesha utakuwa umefanya vyema kama ukikata tamaa.Watu wengi sana huwa wanakata tamaa baada ya kuweka nguvu zao mahali kwa muda fulani kisha wasipoona matokeo kwa uharaka waliokuwa wanautarajia basi wanamua kuachia njiani.

Kuna mambo kadhaa tunaweza kujifunza kutokana na mafanikio ya Debbie.Jambo la kwanza ni kuwa baada ya kuamua kuchagua jambo analotaka kulifanya katika maisha yake aliamua kuchukua hatua na kuanza.Ingawa alikuwa hana uwezo wa kupata ofisi kwa wakati huo ama kupata mashine nzuri;aliamua kutumia meza yake ya chakula kuwa ndiyo ofisi na kuanza kufanya kile alichokiamini kuwa ndicho kitu sahihi kukifanya kuhusiana na ndoto yake.Kila lengo ulilonalo na ndoto unayotaka kuja kuiishi lazima ina mahali pa kuanzia.Kati ya vitu ambavyo vinawakwamishwa watu kufanikiwa haraka,ni kushindwa kwao kuanza na kile walichonacho na pale walipo,huwa wanasubiri vikubwa.

Sijajua una ndoto gani ambayo unataka kuitimiza katika maisha yako,sijajua mwaka huu umejiwekea lengo la aina gani-Lakini ambacho nina uhakika nacho ni kuwa lazima kuna sehemu ya kuanzia.Inawezekana,usiwe na kiwango cha mtaji ambacho unataka,ama mshahara ni mdogo unaolipwa sasa ama hata hauna kazi kwa sasa-Ninachojua ni kuwa kuna hatua ndogo ambayo unaweza kuianza kuiishi ndoto yako na mara zote lazima kuna hatua ambayo haihitaji pesa.Inawezekana ikawa ni kumpigia mtu simu kupata ushauri,inawezekana ni kuhudhuria semina na mafunzo kuongeza ujuzi ambao unauhitaji na ziko semina ambazo hauhitaji kulipia(huwa natoa semina hizi kila mwezi),inawezekana ni kuanza kuandika mipango yako ama kusoma kitabu-Kwa vyovyote itakavyokuwa hebu leo jiulize-“Kwa hili lengo nililo nalo kuna hatua gani ambayo naweza kuanza kuichukua leo?”

Jambo la pili ni kuwa lazima uwe tayari kuendelea kufanya hata wakati ambapo unaona matokeo bado hayaridhishi.Swala la muhimu zaidi katika ndoto ni kuwa na uhakika kuwa unachofanya ni sahihi na kuamua kuwa hayo ndiyo maisha yako.Ukishaamua kwa kiwango hiki basi pasi na shaka mafanikio yatapatikana.Debbie ilimgharimu miaka 5 kufanikiwa,sina uhakika na wewe itakugharimu miaka mingapi hadi umefikia lengo lako.Mara nyingi,ndoto kubwa na za muhimu kwenye maisha yetu huwa zinachukua muda na ni lazima tuwe wavumilivu hadi tuone zinatimia.Wakati unaendelea kusubiri zitimie,unachotakiwa kufanya ni kuendelea kuweka bidii katika mwelekeo wa ndoto yako,Usikate tamaa,

Tatu ni lazima tuwe tayari kuiamini ndoto yetu hata wakati watu wengine wameanza kukosa imani na uwezekano wake.Mara nyingi kuna watu watatuambia tena kwa upendo kabisa kuwa tuachane na kile ambacho tunakifanya sasa kwa sababu hakijaweza kutuletea matokeo tuliyokuwa tunayataka kama ilivyokuwa kwa mume wa Debbie.Katika nyakati kama hizi ndio tunatakiwa kuthibitisha kuwa ndoto tulizonazo ni kweli zimetoka moyoni ama zimetokana na hamasa tu ya muda mfupi.Kama ndoto yako ni ya kweli basi hata kipindi ambacho hakuna mtu ambaye atakuwa anaweza kuiamini,wewe mwenyewe utakuwa na uwezo wa kuiamini.

Je,unayo ndoto kama alivyokuwa nayo Debbie?Je uko tayari kuvumilia hadi itimie?.

Kumbuka Kuwa ndoto yako Inawezekana,
Endelea kutembelea www.JoelNanauka.Com ili kujifunza zaidi.
See You At The Top

Leave a comment

name*

email* (not published)

website