Navigate / search

Sehemu Ya 4:Kwa nini Mkulima Mwamwindi alimuua RC Dr.Kleruu?

mWAMWINDI

Hivi Iringa ya wakati ule ilionekanaje, unakumbuka? Namwuliza Mzee Nzowa.” Mji huu wa Iringa ulikuwa mdogo sana, wengi tulikuwa tunajuana. Hebu ngoja nipekue kwenye kabati langu kuona kama nina picha za zamani”. Mzee Nzowa anainuka kitini. Anakwenda kupekua picha za zamani. Nasubiri kwa shauku.

Wakati tukimsubiri Mzee Nzowa, Jumatatu moja usiku napokea simu kutoka Uingereza; “Ebwana Maggid, niko Uingereza, nafuatilia kisa hiki cha Mwamwindi na Dk. Kleruu. Mimi nilikuwa kijijini Nyang’olo wakati wa tukio lile. Ni kijiji cha jirani na alikoishi marehemu Said Mwamwindi. Nilikuwa na miaka 10. Nakumbuka mambo mengi sana, hata Dk. Kleruu nilimwona, alipenda sana kuja Nyang’olo. Sasa unasikia….”

“Dk. Kleruu alikuwa akija na gari lake. Nyang’olo ni mji wa barabarani. Unajua ndio ilikuwa njia kuu ya kwenda Dodoma mpaka Arusha. Kulikuwa na biashara sana. Kulikuwa na wasomali hata waarabu. Nakumbuka Dk. Kleruu alikuwa akishika kifimbo chake na kuwafokea wazee juu ya mambo ya maendeleo. Kwa kweli wazee wa Nyang’olo hawakumpenda Kleruu,” anasema msomaji huyu ambaye sasa ana miaka 50 na anaishi nchini Uingereza.

Na wakati tukiendelea na simulizi hii ya Mwamwindi zimenifikia habari mbaya. Ni taarifa ya msiba wa Mzee Augustino Hongole Mzee Hongole ambaye, hadi kifo chake alikuwa mwenyekiti wa Bodi ya Uhariri wa gazeti la Kwanza Jamii, Njombe amefariki majuma mawili yaliyopita. Amezikwa kijijini kwao Lupembe., Njombe.

Kwangu mimi, Mzee Hongole ni mmoja wa wazee waliochangia sana katika kuifanya simulizi hii iwe na maana kubwa. Maana, katika utafiti wangu juu ya kisa hiki cha Mwamwindi na Mkuu wa Mkoa Dk. Kleruu, nimepata bahati ya kufanya mazungumzo marefu ya ana kwa ana na hata kwa njia ya simu na marehemu Mzee Hongole.

Na kweli mwandishi wa habari mwandamizi wa magazeti ya HabariLeo na Daily News, Beda Msimbe ndiye aliyenisisitiza sana umuhimu wa kumhoji Mzee Hongole huku kaka yangu Msimbe akisema; “Usichelewe sana, maana wazee hao ndio wanaondoka taratibu”.

Na hakika nimefanya jitihada za ziada za kupokea simulizi za Mzee Hongole juu ya anachokikumbuka katika wakati ule wa tukio.

Na katika hili la simulizi ya Mwamwindi mchango wa marehemu Mzee Hongole ni mkubwa sana. Mzee Hongole amechangia kutoa elimu kubwa ya kimapokeo. Hakika, nina maelezo mengi ya Mzee Hongole ambayo nimeyahifadhi kwa simulizi za baadae.

Huko nyuma nimewahi kusimulia yafuatayo niliyoyapokea kutoka kwa Mzee Hongole juu ya tukio la mkulima Mwamwindi kumpiga risasi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Kleruu.

Mzee Hongole aliyepata kuwa mwandishi wa habari kijana sana wakati wa tukio la Mwamwindi kumuua Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Kleruu lililopotokea anasema; “Ndio kwanza nilikuwa nimepangiwa kufanya kazi kama mwandishi wa habari kwenye gazeti la Kanisa pale Iringa.

“Lilikuwa tukio kubwa sana. Kama mwandishi nilitamani kuandika kilichotokea na kupata maoni ya watu wa Iringa na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla. Kwa wakati ule mfumo haukuruhusu kitu kama hicho. Mwamwindi story was an embargoed one (Stori ya Mwamwindi ilikuwa haiandikiki). Lakini nataka kukwambia: “Watu wengi wa Iringa hawakumpenda Dk. Kleruu kutokana na unyanyasaji wake”.

Mzee Hongole anazidi kusema; “Unajua wakati huo kulikuwa na hofu kubwa juu ya dola. Waliokuwa tayari kumtetea Mwamwindi hadharani walihofia kukamatwa na makachero. Na mimi kalamu yangu ikawa nzito kwa kuogopa jela.

Lakini, kikubwa ni kuwa watu wa kanda hii walikuwa wamoja katika kumuunga mkono Mwamwindi. Shida kubwa ilikuwa kwenye uUtekelezaji wa Azimio la Arusha. Utekelezaji ule kwa mtazamo wangu ulifanywa kimakosa katika maeneo mengi ya nchi ikiwamo kanda yetu hii. Wananchi hawakuulizwa wanataka nini. Walilazimishwa tu na viongozi.

Nakumbuka kule Ilembula kuna wanafunzi waliolazimishwa baada ya masomo waende wakapande miche ya kahawa kwenye shamba la kijiji. Wazazi hawakupenda kilimo cha kahawa, lakini, Serikali ilitaka walime kahawa. Basi, ikatokea, kwa wazazi kuwaambia watoto wao, kuwa wakifika shambani waigeuze miche ya kahawa. Wapande juu chini. Hivyo hawakupanda, walipandua,” anasema Mzee Hongole.

Mzee Hongole anaendelea kusema; “Unajua ni mazingira kama hayo ndio yaliyochangia uzalishaji upungue. Wananchi walijisikia kushurutishwa. Hawakufanya kazi kwa moyo. Na vyombo vya habari navyo havikuwa huru kuweza kuelezea hali halisi za wananchi. Hapa utaona jinsi tulivyokuwa, kama taifa, tukitoka kwenye reli. Maggid, nawaonea wivu sana katika wakati wenu huu kama wanahabari.

“Sisi tulisomea taaluma hii. Tena mimi nilipelekwa na Kanisa mpaka Sweden. Lakini, taaluma zetu zikaishia kufanya kazi ya kusifia Serikali tu, hata kwa mambo ya kipuuzi yaliyofanywa na baadhi ya viongozi. Wakati huo wa tukio la Mwamwindi watu wengi walikuwa na hamu ya kutaka kuujua ukweli. Lakini, sisi wanahabari tuliogopa hata kufika kijijini kwa Mwamwindi kuwahoji waliokuwepo siku ya tukio”

Mzee Hongole anasisitiza kwa kusema kuwa wakati umefika kwa Watanzania kuipitia upya historia yao. Hii itasaidia kuwafanya vijana wa kizazi hiki kujitambua. Watajenga mioyo ya uzalendo na kuwa tayari kuipigania nchi yao.

“Mimi nina shaka kuwa vijana wa siku hizi wamekosa kujiamini kwa vile hawajitambui. Hawaijui historia yao. Wana kiu ya kutaka kuifahamu historia yao. Ni kazi yenu nyinyi waandishi vijana kufanya tafiti juu ya historia yetu na kuisimulia,” anasema Mzee Augustino Hongole. . Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi, Amen.

Inaendelea

Mwandishi:Maggid Mjengwa

Leave a comment

name*

email* (not published)

website