Navigate / search

Sabasaba – Kutoka siasa ni kilimo, hadi siasa ni biashara

Siku moja nilimuuliza mtu ninayemuheshimu na kumuamini sana swali;Hivi kwa nini siku ya wakulima ilihamishwa kutoka sabasaba hadi nanenane?Kwa nini wasingeanzisha siku mpya ya biashara iwe nane nane na sabasaba ikabaki ni maadhimisho ya kilimo?Ukweli ni kwamba alikosa jibu la kuniambia zaidi ya kusema ni uamuzi wa serikali.Ukweli ni kwamba hakuna sababu yoyote ya kihistoria ya tarehe 8 mwezi wa 8,bali siku ya tarehe 7 mwezi wa 7 ni siku muhimu sana katika historia ya nchi yetu.

Wakati naendelea kutafakari zaidi nikagundua kuwa wakulima wa nchi yetu ni kati ya kundi nyonge sana katika kufanya maamuzi yao wenyewe.Hawana sauti bungeni wala mtaani,ingawa ni wengi lakini hawawezi kuamua kuhusu mambo yao.Na kwa sababu ya kutaka kujua zaidi nikaamua kufanya “upembuzi yaakinifu” kuhusiana na historia ya siku hii na nini kilichojiri mpaka kutoka kuwa siku ya wakulima hadi maonyesho ya biashara.

Tarehe 7 mwezi wa 7 ni tarehe muhimu katika historia ya siasa ya nchi yetu.Ikumbukwe kuwa chama cha TANU(Tanganyika African National Union) kilianzishwa rasmi tarehe hiyo mara baadaa ya kuungana kwa chama cha Tanganyika African Association(TAA) na African Association(AA).Ili kuendeleza kuimarisha chama hiki pamoja na kukumbushia umoja wa nchi,tarehe hii ilianza kusherehekewa kama sikukuu ya kitaifa kila mwaka.Umuhimu wa sherehe za sabasaba uliongezeka pale ambapo TANU iliweza kuleta uhuru kamili wa kisiasa wa Tanganyika.Hivyo basi ili kukumbusha juhudi za mapambano ambayo waasisi na wananchama wa TANU walizifanya,ilibidi kuweka mwendelezo wa maadhimisho ya siku hii muhimu ya kuzaliwa kwa chama kilichotuletea uhuru wetu.Hii ilisaidia kuendelea kuwakumbusha vizazi vilivyokuwa vinafuata tulikotoka na wajibu wao wa kuleta mabadiliko kwa ajili ya kizazi chao na kile ambacho kitafuata.

Mara baada tu ya uhuru TANU na serikali yake ilihimiza sana kilimo kuwa ndio njia pekee ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi wote wa Tanganyika.Ili kufanikisha hilo serikali ilitangaza kauli mbiu ya SIASA NI KILIMO(Sio siasa kwenye kilimo) wakati wa azimio la Iringa la mwaka 1972.Tamko hili halikuwa ni kauli mbiu ya kupatia kura ,ama ya kuleta vibwagizo mikutanoni,la hasha ilikuwa ni falsafa iliyoaminiwa na kufuatwa kwa bidii.Ili kuhakikisha kuwa falsafa hii inaleta matunda yanayotakiwa,chama tawala kwa kuongozwa na mwenyekiti wake Mwalimu Julius Nyerere walifanya ziara nchi nzima kuhimiza shughuli za kilimo cha kisasa na chenye tija kwa kila mkulima.

Ilisisitizwa viongozi kuwa mfano,kila kiongozi alitakiwa kuwa na shamba la mfano,alime kisasa na atumie mbolea na mbegu za kisasa.Msisitizo ulikuwa kama wewe ni mwanasiasa mzuri basi uthibitisho wake ni kuwa mkulima mzuri.Mwalimu alisafiri nchi nzima kusisitiza kilimo naye akishiriki katika kulima kwenye mashamba ya ushirika,alipiga kambi katika baadhi ya sehemu hadi wiki mbili.

Hamasa ya Kilimo iliongezeka hadi katika maonyesho ya Mbeya ya mwaka 1978 iliyokuwa bendi maarufu ya Orchestra Marquis du Zaire ilitunga wimbo maarufu sana uliokuwa na maneno ” “…Safari yetu Mbeya, tulifurahi sana. Wakazi wote wa Mbeya, walitushangilia. Sikukuu ya wakulima Saba Saba!”.Hii ni kusema pia kila mwananchi aliona umuhimu wa kilimo na alijisikia kama ni sehemu ya kushiriki ama kuhamasisha kilimo.Nadhani aina ya nyimbo tunazozikia zikiimbwa na wanamuziki wetu leo zinaweza kutupa picha halisi ya falsafa yetu kama taifa,nyimbo huwa zinaakisi mambo tunayoyathamini kama nchi.

Katika maonyesho ya sabasaba pamoja na kukumbuka kuzaliwa kwa TANU msisitizo uliongezeka na kuwa ni kushiriki maonyesho ya bidhaa za kilimo zilizoletwa na wakulima wa maeneo mbalimbali.Vyuo vya kilimo kama vile SUA(Sokoine University of Agriculture) villitumia fursa hiyo kuonyesha ugunduzi mpya wa mbegu za kisasa,dawa za kuua wadudu ama mbinu mpya za kuongeza mazao ya killimo.Hii ndio ilikuwa sabasaba,na mantiki hapa ilkuwa ni kutuma ujumbe kuwa chama kilichotuletea uhuru kilikuwa kinathamini sana kilimo kama njia ya kuleta mendeleo katika nchi yetu.Kutokana na kukubalika kwa falsafa hii,serikali iliamua kuwa katika kila mkoa kuwe na uwanja maalumu wa kufanya maonyesho haya ya kilimo,na ndivyo ilivyokuwa,hapa ndipo Dar Es Salaam ilipotenga viwanja malumu Kilwa road ambavyo vinajulikana kama viwanja vya maonyesho vya sabasaba.

Hata hivyo,ilipofika miaka ya tisini falsafa ya nchi yetu ilibadilika kimyakimya,hasa baada ya azimio la Zanzibar lililofuta azimio la Arusha kinyemela.Msisitizo ulihama kutoka kwenye kilimo na kuingia kwenye biashara zaidi,hasa biashara huria.Kutokana na nguvu ya falsafa hii ghafla maonyesho ya sabasaba yakaanza kujaa bidhaa za biashara na sio mazao ya kilimo.Ulimwengu wa kibiashara ni ulimwengu unaoongozwa na kutengeza faida,wenye nguvu ndio hupata nafasi.Wakulima waliozoea kupata nafasi za bure kuweka bidhaa zao za maonyesho sasa walitakiwa kulipia ada ili kuweka bidhaa zao(siasa ni biashara),wananchi waliokuwa wamezoea kwenda katika viwanja hivi kujifunza na kununua bidhaa za kilimo,sasa walikutana na utaratibu mpya wa kulipishwa kiingilio.

Ukweli ni kuwa huwezi kulinganisha nguvu ya wakulima wetu na wafanyabiashara,baada ya miaka michache,wafanyabishara walikuwa wengi kuliko wakulima katika viwanja vya maonyesho.Dhima ikabadilika kimyakimya kutoka kuwa maonyesho ya ugunduzi wa mbinu mpya na za kisasa za kilimo hadi soko kubwa la uchuuzi.Ndio,ni soko la uchuuzi kwa sababu bidhaa nyingi zinazoonyeshwa sabasaba hazizalishwi hapa nchini.Sabasaba imegeuka kuwa ni siku za kutoa offer(punguzo la bei) kwa wananchi.

Kutokana na unyonge wa wakulima wetu ilibidi wapozwe kwa kuchaguliwa siku nyingine ambayo ni tarehe 8 mwezi wa 8. Hata kama nia si kuendeleza dhana ya siasa ni kilimo,angalau kuwafanya wakulima wetu wasinu’gunike.Lakini swali la kujiuliza,Kufanya maonyesho ya biashara badala ya kilimo siku ilyozaliwa TANU ina tafsiri yoyote kifalsafa?

Mimi nadhai inabeba tafsiri kubwa ambayo haipaswi kupuuzwa.Mwanzoni TANU kilijulikana kama chama cha WAKULIMA na wafanyakazi,hii ndio maana hata alama zake katika nembo ilchagua jembe na nyundo,na hili ndilo lilipelekea kuwa na azimio la iringa la SIASA ni KILIMO.Kubadilika kwa siku hii na maudhui yake ni kusema kuwa falsafa ya chama na serikali imeshabadilika na hakuna mjadala,,sasa imekuwa SIASA NI BIASHARA.Nadhani hata nembo za chama sasa zinatakiwa zibadilishwe.

Hivi kuna mkulima ana sauti leo ndani ya Chama au ndani ya serikali?Unamfahamu mkulima yoyote ambaye ana nafasi kubwa ya kisiasa?kama wapo wanahesabika.Lakini je unawafahamu wafanyabiashara wakubwa wenye nafasi za kisiasa?Bila shaka ndio.Ingawa mtu hakosi sifa ya kuwa kiongozi kwa sababu ni mfanyabiashara ila tumeshuhudia jinsi wanasiasa wengi wakitumia nafasi zao kibiashara na kuleta mgongano wa kimaslahi.Hii si kwa sababu haiwezekani ukawa mfanya biashara na kuwa kiongozi mzuri,bali ni kwa sababu ya udhaifu wa mifumo yetu ya kitaasisi na sheria imefanya siasa kuwa ni mwanya mzuri wa kujitajirisha kibiashara.

Ingawa ni kweli kuwa bodi ya biashara ya nje(BET) inafanya kazi nzuri ya kuwaunganisha wafanyabisahara na masoko kupitia monyesho ya sababsaba lakini dhima ya kuadhimisha tarehe 7 mwezi wa 7 kuwa ni siku ya kuzaliwa TANU,Kuhimiza kilimo na kukumbuka mapigano yetu na wakoloni ni muhimu.Hii ilikuwa ni siku ya kukumbusha kizazi cha leo kuunganisha nguvu kama walivyofanya TAA na AA ili kupambana na “mkoloni wao” ambaye ni umaskini,kuweka tofauti zao za kidini na kikabila na kukusnya nguvu pamoja.Kama vile ambavyo huwezi kuamua kusherehekea siku yako ya kuzaliwa(birthday) tarehe tofauti na ile uliyozaliwa,pia hatuwezi kusherehekea kuzaliwa kwa TANU na kujikumbusha alama za TANU za kilimo na Kazi siku tofauti. Siku hizi tukisherehekea sabasaba mambo haya muhimu ya kihistoria hayatajwi kabisa.Hii si sawa!

NAWATAKIA SHEREHE NJEMA YA SABASABA!

Leave a comment

name*

email* (not published)

website