Navigate / search

Sababu za Kushuka kwa thamani ya Shilingi Yetu na Hatua za kuipandisha

win_20150203_182446

Kwa hivi karibuni kumekuwa na majadala mkali kuhusu sababu zilizopelekea kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa,wachumi na watanzania wa kawaida wamejitokeza kueleza maoni yao na hisia zao kuhusiana na jambo hili..Katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na Taarifa rasmi na za kitaalamu kuhusu jambo hili,Benki kuu ya Tanzania imetoa maelezo maalumu juu ya sabbau za kushuka kwa thamani ya shilingi na kuainisha hatua ilizochukua na nini kinatakiwa kifanyike ili kunusuru hali hii.

 

MAELEZO YA BENKI KUU KUHUSU KUHUSU KUHSUKA KWA THAMANI YA SHILINGI YA TANZANIA KWA KAMATI YA FEDHA,UCHUMI NA BIASHARA.

1. Utangulizi

1.1 Thamani ya Shilingi kwa Kipindi cha Mwaka 2010 mpaka 2014

Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani katika soko la jumla la fedha za kigeni (Interbank foreign exchange market-IFEM) ilishuka kutoka shilingi 1,318 kwa dola moja mwezi Januari 2010 na kufikia kiwango cha shilingi 1,543 kwa dola moja ya Marekani mwezi Juni 2011. Katika kipindi hicho thamani ya shilingi katika soko la rejareja ilishuka kutoka shilingi 1,333 kwa dola moja ya Marekani na kufikia shilingi 1,547 kwa dola. Kushuka kwa thamani ya shilingi kulichangiwa na mfumuko mkubwa wa bei pamoja na mauzo hafifu nje ya nchi hasa kufuatia mdororo wa uchumi duniani.

Thamani ya shilingi ilishuka kwa kasi zaidi kati ya mwezi Juni 2011 hadi Oktoba 2011 kufuatia baadhi ya washiriki wa soko la fedha za kigeni kucheza kamari/kufanya biashara ya dola kwa lengo ya kujinufaisha (speculation). Kufuatia hali hii, hatua mbalimbali zilichukuliwa na Benki Kuu ikiwa ni pamoja na kuongeza viwango vya akiba ambavyo mabenki yanatakiwa kuhifadhi Benki Kuu (SMR) kutoka asilimia 20 mpaka asilimia 40 kwa amana za serikali; kupunguza kiwango cha fedha za kigeni ambazo mabenki yanaruhusiwa kubaki nazo—ambazo zinaweza kutumika kutafuta faida kwa miamala ya fedha za kigeni (net open position, NOP)—kutoka asilimia 20 hadi asilimia 10 na hatimaye asilimia 7.5. Benki kuu pia iliongeza kiwango cha mauzo ya fedha za kigeni kwenye soko la jumla. Kufuatia juhudi hizo, thamani ya shilingi iliimarika tena na kubaki tulivu kwa takribani miaka mitatu hadi kufikia robo ya mwisho ya mwaka 2014 (Jedwali Na. 1 na Chati Na. 1a & 1b).

Chati Na 1a: Wastani wa Mwenendo wa Thamani ya Shilingi dhidi ya dola ya Marekani

chati 1

Chati Na 1b: Wastani wa bei ya dola kwa shilingi – soko la jumla

chati 1b

Kama inavyoonekana katika Chati Na. 2 hapo chini, thamani ya shilingi ilipungua kwa wastani wa asilimia 8.6 kwa mwaka kati ya Januari 2010 hadi Mei 2011. Baada ya hapo kasi ya kushuka thamani ilipanda hadi wastani wa asilimia 11.7 kwa mwaka kati ya Juni 2011 hadi Novemba 2011. Kutokea Desemba 2011 hadi Septemba 2014 thamani ya shilingi ilitulia ambapo ilipungua kwa wastani wa asilimia 1.8 kwa mwaka.

Chati Na. 2: Mwenendo wa Thamani ya Shilingi dhidi ya dola ya Marekani

Chati 2

2. Thamani ya shilingi kwa kipindi cha Machi 2014 hadi Machi 2015

Katika kipindi cha Machi 2014 hadi Machi 2015, thamani ya shilingi ilishuka kwa asilimia 9.6 katika soko la jumla na asilimia 13.0 katika soko la rejareja (Jedwali Na. 1). Kushuka huku kulitokana zaidi na kuimarika kwa uchumi wa Marekani. Kuimarika kwa uchumi wa Marekani kumefananya wawekezaji wengi duniani kuwekeza zaidi Marekani na hivyo kuongeza mahitaji ya dola ya Marekani. Kwa sababu hiyo sarafu za nchi nyingi duniani pia zimeshuka thamani dhidi ya dola ya Marekani kama inavyoonekana katika Jedwali Na. 2. Baadhi ya sarafu hizo kama vile Euro ya Ulaya, Pauni ya Uingereza, Yen ya Japan, Shilingi ya Uganda, na Rand ya Afrika Kusini, zimeshuka kwa kasi zaidi ya shilingi ya Tanzania.

Jedwali Na. 1: Mwenendo wa Thamani ya Shilingi dhidi ya dola ya Marekani
Machi 2014              Machi 2015                Badiliko
Soko la jumla (IFEM)                      1,629.6                     1,786.3               9.6%
Soko la rejareja (bureau-mean rate) 1,631.9            1,844.5                 13.0%

Jedwali Na 2: Mwenendo wa Thamani za Sarafu Mbalimbali dhidi ya Dola ya Marekani
Machi 2014               Machi 2015       Badiliko
Tanzanian Shilling               1,629.60                  1,786.30            9.62%
Great Britain Pound                    0.60                         0.68               12.65%
Euro                                               0.73                      0.93                   28.27%
Japanese Yen                              103.27                119.86             16.07%
Indian Rupee                                 59.97                   62.50               4.23%
Kenyan shilling                             86.55                     92.40            6.76%
Ugandan Shilling                           2,588.73               3,030.32       17.06%
South African Rand                      10.57                          12.18              15.26%

2.1 Sababu nyingine za kushuka kwa thamani ya shilingi kwa kipindi cha Machi 2014 hadi Machi 2015

2.1.1 Kupungua kwa kasi ya upatikanaji wa dola nchini ukilinganisha na mahitaji

Upatikanaji wa dola nchini umepungua kutokana na sababu mbalimbali kama zinavyoainishwa hapa chini:

Kupungua kwa mapato ya mauzo nje ya nchi

Mapato yanayotokana na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yamekuwa yakiongezeka kwa kiasi kidogo ukilingalisha na mahitaji ya fedha za kigeni kwa ajili ya kununua bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi. Kwa kipindi cha mwaka unaoishia Machi 2015, mauzo ya bidhaa na huduma nje yalifikia dola za Marekani milioni 9,355.5 ukilinganisha na uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ambao ulikuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 13,456.9.

Eneo mojawapo ambalo mapato yake yamepungua ni mauzo ya dhahabu kutokana na kushuka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia na kupungua kwa uzalishaji wa dhahabu nchini. Uzalishaji wa dhahabu ulipungua katika kipindi hicho kutokana na kufungwa kwa baadhi ya migodi kama Tulawaka na Resolute. Kwa mwaka unaoishia Machi 2015, mapato kutokana na dhahabu yalishuka hadi dola za Marekani milioni 1,377.2 kutoka milioni 1,588.9 zilizopatikana katika mwaka ulioishia Machi 2014. Hali hii imepunguza ahueni ambayo ingeweza kupatikana kutokana na ongezeko la mauzo ya bidhaa za viwandani pamoja na utalii.

Chati Na. 3: Mwenendo wa Mauzo ya Dhahabu Nje ya Nchi kwa Mwaka Unaoishia Machi (Dola Million)

Chati 2

Ucheleweshwaji wa fedha kutoka kwa wahisani na mikopo ya kibiashara toka nje ya nchi

Kuanzia robo ya pili ya mwaka 2014/15, wahisani hawakutoa fedha za kigeni kama ilivyokuwa imetarajiwa. Katika kipindi cha robo tatu za kwanza za mwaka 2014/15 fedha za wahisani zilizopokelewa zilikuwa dola za Marekani milioni 122 ikilinganishwa na makisio ya dola za Marekani milioni 473.7. Hali hii imechangia katika upungufu wa fedha za kigeni nchini na pia kuleta hisia ya kuwepo kwa uhaba katika soko la fedha za kigeni.

Katika mwaka 2014/15, serikali ilitarajia kupokea mikopo ya kibiashara kutoka nje yenye thamani ya dola za Marekani milioni 800, lakini hadi mwezi Machi 2015 mikopo yenye thamani ya dola milioni 310 tu ndiyo iliyokuwa imepatikana. Hali hii pia imechangia upungufu wa fedha za kigeni nchini.

Chati Na. 4: Mwenendo wa Upatikanaji wa Fedha za Kigeni kwa Bajeti

Chati 4

Msimu wa mapato madogo (low-season) yatokanayo na utalii na bidhaa za kilimo

Kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili ni msimu wa mapato madogo yatokanayo na bidhaa za kilimo na utalii hali ambayo inachangia upungufu wa dola kwenye soko. Ni matarajio kwamba hali hii itabadilika katika kipindi cha mwezi Mei hadi Septemba wakati wa msimu wa utalii na mavuno ya kilimo.

Kuongezeka kwa malipo ya serikali nje ya nchi (foreign government obligations)

Malipo ya serikali nje ya nchi yameongezeka katika mwaka wa fedha 2014/15 yakijumuisha yale ya mashirika ya umma kama TANESCO na TRL.

Chati Na. 5 Malipo ya serikali kwa dola

chati 5

3. Thamani ya shilingi kwa kipindi cha mwezi April 2015

Katika mwaka ulioshia Machi 2015, shilingi ilishuka thamani kwa asilimia 13.0. Hata hivyo kwa mwezi April 2015, kasi ya kushuka thamani iliongezeka ambapo shilingi ilishuka thamani kwa asilimia 8.0 ndani ya mwezi mmoja tu (Jedwali Na.3).

Jedwali Na. 3: Mwenendo wa thamani ya Shilingi dhidi ya sarafu mbalimbali (badiliko kwa asilimia)
Mar-14 to Mar 15 31st                           Mar-15 to 29th Apr-15
US dollar                                 13.0                                                              8.0
Great Britain Pound                1.5                                                                12.6
Euro                                           -11.7                                                           12.0
Japanese Yen                            -4.2                                                             9.1
Indian Rupee                              10.1                                                            6.7
Kenyan shilling                            6.2                                                             5.5
Ugandan Shilling                          -3.2                                                           7.8
South African Rand                         0.3                                                         11.2

Sababu za kushuka thamani kwa kasi:

“Shortage psychology”na speculation (hisia za upungufu)

Taharuki iliyoletwa na hisia za upungufu katika soko zimesababisha ongezeko la mahitaji ya dola hata kwa wale ambao hawana mahitaji ya kimsingi ya dola. Aidha wengine wanafanya biashara/kamari ya dola kwa malengo ya kujinufaisha na mabadiliko ya thamani (speculation).

Wasiwasi unaohusiana na uchaguzi (uncertainty)

Katika nchi nyingi ambazo zimekuwa na historia ya matukio hatarishi wakati wa uchaguzi; wawekezaji na wafanyabiashara wamekuwa na tabia ya kuhamisha kwa muda mali/fedha zao nje ya nchi wakisubiri matokeo ya uchaguzi. Katika nchi hizo kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kuhamisha familia zao kwenda kusubiri matokeo nje ya nchi. Hii imesababisha ongezeko la mahitaji ya fedha za kigeni ili kukamilisha uhamisho huo. Takwimu za illicit flows mara nyingi zinaonyesha kuongezeka kwa kasi ya uhamishaji huo katika kipindi cha uchaguzi. Ingawa kwa Tanzania, matukio mabaya yanayohusiana na uchaguzi ni nadra, takwimu za illicit flows zinaonyesha kuwepo kwa uhusiano na election cycles. Kuna uwezekano mkubwa kuwa sehemu ya taharuki inayohusisha uhamishaji wa fedha za kigeni imechangia kuongezeka kwa mahitaji.

4. Madhara ya kushuka kwa thamani ya shilingi
i. Kupanda kwa bei za kuagiza bidhaa nje (import bill) na hivyo kusababisha mfumuko wa bei (imported inflation).
ii. Kuongezeka kwa mzigo wa malipo ya mikopo ya nje kwa mikopo ya serikali na ya sekta binafsi.
iii. Wasiwasi wa uchumi kwenda mrama unaweza kupunguza uwekezaji.

Wapo Walionufaika:
i. Wanaouza bidhaa nje wanapata shilingi nyingi zaidi kwa kila dola. Kwa mfano kwenye biashara ya utalii, wauzaji mazao ya kilimo, bidhaa za viwanda, madini na kadhalika nje ya nchi.
ii. Wanaopokea fedha toka kwa jamaa zao nje (remittances).
iii. Kuongezeka kwa mapato ya serikali yatokanayo na kodi za bidhaa na huduma kutoka nje (ushuru wa forodha) pamoja na misaada na mikopo kutoka nje.

5. Matarajio na hatua zinazochukuliwa

Kwa kipindi kijacho mambo makubwa matatu yatasaidia kupunguza kasi ya kushuka kwa thamani ya shilingi:

i. Kuanza kwa msimu wa mapato ya utalii mwezi Mei 2015 ambapo inatarajiwa kuongeza mapato yanayotokana na shughuli za utalii nchini. Mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa za kilimo nje ya nchi nayo yanatarajiwa kuongezeka kuanzia mwezi Agosti 2015.

ii. Kutolewa kwa fedha za wahisani (World Bank na AfDB) na kupatikana kwa mikopo yenye masharti ya kibiashara (ENCB). Matarajio yetu ni kwamba fedha hizo kutoka nje zitaingia kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha 2014/15. Hali hii itaongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.

iii. Mategemeo ya kutengemaa kwa uchumi wa ukanda wa Euro na kuimarika kwa uchumi wa nchi za Ulaya. Hii itaongeza mahitaji ya bidhaa kutoka Tanzania.

Hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu
Benki Kuu ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali, hasa za utekelezaji wa sera za fedha ili kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania.
i. Benki Kuu imeongeza mauzo yake ya dola kwenye soko la jumla. Katika kipindi cha Januari hadi Aprili 2015, Benki Kuu imeuza dola milioni 339 katika IFEM, takriban sawa na kiasi kilichouzwa kipindi kama hicho mwaka 2014, ingawa malipo nje ya nchi yalizidi yale ya mwaka 2014 kwa zaidi ya dola za milioni 300.

ii. Kupunguza ujazi wa fedha katika uchumi ili kudhibiti kasi ya ukuaji wa miamala katika soko la fedha za kigeni. Hii ikiwa ni pamoja na kuongeza SMR ili kupunguza uwezo wa mabenki kutumia zaidi fedha walizonazo kufanya miamala katika IFEM ili kujinufaisha.

iii. Kudhibiti biashara za fedha za kigeni
a. Swaps: Benki Kuu imeongeza maturity
b. Net Open Position (NOP)- Kupunguza kiwango cha fedha za kigeni ambazo mabenki wanaruhusiwa kubaki nazo ambazo zinaweza kutumika kutafuta faida kwa miamala ya fedha za kigeni.

Matarajio ya mwelekeo wa thamani ya Shilingi

Kasi ya kushuka kwa thamani ya Shilingi inatarajiwa kupungua katika siku zijazo kutokana na hatua zinazoendelea kuchukuliwa kama ilivyotokea mwaka 2011.

Comments

Emmanuel
Reply

I am satisfied, though we have to knw that economics is crafty!! we need aggressive and patriot economists to defend our economy. We do not have to regard the results bt rather we have to be predetermined everyday in redeeming and protecting ours.

Leave a comment

name*

email* (not published)

website