Navigate / search

Sababu Inayokukatisha Tamaa Na Jinsi Ya Kuishinda !!!

Maneno ya Donovan Bailey ni muhimu sana hasa pale aliposema-“Fuata moyo wako unataka nini,jiandae kufanya kazi kwa bidii na kujitoa sana na zaidi ya yote usiruhusu MTU YOYOTE yule akuwekee MIPAKA ya kile ambacho unaweza kukifanya kwenye maisha yako (Follow your passion, be prepared to work hard and sacrifice, and, above all, don’t let anyone limit your dreams).

Siku moja nilipokea simu toka kwa mtu mmoja ambaye kwa hali ya kawaida alikuwa amenizidi kila kitu-Umri,elimu,utajiri na umaarufu.Mtu huyu alinitaka tuonane kwa faragha kwani alikuwa na jambo muhimu sana la kuniambia kwa maelezo ambayo alinipa.Kabla hata sijakutana naye,nilikuwa nina maswali mengi sana kichwani-“Anataka kuniambia nini?” lakini kila nilipojaribu kutafakari sikupata majibu.

Baada ya kukutana naye nikiwa na shauku kubwa sana kujua anataka kuniambia nini,mara baada ya kusalimia akatoa kitabu changu cha TIMIZA MALENGO YAKO na akafungua sura ya kwanza inayosema “Umekuja duniani kufanya nini?Lijue kusudi lako la kuzaliwa”.Kisha akaanza kuniambia-“Najua kwa nje unaniona nimefanikiwa sana lakini ukweli ni kuwa baada ya kusoma kitabu chako ndio nimegundua kusudi la kuumbwa kwangu na nakosa usingizi kwani naona umri wangu umeenda sana na sijui nitafanya nini nianze kuishi ndoto yangu.Nimeishi kwa mwonekano wa mafanikio ya nje ila ukweli ni kuwa kwa ndani sijafanikiwa kabisa,ninachofanya sicho ambacho haswaa natakiwa kufanya,naomba unisaide”.Ukweli ni kuwa baada ya kumsikilzia  nilivuta pumzi kwa uzito mkubwa na baada ya hapo niliendelea na kumshauri hatua za kuchukua.

Moja ya changamoto kubwa sana ambayo iko duniani kwa sasa ni watu kuishi maisha yasiyo ya kwa;kwa maneno mengine kuna watu wengi sana wanaishi ndoto za watu wengine.Kuna watu ambao kwa nje huwa wanaonekana kama wamefanikiwa sana ila wao pia wanatamani kupata msaada wa kutoka pale walipo.Kuna watu wengi sana ambao wanafanya kazi ambazo sio chaguo lao, ila lilikuwa ni chaguo la wazazi wao.Ndani yao wanajua kabisa kuwa wanachofanya sicho ambacho walitakiwa kukifanya.

Kuna watu ambao wanafanya kazi kwa sababu matokeo yao ya shule yaliwalazimisha kwenda kozi fulani lakini ukweli ni kuwa hiyo kazi hawaipendi kabisa.Kuna wengi ambao wamejikuta wamekwama katika mazingira na kazi ambazo ukweli sio kitu wanachotamani kuendelea kukifanya.Na hii ndio sababu mojawapo kubwa sana ya watu kukata tamaa katika kuelekea malengo yao.Moja ya kitu ambacho kinawasababisha watu wengi wakate tamaa kwa haraka katika kile ambacho wanakitafuta ni pale ambapo wanajikuta wanafanya kitu ambacho hawakutakiwa kufanya kabisa.Utajuaje kama unachofanya sio kitu sahihi kwako?

Dalili ya kwanza ni hofu ya kuwaangusha watu kama ukiacha.Hii inamaanisha kuna watu ambao kila wakati unawaza-“Hivi mama ambavyo alikuwa anatamani niwe daktari nisipokuwa atajisikiaje?”,”Hivi babu alishasema anataka niwe mwalimu,itakuwaje kama nisipojkuwa mwalimu?”-Kwa ufupi ni kuwa kwa kile uanchofanya akili yako yote inaelekezwa katika kuwapendezesha wengine na sio kufurahia kukifanya.Hebu jichunguze,kile uanchofanya kwa sasa unafanya kwa ajili yako ama kwa ajili ya kufurahisha na kutimiza ndoto za wengine.Kumbuka kuwa una maisha ya mara moja tu,usiyafanyie majaribio.Kama wewe ni mzazi ningekushauri uwe mshauri kwa mtoto wako ila usimlazimishe kuishi ndoto zako,kwani kila mtu amepangiwa njia tofauti ya kufanikiwa na ana vipawa na uwezo tofauti.

Dalili ya pili ni kuchukia unachofanya.Kuna watu wako kwenye kazi ambazo ukweli zimewasabishia vidonda vya tumbo,wamepata msongo wa mawazo,wamepoteza hali ya kujiamini na hawaoni kama wanaweza tena.Kazi yoyote ile ambayo inaua uwezo wako wa KUJIAMINI na KUJIKUBALI(self-esteem and courage) sio kazi nzuri kwako.Kama wewe wakati wote unakuwa na furaha ila ukiwaza kuhusu kwenda ofisini kwako unaanza kusikia huzuni,basi ujue hauko mahalil sahihi.Kazi yoyote unayoifanya haitakiwi iwe chanzo cha wewe kupoteza FURAHA YAKO na kupoteza kujiamini kwako.

Dr.Myles Munroe aliwahi kusema kuwa –“Umeumbwa orijino usikubali kufa ukiwa nakala ya mtu”(You were born original, don’t die a copy).Unatakiwa uwe na ujasiri wa kuamua kuanza kuishi maisha unayoyataka leo.Usikubali kuwa kama yule mzee ambaye nilikutana naye na akawa anatamani miaka irudishwe nyuma ili aanze upya.

Moja ya sababu kubwa inayowafanya watu kukata tamaa kila wakati ni pale wanapojilazimisha kukaa na kuendelea kufanya kitu ambacho sio cha kwao.Kumbuka kuwa kwenye kila unachofanya ni lazima utakutana na changamoto ambayo utahitaji nguvu kubwa kuweza kuitatua.Kama uko kwenye kitu ambacho haukipendi basi utajikuta hauna nguvu na changamoto yoyote ambayo inakuja mbele yako itakuangusha kirahisi sana.

Jikague leo na ujiambie-“Nitakuwa tayari kulipa gharama ya kufanya maamuzi yoyote ambayo yatanifanya niiishi kwa furaha maisha yangu yote yaliyobakia”

@JoelNanauka

See You At The Top

Leave a comment

name*

email* (not published)

website