Navigate / search

PHELPS:NIMEWEZAJE KUPATA MEDALI 23 ZA DHAHABU KATIKA MASHINDANO MBALIMBALI.

1-32972wazj4a0z3mrr289hm

Katika michezo ya olimpiki iliyofanyika Brazil mwaka huu,muogeleaji maarufu sana wa marekani alistaafu mchezo huo akiwa amefikisha medali 23 za dhahabu katika mashindano mbalimbali aliyowahi kushiriki.Kiwango hiki cha mafanikio ni kikubwa sana kwa mwanamichezo yoyote yule na inahitajika uwezo wa hali ya juu kuweza kukifikia.

Ingawa wako wanamichezo wengi sana ambao wana vipaji na bidii katika kufanya mazoezi mbalimbali ili kufikia kilele cha mafanikio yao,Michael Phelps amedhihirisha kuwa,ili kuweza kufikia kilele cha mafanikio unahitaji mambo mengine zaidi ya kipaji ulichonacho.Na hii inadhihirishwa wazi na ukweli kuwa kuna watu wengi sana duniani wenye vipaji vya hali ya juu lakini huwa wanashindwa kufikia mafanikio ya kiwango cha namna hii.

Hii ni sawa na pale unapowakumbuka watu waliokuwa na akili nyingi sana darasani lakini leo wanaishi maisha ya hali ya chini ukilinganisha na watu ambao walikuwa ni wa wastani kwa ufaulu.Hii ni sawa na kukuta mtu aliyeanza kazi hivi karibuni anapiga hatua kubwa na za haraka za maendeleo kuliko mtu mwenye miaka lukuki akiwa anafanya kazi.Leo nataka tuangalie mambo kadhaa ambayo huwa yanaleta tofauti kubwa katika hatua zetu za maendeleo kupitia maisha ya Michael Phelps.

Moja ni kujiandaa kukabiliana na kila hali ambayo tutakutana nayo tukiwa njiani kuelekea katika kutimiza malengo yetu.Phelps anasema kuwa akiwa anajiandaa na mashindano yoyote yale basi huwa anajitahidi sana kufanya mazoezi ya kutosha kukabiliana na kila hali ngumu ambayo inaweza kujitokeza katika mashindano halisi.Na kwa kufanya hivi imemsaidia sana.

Wakati wa mashindano ya olimpiki ya mwaka 2008 ya Beijing kwenye mashindano ya kuogelea ya mita 200 ya mtindo wa kipepeo wakati yanaanza,miwani ya Phelps ilivunjika.Lakini kwa sababu aliwahi kufanya mazoezi ya kuogelea bila miwani,hali hii aliweza kuikabili na kumaliza mashindano kwa kuvunja rekodi.
Katika kuelekea kutimiza malengo yako ni lazima ujiulize-Hivi ni jambo gani baya kabisa linaloweza kutokea katika nia yangu ya mafanikio?Je ni kupoteza mtaji wote?Au kukataliwa?au mazao kutozaa vya kutosha?Ukishajua hali hizi zinazoweza kutokea basi unajiandaa kisaikolojia kupambana nazo.Hii haimaanishi kuwa utakuwa ukizisubiri zitokee,Hapana,Inamaanisha kuwa utakuwa umejianda mara tu zitakapotokea utakuwa tayari uzikabili na hazitakukatisha tamaa hata kidogo.

Jambo la pili ni kuwa na malengo.Phelps anasema tangu akiwa na umri wa miaka 8 aliweka malengo ya kushinda mashindano ya Olimpiki.Wakati akihojiwa na mtangazaji wa chaneli ya Michezo ya Fox Sports,Bwana Joe Buck anlionyesha karatasi ya malengo yake ambayo aliiandika tangu akiwa mtoto mdogo.

Kwa maneno yake mwenyewe alisema-“Nimeandika malengo yangu mahali ambapo kila siku huwa nayaona ninapoamka na ninapoenda kulala,Hii inanifanya kuwa na hamasa na kila siku kuyatamani kuyatimiza”.

Watu wengi sana wanadharau nguvu iliyopo katika kupanga malengo ya maisha yao na hudhani kuwa kupanga malengo ni jambo la kujifurahisha.Kila unayemuona amefanikiwa leo katika maisha yake kuna siku aliweka malengo ya namna hiyo,hakuna kufanikiwa kwa bahati.Weka malengo yako na yawe mahali ambapo itakuwa ni rahisi kwako kuyaona na kuyasoma kila siku.
Sayansi ya mafanikio inashauriwa kuwa kila siku upate muda wa kuyaandika malengo yako.Kwa kufanya hivyo utakuwa unaufanya ubongo wako uyachapishe na uyatafakari namna ya kuyafanikisha kila wakati.Maisha bila malengo ni sawa na basi la mwendo kasi lilitoka nje ya barabara yake,litasababisha ajali.Kama hauna malengo jaribu kuanza kuyaandika leo,na kama unayo basi hebu jaribu kuyapitia na kuyasoma tena leo,kwa kufanya hivyo kuna hamasa kubwa sana utaipata.

Jambo la tatu ambalo phelps anaamini kuwa limekuwa na mchango mkubwa sana katika mafanikio yake ni kujifunza kila anapokosea.Kuna watu wakikosea basi huwa wanakata tamaa,kuna wengine wakikosea huwa wanajilaumu ama kulaumu watu wengine,lakini yeye hakuwa mtu wa namna hiyo,katika kila alipokosea aliangalia namna ya kufanya vyema katika mashindano yaliyofuata.

Katika mashindano ya olimpiki ya mwaka 2012 ya London,Phelps alikosa ushindi kwa nukta 0.5 ya sekunde na Chad le Clos wa Afrika kusini akashinda. Baada ya mashindano Phelps aliamua kuangalia video ya mashindano mara nyingi sana na akagundua wapi alikosea.Wakati anajiandaa na mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2016 alisema kuwa hatarudia tena makosa aliyofanya mwaka 2012 kwani alishajifunza.

Chochote ambacho uliwahi kufeli huko nyuma kwenye maisha yako hakitakiwi kiwe ni kizuizi cha kukufanya ushindwe kuendelea kufanikiwa katika ndoto yako.Kila mahali ambapo uliwahi kufeli hebu jiulize-Nilikosea wapi kisha ukishagundua jipange kutokukosea tena.Kwenye maisha wanaofanikiwa si wale ambao huwa hawaanguki ama hawafeli bali ni wale ambao kila wakijikuta wamefeli huwa wanajifunza makosa yao kwa haraka na wanainuka na kuendelea na safari yao.

Jambo la nne ni kuwa na bidii isiyo ya kawaida katika kile unachokifanya.Ingawa mafanikio ni jambo linalowezekana ila sio jambo ambalo ni rahisi sana kulipata.Bila bidii ya mazoezi Phepls asingefanikiwa kwa kiwango hicho.Ingawa kwenye mashindano anaongelea kwa dakika chache sana,muda anaoutumia kufanya mazoezi ni mkubwa sana.Akikumbukia mashindano ya olimpiki ya mwaka 2004 anasema alifanya mazoezi kwa siku zote 365 za mwaka ikiwemo na siku ya sikuuu ya Christmass pamoja na siku yake ya kuzaliwa.Kocha wake Bob Bowman alithibitisha hilo pia.
Ili ufanikiwe ni lazima uwe na juhudi isiyokuwa ya kawaida katika kufanya kile ulichokusudia.Bila kujali unafanya kazi gani kwa sasa,jitahidi kuwa mtu mwenye juhudi isiyo ya kawaida ili upate matokeo yasiyo ya kawaida.

Hata wewe unao uwezo wa kufanikiwa kwa kiwango kisicho cha kawaida kama utaamua kuzingatia kanuni ambazo phelps amezitumia.Watu wengi wana uwezo wa kufikia mafanikio ya hali ya juu ila hadi wanakufa huwa wanashindwa kufikia-Leo amua kwa kujiambia-“Mimi sitakuwa mmoja wao,Nitafikia Kilele cha mafanikio Yangu”

Endelea kutembelea www.JoelNanauka.com/www.mentorship.co.tz ili kujifunza zaidi.

Kumbuka kuwa ndoto yako inawezekana.

See You At The Top.

©JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website