Navigate / search

Njia 3 za Kuishinda Tabia Ya Kughairisha Mambo

88

Zimebaki wiki mbili kabla siku ya mwisho haijafika,hakuna shida bado nina muda wa kutosha sana.Zimebakia siku tatu kabla ya siku ya mwisho,hakuna shida ngoja nimalizie kusoma kitabu cha hadithi na kuangalia filamu inayosisimua mpya iliyotoka hivi karibuni kisha nitamalizia jukumu kabla ya siku ya mwisho haijafika.Imebakia siku moja,kwa kweli muda hautoshi na hivi kwa nini wasisogeze mbele siku ya mwisho.Leo sitaki usumbufu,nitazima simu na nitafanya hii kazi usiku kucha hadi asubuhi niikamilishe.Je,umeshawahi kupitia katika hali kama hii maishani mwako?

Tabia ya kughairisha mambo katika maisha yetu inawakabili wengi sana na bila kujua imekuwa ni chanzo cha watu wengi sana kushindwa kufikia malengo ya maisha yao.Mtaalamu wa mambo ya saikolojia,Profesa Clarry Lay anasema-Kughairisha mambo ni matokeo yanayoletwa na tofauti kati ya ulichokusudia kufanya na kile ambacho unajikuta unafanya.Hii ni rahisi sana kuelewa kwa kuangalia leo umekusudia kufanya nini na kisha mwisho wa siku kuangalia utakuwa umekamilisha mangapi katika yale uliyokusudia kufanya.

Swali la msingi ni kuwa kwa nini watu wanaghairisha mambo ambayo kwa uhakika wanajua ni mambo muhimu sana katika maisha yao?

Kughairisha mambo ni matokeo ya mashindano ya sehemu mbili za ubongo wako.Sehemu ya kwanza inajulikana kitaalamu kama “Limbic System” ambayo hii hufanya kazi bila wewe mwenyewe kuiamrisha na huusisha hisia za mambo yanayokupa hisia mbalimbali.Sehemu ya pili inahitwa “prefrontal Cortex” ambayo unaweza kuiamuru na kuitumia kupanga mambo ambayo umekusudia kuyafanya.Limbic System ni sehemu ya ubongo ambayo inachukua sehemu kubwa ya ufanyaji kazi wa ubongo na huwa imeshatengenezwa na kukokamaa wakati unapokuwa umezaliwa.Hisia kama vile hasira,furaha,raha huendeshwa na sehemu hii ya ubongo.Hii ndio sehemu itakayokuamrisha uinue mguu wako bila kupata muda wa kufikiria sana mara tu unapokanyaga miiba.Kwa upande mwingine Prefrontal Cortex ni sehemu dhaifu na hii hupokea taarifa na kuzifanyia maamuzi kisha kukusaidia kuchukua hatua,na hii ndio hutofautisha kati ya wanadamu na wanyama.Hii haifanyi kazi yenyewe,inahitaji kutumia juhudi kuifanyisha kazi.Mara tu unapoacha kuweka nguvu kufanya jambo fulani,limbic system huchukua nafasi yake na kukupelekea kufanya kitu kisicho na uzito lakini kinakupa furaha.

Hivyo basi kughairisha mambo ni matokeo ya kisayansi yanayotokana na kuendelea kuiachia sehemu ya ubongo wako inayopenda raha kuwa na nguvu kuliko sehemu ya ubongo wako inayoweza kukusaidia kufanya yaliyo ya muhimu katika maisha yako ya kila siku.

Ili kujua kama wewe ni mmoja wa watu walioathirika na jambo hili ,unaweza kujichunguza kwa kujiuliza maswali yafuatayo.Hivi kila wakati huwa napanga mambo ya kuyafanya kila siku ambayo ni ya muhimu lakini huwa nayaacha bila sababu za msingi?Je,mimi huwa ni mtu ambaye kila wakati niko tayari kukubali majukumu/wajibu ninaopewa na wengine hata kama si wa muhimu na ninajikuta kila wakati nayaacha yaliyo ya muhimu?Je,mimi ni mtu ambaye kila wakati huwa nasubiria kuwa na hisia fulani nzuri ama kujisikia vizuri ili niweze kufanya kitu hata kama ni cha muhimu na nisipojisikia kufanya huwa naacha?Je,Mimi ni mtu ambaye nikikasirishwa kidogo tu huwa ninaamua kuacha kabisa kufanya jambo fulani hata kama ni la umuhimu?Kama jibu lako ni ndio kwa maswali haya basi inamaanisha kuwa na wewe umeshaingia katika tatizo la kuwa mtu wa kughairisha mambo na jambo hilo limechangia kwa sehemu kubwa sana kukufanya usifanikiwe ama kukucheleweshea mafanikio yako.

Je,ufanye nini ili usiendelee kuwa mtu wa kughairisha mambo?.

Jambo la kwanza unalotakiwa kujua ni kuwa kughairisha mambo ni tabia inayojengwa kwa muda mrefu katika maisha ya mtu,hivyo ili uishinde ni lazima uibaini,uikubali na uiwekee mikakati ya kuishinda.Hebu jaribu kufikiria katika maisha yako,kuna maeneo gani ambayo umekuwa ukighairisha mambo kila wakati?Tumia muda kuyaorodhesha sasa hivi.

Hatua ya pili baada ya kuyagundua mambo ambayo umekuwa ukiyaghairisha kila wakati,hebu jaribu kujiuliza ni kwa nini umekuwa ukifanya hivyo.Mara nyingi utagundua kuwa hauna sababu za kufanya hivyo ama kuna visingizio ambavyo unaendelea kuvitumia kwa muda mrefu sana na ambavyo haujawahi kudhamiria kuvishinda.Kila lengo ulilonalo kuna hatua ya kwanza ambayo haiitaji pesa kabisa.Katika kila ambalo umekuwa ukilighairisha kila wakati hebu jiulize,kuna hatua gani naweza kuianza leo?Njia rahisi ya kushinda hali ya kughairisha mambo ni kuanza kufanya kile ambacho umeghairisha.

Hatua ya tatu ni kumwambia mtu kusudio lako la kufanya jambo ambalo umekuwa ukilighairisha kila wakati.Nashauri utafute mtu ambaye unamuheshimu na ambaye anaweza kukuuliza maswali na kiukweli hupendi kumuangusha wakati wowote.Hii ni njia ninayojulikana kitaalamu “Self-Policing System”;Ni njia ya kujiwekea wajibu wa kufanya wewe mwenyewe.Mueleze unataka kufanya nini na lini na umwambie kuwa ningefurahi kama ukiwa sehemu ya malengo yangu na nitakuwa nakushirikisha kila wakati.Hii itakusaidia kwani kila wakati ambapo utaona kama unataka kughairisha ukikumbuka kuwa kuna mtu unawajibika kwake,itakupa nidhamu ya kujirudi na kufanya.

Ninaamini leo ndio itakuwa mwisho wako wa kughairisha mambo katika maisha yako na utaanza kufanya yaliyo ya muhimu kwenye maisha yako.Ili ufanikiwe,leo anza na mambo ya muhimu zaidi na usighairishe kabisa,ukiweza leo-Utashangaa jinsi ambavyo utaanza kuweza kila siku.

Kumbuka kuwa Ndoto Yako Inawezekana.

Endelea kutembelea www.JoelNanauka.Com na www.Mentorship.co.tz ili Kujifunza zaidi.

See You At The Top.

©JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website