Navigate / search

Mkataba wa Bandari(TPA) na Impala:Yajue mambo 4 yanayotia Shaka

maxresdefault

Hivi Karibuni serikali imesimamisha mkataba wa mabilioni ambao mamlaka ya bandari Tanzania ulikuwa umeshafanya makubaliano ya awali na mwekezaji kampuni ya Impala Terminals Tanzania Ltd kampuni tanzu kutoka Uswisi.Hii imekuja siku chache baada ya WazirI wa uchukuzi,Mheshimiwa Samuel Sitta kumsimamisha aliyekuwa mkurugenzi wa bandari Bwn.Madeni Kipande kwa tuhuma za matumizi mabaya ya nafasi yake.Sababu kubwa ya kufuta makubaliano haya ya awali(Memorandum of Understanding) ni kufanya tathmini upya kuona kama mkataba huu ungekuwa na manufaa kwa Taifa.

Hata hivyo rekodi zinaonyesha kuwa taarifa muhimu za kampuni ya Impala zinazohusu anwani yao,umiilki wa hisa,marejesho ya kodi hayapo katika rekodi za RITA.Masuala ya uhalali wa usajili kampuni yaliwahi kuibuka katika kashfa ya ESCROW kuhusiana na kampuni ya PAP ya Harbinder Singh Seth aliyesema kuwa alinunua 70% ya hisa za IPTL
UKweli ni kuwa mkataba huu una kila dalili ya rushwa na ukiukwaji wa sheria nyuma yake kwa kuzingatia mambo yafuatayo:Kwanza ni vyema kuelewa kuwa mkataba huu ulikuwa umependekeza kuwa na umiliki wa ubia kati ya Kampuni ya Impala Terminals Tanzania Ltd na TPA(Mamlaka ya Bandari Tanznaia).Katika hatua ya kwanza kampuni ya kampala ilitarajiwa kuwekeza kiasi cha shilingi bilioni 334 kwa ajili ya kuendeleza kujenga na kuwekeza fedha kwenye ujenzi wa terminal ya gerezani.Mkataba huu umeleta utata mkubwa katika maeneo yafuatayo;

Moja ni utaratibu wa namna kampuni ya Impala ilivyopatikana.Katika tenda kubwa namna hii ni matakwa ya sheria ya ugavi na manunuzi ya umma(Public Procurement Act) kuwa ni lazima kuwe na matangazo yaliyo rasmi kwa ambao wangependa kuwa sehemu ya mradi na sio kuchagua mtu(single sourcing) bila kuwa na sababu za kujiridhisha na zIlizokubaliwa na vyombo vyote husika vya serikali.Katika mkataba huu,inaonekana jambo hili halikuzingatiwa na kutia shaka kuwa utaratibu wa kisheria tuliojiwekea tumeukiuka,na swali ni je?kwa nini utaratibu huu uliamua kukiukwa?Kukiukwa kwa utaratibu wa manunuzi ya umma ndio ilikuwa chanzo cha msingi cha kashfa ya RICHMOND iliyopelekea kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa.

Pili makubaliano ya Mkataba huu yalikuwa yanataka nguvu ya umiliki iwe kwa Impala kwa 51% na kubakiza 49% kwa mamlaka ya bandari.Hii ina maana kuwa nguvu ya kufanya maamuzi juu ya mustakabali wa mambo yahusuyo bandari ya Dar yangekuwa kwa kampuni binafsi kwa kiwango kikubwa.Kwa kuzingatia mchango mkubwa wa bandari na makusudi ya hivi karibuni ya kuindeleza na kuongeza ufanisi wake,jambo hili linahatarisha ustawi wa Taifa kiuchumi.Unapopoteza nguvu ya maamuzi katika kitega uchumi kikubwa kama hiki bila sababu zenye nguvu ni sawa na kupoteza fursa ya kutekeleza mipango yako uliyojiwekea kama Taifa.Kwa kuzingatia ukuaji wa bandari ya Dar Es Salaam wa asilimia 2.8 ni kusema kuwa faida ya ukuaji huu kwa kiwango kikubwa itawaendea wawekezaji zaidi,Hii ni rahisi kuelewa kwani mkataba huu ulitaka pia kama TPA itashindwa kununua gharama ya hisa za ziada basi Kampuni ya Impala itaendelea kuongezewa hisa zake za umiliki.

Tatu ni kuwa sheria ya nchi yetu inataka kila kampuni inayofanya kazi nchini Tanzania bila kujali kama ni tawi,ya kimataifa ama ni kampuni tanzu taarifa zake ziweze kupatikana kwenye shirika la usajli,ufilisi na udhamini(Sehemu ya Pili na Article 4) na ziweze kupatikana katika utaratibu uliowekwa kwa wale ambao watakuwa wanazihitaji.Hata hivyo taarifa zinaonyesha kuwa taarifa muhimu za kampuni hii zinazohusu anwani yao,umiliki wa hisa na marejesho ya kodi hayapo katika taarifa za RITA.Swali ni kwamba;kampuni hii haijasajliwa rasmi ama ni kampuni hewa ama kunani?RITA iliingia kwenye kashfa ya ESCROW baada ya mkurugenzi wake Mr.Phlippe Saliboko kutuhumiwa kupokea pesa shilingi milioni 40.2 kinyume na maadili na kufunguliwa mashtaka katika mahakama ya Kisutu.Masuala ya usajili ndiyo yalileta utata katika umiliki wa kampuni ya PAP iliyohusika katika kashfa ya ESCROW.

Nne,ingawa mkataba wa makubaliano ya ubia yalifanywa september mwaka 2014,katibu mkuu wa wizara ya uchukuzi wanaosimamia bandari hiyo na uongozi wake,Shaaban Mwinjaka alitamka hadharani kuwa hafahamu kuhusu uwepo wa mkataba huu.Kama mtendaji mkuu wa serikali hafahamu mkataba huu,nani mwingine anatakiwa kuufahamu?Ulikuwa ni mkata uliofichwa?nani aliuidhinisha?.

Kwa namna yoyote ile mkataba huu,una chembe nyingi za shaka na ni akisi ya mikataba mingi inayofanywa kinyume na utaratibu na kuvutia mazingira ya Rushwa.Kwa vyovyote vile hatua ya kubatilisha mkataba huu na kuchunguza uhalali na manufaa kwa nchi ni ya muhimu.Ule wito wa kurejea mikataba 26 ya madini ulioyolewa mwaka 2012 na kamati ya PAC nadhani unatakiwa utolewe pia katika kureje mikataba mikubwa ya mashirika ya umma.

Njia nzuri ya kuhakikisha mikataba haiwi sababu ya kuingiza hasara katika Taifa ni kuendelea kuhimiza uwazi katika michakato tokea inapoanza hadi pale inapoanza kufanya kazi.

Naipenda Tanzania,

Joel Arthur Nanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website