Navigate / search

Miaka 20 maadhimisho ya mauaji ya Kimbari Rwanda; Afrika bado haijajifunza?

Wanasiasa, vyombo vya habari na matumizi ya dini na ukabila yanaendeleza migogoro Afrika – Nimekumbuka ile kauli ya Rais ajaye Tanzania Hatatoka Kaskazini.

Mwezi huu yalianza maadhimisho ya kukumbuka mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda miaka 20 iliyopita(1994) ambayo yalishuhudia watu kati ya 800,000-1,000,000 wakipoteza maisha ndani ya siku mia moja kati ya April 7 na julai 15,1994.Ni mauaji ambayo hayakuwahi kutokea mahali popote katika kiwango kikubwa cha namna hii.Mauaji haya ya kutisha yaliwalenga zaidi watusi na wahutu ambao walikuwa na msimamo wa huruma kwa wahutu(moderate hutus).

Mauaji haya ingawa yalitokea ndani ya muda mfupi ukweli ni kwamba vuguvugu la kutokea kwa mauaji haya ilianza siku nyingi sana kulingana na historia ya nchi ya Rwanda.Tangu kutokea kwa mauaji haya wengi wamenyooshewa vidole kuwa ni chanzo au sababu ya mauaji haya kutokea.Wapo wanaolaumu UN kwa kuchelewa kuchukua hatua chini ya katibu mkuu wake aliyekuwa mwafrika Boutrous Boutrous-Ghali,Wengine wanalaumu mfumo wa kibelgiji wakati wa ukoloni uliowapa nguvu watusti na kuwapa madaraka zaidi kuliko wahutu walio wengi,wapo wanaolaumu waliokuwa waasi wa RPF wakati huo wakiongozwa na Rais wa sasa wa Rwanda Paul Kagame,wengine wanawanyooshea kidole waandishi wa habari kwa kuongeza chuki kupitia maandishi na sauti zao na wengine wanalilaumu jeshi;ili mradi kujaribu kutafuta hasa chanzo chake kilikuwa ni nini.Katika wingu la malaumu haya bado Afrika ina mengi ya kujifunza na kuyafanyia kazi ili kuepusha yasitokee mahali pengine tena.

Mwaka 1993 jumuiya ya kimataifa ilisimamia kusainiwa kwa mkataba wa amani kati ya serikali ya Rwanda iliyokuwa inaongozwa na Juvanal Habyarimana(mhutu) na waasi wakitutsi RPF waliokuwa wanaendesha mapigano yao kutokea Uganda.Serikali ya Habyarimana ilikuwa inaonekana kwa muda mrefu kuwakilisha wahutu waliofanya mapinduzi ya mwaka 1959(hutu revolution) yaliyowafanya watutsi wengi kukimbia nchi yao.Katika mapinduzi hayo watutsi wengi walikimbilia kaskazini mashariki mwa kongo ambao kwa sasa wanajulikana kama banyamulenge na wengine walikimbilia nchi ya Uganda.Wale waliokimbilia Uganda walikutana na vuguvugu la vita ya msituni iliyokuwa inaendeshwa na Yoweri Museveni na waasi wake wa NRA.Kati ya watustsi waliojiunga na kundi la msituni la Yoweri Museveni alikuwepo pia Rais wa sasa Paul Kagame.

Wakiwa ni theluthi moja ya jeshi zima la Rais Yoweri Museveni baada ya kuchukua madaraka Uganda,watusti wengi walipewa madaraka makubwa jeshi la Uganda akiwemo Fred Rwegyema aliyepewa wadhifa wa “Chief of Staff” wa jeshi la Uganda.Wakati Paul Kagame akiwa amepelekwa kupata mafunzo ya kijeshi marekani waasi wa RPF wapatao 3000 wakiongozwa na Fred Rwegyema walijaribu kuivamia Kigali ili kufanya mapinduzi,hata hivyo jaribio hilo lilishindwa baada ya siku tatu na wakiwa wameshaigia ndani ya Rwanda takribani kilometa 60 na Fred Rwigyema aliuawa.Baada ya tukio hili ndipo msaidizi wake Paul Kagame alichukua uongozi na kuanza kuimarisha RPF kwa kutumia msaada wa kifedha toka kwa watutsi mbalimbali waliokuwa wako uhamishoni katika nchi za ulaya.

Ndipo baadaye Paul Kagame aliendelea kufanya mashambulizi ya mara kwa mara yaliyosababisha jumuiya ya kimataifa kushinikiza kufanyika kwa makubaliano ya amani ya kusitisha mapigano yaliyojulikana kama “Arusha Accord”.Makubaliano haya yaliruhusu jeshi la RPF kuingizwa kama sehemu ya jeshi la Rwanda na wanajeshi wake takribnai 600 walikuwa Kigali,na walipewa sehemu ya jengo la bunge la Rwanda kulitumia ikiwa ni sehemu ya makubaliano yaiyofanyika Arusha.

Makubaliano haya yaliwaudhi sana kikundi cha wahutu wenye msimamo mkali waliokuwa wanajulikana kama “Akazu”,waliokuwa wana nafasi kubwa serikalini,wasomi na wenye fedha.Walimuona Habyaramana kama ni msaliti wa mapinduzi ya wahutu ya mwaka 1959.Kikundi cha Akazu kilikuwa na nguvu kubwa hasa kutokana na ukweli kuwa mke wa Rais Agathe Habyarimana alikuwa ni sehemu ya kikundi hiki.Hapo ndipo mkakati wa kuwashughulikiwa watutsi ulipoaanza kwa kushirikisha wanasiasa,wanajeshi na vyombo vya habari.

Chama tawala cha Rwanda kiligawanyika kati ya wale wanaokubaliana na hatua ya Rais kukubali kusaini mkataba na waasi na wale ambao walikuwa na msimamo mkali na kuona hatua hiyo ya Rais ni usaliti kwa wahutu na inahatarisha nafasi ya wahutu kisiasa,kiuchumi na kiusalama.Kutoka na hili ndipo chama cha Coalition for Defence of the Republic(CDR) kikiwa na lengo la kuwalinda wahutu na kuzuia kwa namna yoyote watutsi kuchukua nafasi yoyote katika serikali ya Rwanda.Kuona hivyo Rais Habyaramana alijaribu kuwaondoa kwenye madaraka wengi wa wale aliokuwa anaona wana msimamo mkali.Lakini hata hivyo baadhi yao kutokana na kuwa walikuwa kwenye nafasi nyeti alishindwa kuwaondoa akiwemo Theoniste Bagosora aliyekuwa “chief of staff” wa jeshi.

Baada ya kugundua mbinu ya Rais kuvunja nguvu yao ndipo wahutu wa msimamo mkali walianza kujipanga na kutoa mafuzo kwa vijana,kuwapatia silaha na kuwafundisha ukatili na mauaji kwa “maadui” zao wa kitutsi.Hapa ndipo chama tawala chini ya uongozi wa watutsi wenye msimao mkali walipounda kikundi cha Intarahamwe na CDR wakaunda impuzamugambi;vikundi vyote vikipewa mafunzo na silaha hasa mapanga.Ndani ya mwaka mmoja chini ya uongozi wa Theoneste Bagosora yaliagizwa mapanga takribani 500,000 na kuanza kugawiwa kwa vikundi hivi kidogokidogo.Walitumia kisingizio cha kujilinda(self-defence) kama vile sungusungu kwa jina maarufu la hapa Tanzania.

Baada ya kifo cha Rais wa Burundi,Melchior Ndadaye(Rais wa kwanza mhutu wa Burundi) aliyeuawa na watutsi wenye msimamo mkali ndipo wahutu wenye msimamo mkali wa Rwanda walipoeneza huki zaidi kwa kuonyesha kuwa watutsi hawawezi kuaminiwa.Hapa ndipo vikundi vya Intarahamwe na impuzamugambi walipoanza kupewa silaha nyingi zaidi.

Ndege ya Rais iliyokuwa imembeba Rais wa Rwanda Habyaramana,Rais wa Burundi Cyprian Ntryaramira na mawaziri kadhaa ilitunguliwa 6 April,1994 ikijiandaa kutua Kigali.Wahutu wenye msimamo mkali waliwalaumu watusti wa RPF na watutsi waliwalaumu wahutu wenye msimamo mkali kwa tukio hilo.Kanali Theoneste Bagosora mwenye msimamo mkali kinyume na watutsi aliunda kamati aliyoiongoza na akakataa kabisa kukabidhi madaraka kwa waziri mkuu Agathe Uwingiliyimana, kama katiba ilivyokuwa inataka.Wanajeshi wa Ubelgiji walienda kumchukua waziri mkuu ili kumpeleka Radio Rwanda kwenda kutoa tamko la serikali.Kuona hivyo kikundi cha ulinzi cha Rais(Special Presidential guards) walivamia radio.Baada ya muda mfupi nyumba ya waziri kuu ilivamiwa na aliuwawa yeye na mume wake na wanajeshi wa kibelgji walichukuliwa hadi kambi ya jeshi walikoteswa na kuuwawa.Watoto wa waziri mkuu waliokolewa kwa kusaidiwa na askari wa jeshi la la umoja wa mataifa(UNAMIR-United Nations Assistance Misions for Rwanda) kapteni Mbaye Diagne raia wa senegali,shujaa anayekumbukwa kwa kuwaokoa watutsi takribani 1000 kwa njia ya kuwahonga wine au sigara wahutu waliokuwa wameziba barabara ili wamruhusu apite.

Kiongozi wa misheni ya umoja wa mataifa nchini Rwanda raia wa Canada Romeo Dalalire alijaribu kadiri alivyoweza kuwasiliana na umoja wa mataifa na kuwaeleza haja ya kuongeza mamlaka(mandate) ya umoja wa mataifa katika kukabiliana na wahutu waliokuwa wanaua lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.Balozi wa marekani katika umoja wa mataifa wakati huo Madeline Albright alijaribu kushawishi baraza la usalama la umoja wa mataifa lichukue hatua bila mafanikio.Badala yake UN walibadili kazi ya askari wa umoja wa mataifa kutoka kulinda raia na kuwapa kazi ya kuwaondoa salama raia wa mataifa mengine na wafanyakazi wa umoja wa mataifa.Marekani ikiwa na kumbukumbu mbichi juu ya kipigo walichopokea Somalia katika misheni ya kumtafuta jabali wa vita Aideed walionyesha kutokuwa tayari kabisa ingawa baadaye Rais Clinton aliomba msamaha kwa kutofanya kilichohitajika kwa wakati.

Vyombo vya habari vilivyoanzishwa kwa minajili ya ukabila kama vile gazeti la kangura(ikimaanisha nguvu ya wahutu-hutu power) lilitumika kueneza propaganda ya mauaji ya watutsi.Mhariri wa gazeti hilo,Hassan Ngeze,aliyehukumiwa miaka 35 jela na mahakama ya mauaji ya kimbari Rwanda aliruhusu makala iliyojulikana kama-Amri kumi za kihutu(Hutu ten Commandments) zilizoongeza chuki kati ya wahutu na watutsi.Gazeti la Kangura lilitumia hadi vikatuni kueneza chuki kwa wananchi na kuchochea mauaji ya kimbari.

Radio Mille Collines iliyoanzishwa mwaka 1993 nayo ilikuwa sehemu kubwa ya mauaji ya Rwanda.Ikitumia lugha ya mtaani,ikipiga mziki mara nyingi na watu kupiga simu katika vipindi vyao ilionekana ni redio ya kuburudisha na ilipata wasikilizaji wengi hasa vijana.Taratibu ilianza kujiingiza katika kutoa matangazao yenye chuki na kutaja hadi majina ya watu na anwani zao/mahali wanapoishi ili wakashambuliwe.Wengi walipigia kelele jambo hili lakini mataifa ya magharibi wakiwemo marekani walisema wanaamini katika uhuru wa kuongea.Wanamuziki kama Simon Bikindi alitumia kipaji chake vibaya kwa kutunga nyimbo mbalimbali kuhamasisha chuki kwa watutsi.

Mauaji ya Rwanda yanatoa funzo kubwa kwa kila nchi.Uroho wa madaraka wa wanasiasa unawafanya kuanzisha vikundi vya vijana kama Intarahamwe ili kuwadhuru wapinzani wao.Mara ngapi tumesikia katika kampeni za kisiasa hapa Tanzania watu wakivamiwa kupigwa mapanga na hata kumwagiwa tindikali?Kama vikundi hivi havitadhibitiwa vitaendelea kupata nguvu na kutumia tiketi ya udini na ukabila kuhalalisha uovu wao.Vijana wasio na ajira maalumu ndio huwa chambo katika matukio kama haya.

Radio na magazeti yalikuwa nguzo muhimu kueneza chuki za ukabila Rwanda.Hakuna uhuru usiokuwa na mipaka,nilifurahi kusikia radio mbili za dini(moja ya kikristo na moja ya kiislamu) ikifungiwa kwa kueneza chuki.Hii ni hatua muhimu katika kudumisha amani,tukisema kama marekani walivyosema..”tunaheshimu uhuru wa kuongea”-tutajikuta kesho hatuna uhuru huo tena.

Viongozi wanaotafuta vyeo kwa kutumia karata ya ukabila au udini hawapaswi kuwaacha kuendelea katika siasa,lazima sheria inayokataza matumizi ya ukabila na udini katika siasa iwe yenye nguvu na inayosimamiwa.Afrika ya kati yamewakuta ya Rwanda;wao wanapigana kwa sababu ya tofauti ya dini zao.Sudani kusini yamewakuta wao wanapigana kwa sababu ya tofauti ya makabila yao,Neur na Dinka.Tunakumbuka mauaji ya Kenya 2007/2008 yalijikita katika ukabila na watu walipoteza maisha.Lakini katika mauaji haya yote ni uroho wa wanasiasa kushika madaraka kwa gharama yoyote ile.

Hapa Tanzania si mnakumbuka tamko la Bagamoyo,kwamba Rais ajaye hatatoka Kaskazini?Sikusikia chama husika kikikemea wala kukubali,ni ukimya tuu!!!Huo ndio mwanzo wa propaganda za hatari.

Yanayoendelea katika nchi zetu ni kusema kuwa bado Hatujajifunza???

Leave a comment

name*

email* (not published)

website