Navigate / search

Mbinu 3 za Mafanikio Toka Kwa Mwanzilishi wa KFC

kfc

Akiwa na umri wa miaka 5 alifiwa na baba yake na akajikuta alipofikisha miaka 16 basi ameshindwa kabisa kuendelea na shule.Kwa sababu hiyo aliamua kujiingiza katika shughuli mbalimbali za kuajiriwa na ndani ya mwaka mmoja hadi anafikisha miaka 17 alikuwa tayari ameshafukuzwa kwenye kazi nne.Baada ya hapo alijaribu kuomba kujiunga na shule ya sheria lakini alikataliwa na akaamua kuwa wakala wa masuala ya bima na hapo akafeli tena.
Alipofikisha miaka 19 alipata mtoto na mchumba wake lakini hata hivyo mchumba wake alikimbia na mtoto wao.Akiwa karika hali ya kutafuta maisha aliamua kuajiriwa kama muosha vyombo katika mgahawa mmoja hivi ambapo pia alianza kujifunza kupika vyakula mbalimbali. Alipofikisha miaka 65 baada ya kuishi maisha ya kutofanikiwa kwa muda mrefu aliamua kustaafu.

Siku ya kwanza alipostaafu alikabidhiwa hundi ya kiasi cha dola 105 kutoka serikalini.Baada ya kupokea hundi hii aliona kama vile maisha yameshafikia mwisho kabisa na hawezi kuendelea kuishi maisha yenye furaha tena.Kutokana na hali hii aliamua kujiua kwani aliona kama vile maisha hayana thamani tena kuendelea kuyaishi.Kabla hajafanya hivyo aliamua kukaa chini ya mti na kuanza kuandika hati yake ya urithi(will),lakini badala ya kuandika hati yake ya urithi akajikuta ghafla anaanza kuandika mambo ambayo angeweza kuyatimiza katika maisha yake lakini hakuweza kuyafanikisha.

Baada ya kujiuliza maswali mengi sana akagundua kuwa kati ya vitu ambavyo angeweza kuvifanya kwa mafanikio sana ni kuhusiana na masuala ya mapishi kwani anayapenda na amekuwa anafanya kwa muda mrefu.

Ili kutimiza ndoto mpya aliyoipata siku hiyo aliamua kuchukua hatua haraka sana na akakopa dola 87 na akanunua kuku na baadhi ya viungo na akaanza kupika kuku na kutembea nyumba kwa nyumba akienda kuwauza katika maeneo ya mji wa Kentucky.Kumbuka alikuwa tayari na umri wa miaka 65 kwa wakati huo,lakini miaka 3 baadaye akiwa na miaka 68 Colonel Harland David Sanders alijikuta tayari ni bilionea.Hapa namzungumzia mwanzilishi wa kampuni ya Kentucky Fried Chicken(KFC) ambayo kwa sasa iko duniani kote katika nchi 86 na zaidi ya vituo 9,000.

Safari kuelekea mafanikio kwa kila mtu huwa ni tofauti sana lakini kuna mambo ambayo huwa yanafanana kwa watu wengi.Kuanzia siku ambayo umeamua kubadilisha maisha yako na kuanza kuishi ndoto yako hadi siku ambayo utafanikiwa kuitimiza kutakuwa kuna matukio mengi sana ambayo ni lazima uamue kuyashinda kila yanapojitokeza.

Ukiangalia maisha ya Sanders utagundua kuwa alikutana na matukio mengi sana ya kukatisha tamaa katika maisha yake na hakukuwa na namna angeweza kufanikiwa kuinuka tena kama asingechukua mwelekeo tofauti wa maisha yake.Matukio ya kufiwa na wazazi,kunyang’anywa mtoto,kufukuzwa kazi zaidi ya nne ndani ya mwaka mmoja ni matukio ambayo kama usipokuwa makini basi unaweza kuhitimisha kuwa haujaumbwa ili ufanikiwe na ukaamua kukata tamaa kabisa.Kuna watu wengi sana ambao wameruhusu matukio kama haya yasitishe ndoto zao kubwa ambazo zingeweza kuwafanya kuwa mabilionea leo.

Kuna watu kwa sababu ya kuondokewa na wazazi wao hawaoni tena kama wanaweza kufanikiwa maishani,kuna watu kwa sababu ya kufeli mtihani wanaona kama vile mwisho wa maisha ndio umefika,kuna watu kwa sababu ya kuachwa na wapenzi wao wanaona haitawezekana tena kuishi maisha ya furaha tena,kuna watu kwa sababu waliwahi kuanzisha biashara huko nyuma na wakafeli ama wakatapeliwa wanaona hawawezi kuinuka tena.

Somo kubwa toka kwa sanders ni kuwa,bila kujali umeshawahi kufeli mara ngapi na katika mambo gani;bado unayo fursa kubwa sana ya kuweza kufanikiwa.Usikate tamaa,Usikubali uishie njiani kabla haujaiona hatima yako kubwa.You can Rise Again(Unaweza Kuinuka Tena)

Jambo la pili ni kuwa kila wakati tunapojikuta tumeishiwa nguvu za kuendelea mbele na kutamani hata kuondoka duniani,tunatakiwa tujiulize tena-Hivi hakuna kitu ambacho ninacho na kinaweza kubadilisha maisha yangu?-Ukweli ni kuwa kila wakati unapojikuta kuwa mambo yameenda vibaya na ni kama hakuna tumaini tena,unatakiwa kujiuliza swali hili na upate majibu yake.Kila mtu anacho kitu ambacho kama akiamua kukitumia basi kitamfanikisha sana katika maisha yake,na mara nyingi kitu/uwezo huu unaweza kuonekana na mdogo na wa kawaida sana na unaweza kuudharau.

Hebu fikiria kuwa uwezo wa “kupika” ndio umemfanya sanders awe bilionea,vipi kama angeugundua miaka mingi akiwa kijana.Hebu tulia kidogo kwa dakika moja kabla haujaendelea,jiulize-“Hivi nina uwezo gani wa kipekee ambao unaweza kunifanikisha katika maisha yangu?”

Jibu la swali hili ni muhimu sana kuelekea mafanikio yako,unaweza ukawa na jibu zaidi ya moja,lakini ukijiuliza kwa mara nyingine tena utashangaa yanapungua hadi unapata jibu moja mtu.Siku zote usiangalie umaarufu wa kitu bali angalia uwezo wa kipekee ulionao juu ya jambo fulani.Hata kama leo linaonekana ni jambo lisilo na mvuto,kama ukiamua kutumia nguvu,muda na rasilimali zako kujifunza na kuongeza ujuzi kila siku,utashangaa maisha yako yatakavyobadilika.

Jambo la tatu na la muhimu sana ni kuwa,hakuna kuchelewa katika mafanikio-“There is never too late when it comes to success”.Kuna wakatim unaweza kufika kutokana na umri wako ama ukaona kama umejaribu mara nyingi sana na haujafanikiwa basi ukaona haiwezekani tena kufanikiwa.Hebu fikiria kuwa Sanders alikuwa bilionea baada ya kustaafu,nawe pia katika umri au hali yoyote ile uliyonayo unaweza kufanikiwa kufikia kilele cha ndoto yako.Usikubali jambo lolote katika maisha yako likukatishe tamaa,kumbuka kuwa unao uwezo wa kuinuka,kuanza upya na kubadilisha maisha yako kabisa.

Sina shaka kuwa wewe ni mmoja wa watu utakayetengeneza historia katika maisha yako utakapofanikiwa kuitimiza ndoto yako katikati ya vikwazo vinavyokuzunguka.Kama unaamini katika ndoto yako na unajua kuwa utafanikiwa siku moja sema-“Yes I Can”(Ndio naweza).Tafadhali usiache kunishirikisha mafanikio yako na hatua unazopiga kutokana na mambo haya unayojifunza.
Kumbuka kuwa ndoto yako Inawezekana,

Endelea kutembelea
 www.JoelNanauka.Com kujifunza zaidi.
See You At The Top.
©JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website