Navigate / search

Mbinu 3 za Kupata Maarifa Yatakayofanikisha Malengo Yako

22

Tunaishi katika ulimwengu ambao taarifa mpya zinagunduliwa kila siku.Ukweli ni kwamba kama mtu hatakuwa tayari kujifunza kwa bidii na kila wakati basi atajikuta ameachwa nyuma sana katika eneo lake ambalo ameamua kuwa ndio atatumia muda wake wote katika maisha yake.Siku moja nilikuwa na msikiliza Brian Tracy,mkufunzi maarufu sana wa masuala ya mbinu za mafanikio akasema kuwa kwa ulimwengu wa sasa kila baada ya miaka miwili na nusu maarifa yanapotea na yanakuja mapya kabisa.Hii ikimaanisha kuwa kwa kile uanchokijua leo basi baada ya miaka miwili na nusu kitakuwa hakina manufaa kabisa.

Hii ni sababu mojawapo ambayo imewafanya wengi sana kushindwa kutimizia ndoto zao na malengo yako kwani kila wakati wamejikuta wameachwa nyuma.Hata wewe unaweza kujiuliza hivi ni lini mara ya mwisho ulichukua hatua za makusudi kujifunza kitu kipya katika eneo lako unalofanyia kazi?Ni lini ulihudhuria kozi kujifunza zaidi?Ni lini ulisoma kitabu kuhusiana na taaluma yako?Kuna watu wengi ambao tangu wamalize masomo yao ya chuo hawajawahi kusoma chochote tena kinachohusiana na kile walichosomea,halafu bado wanatarajia kuwa watafanikiwa zaidi kuuliko watu wengine.

Mafanikio katika maisha hayaji kwa sababu za uzoefu wa kile unachofanya,yanakuja kwa sababu una maarifa yanayotakiwa na muhimu ya kukusaidia kufanya kile unachofanya kwa namna ya ufanisi zaidi.Ili utoke hapo ulipo ni lazima upate maarifa ambayo haujawahi kuwa nayo hapo kabla katika maisha yako.Kama kiwango cha maarifa ulichonacho katika maisha yako kwa leo kinafanana na kile cha jana basi itakuwa ni kujidnaganya kabisa kuwa eti unataka kuwa na malengo makubwa.

Haijalishi una malengo makubwa kiasi gani katika maisha yako,kama wewe ni mtu ambaye hauko tayari kufanya bidii kuongeza maarifa kila siku basi hatua zako zitakuwa taratibu sana.Kuna mambo matatu ya kukusaidia ili kuongeza maarifa yako katika kile unachofanya na kuhakikisha kuwa unapiga hatua kwa kasi kuanzia leo.

Moja ni lazima muwe mtu ambaye uko tayari kusikiliza zaidi kuliko kuongea.Dalai Lama aliwahi kusema unapozungumza ni kwamba unarudia unachokijua,lakini unaposikiliza ndipo unapojifunza kitu kipya katika maisha yako.Usiwe aina ile ya watu ambao wao kila kitu wanakijua katika maisha yao na huwa hawawapi wenzao nafasi ya kuzungumza.Kila unayekutana naye katika maisha yako kuna kitu unacho cha kujifunza kwake.

Kuna watu wana kitu kinaitwa kiburi cha akili(Intellectual arrogance);hawa ni aina ya watu ambao wanaamini wanachojua na wanachosema wao ndio sahihi kabisa kuliko mtu mwingine yeyote na pia wanaamini wao ndio wanatakiwa kusikilizwa zaidi.Ukiwa nao kwenye majadiliano kila wakati wanataka wazo lao ndio likubaliwe na wote na lisipokubaliwa basi huwa wanachukia.Ukiwa mtu wa namna hii huwezi kujifunza kitu kipya katika maisha yako.Kila siku inapoanza dhamiria kujifunza kitu kipya toka kwa kila utakayekutana naye.Mwingine utajifunza mambo amzuri ya kuyafanya,mwingine utajifunza mambo mabaya ya kuyaepuka lakini kwa kila mtu unayekutana naye lazima kuna kitu unatakiwa kujifunza toka kwao.

Jambo la pili katika kujifunza,ni lazima utenge muda wako mzuri wa kujisomea.Ukianza kusema hivi kila wakati utasikia mtu anakuambia hana muda kabisa.Lakini mtu huyohuyo anayesema hana muda wa kusoma huwa na muda wa kuangalia tamthilia na kufuatilia kila siku bila kukosa,mtu huyohuyo anaweza kufautilia mechi za mpira wa miguu uingereza bila kukosa,mtu huyohuyo anaweza kupata muda wa kuchart kwenye group bila tatizo lolote lile.Kiufupi ni kwamba kinachowafanya watu wengi washindwe kujisomea si kwa sababu hawana muda wa kutosha bali kwa sababu hawajatoa kipaumbele.Kama kweli unataka kufanikiwa katika maisha yako,ni lazima kila siku utenge muda wa kuongeza maarifa mapya katika kile unachofanya.Leo weka mpango maalumu wa namna utakavyoanza kujisomea na kupongeza maarifa kila siku aktika kile unachokifanya.

Njia ya tatu ni kujifunza kwa wale waliotangulia na kufanikiwa katika kile ambacho umeamua kukifanya katika maisha yako.Katika kila ambacho umeamua kukifanya kuna watu ambao walishatangulia na wakakifanya kwa mafanikio,kazi kubwa uliyonayo ni kuamua kujifunza kutoka kwao.Mafanikio yanaongozwa na kanuni ya kichocheo na matokeo(cause and effect);ambayo inasema kwa koila mafanikio ambayo mtu anayo basi kuna kitu alifanya hadi akafanikiwa na wewe kama utaamua kufanya walichofanya basi ana wewe bila shaka utafanikiwa.

Kwa kuijua kanuni hii unatakiwa uanze kufanya bidii kutafuta waliotangulia katika eneo lako na kuanza kujifunza namna walivyoanza hadi kufika hapo walipo leo ambapo na weew unatamani.Antony Robins aliwahi kusema,Mafanikio huacha alama njiani hivyo kama unaweza kuzifuatilia basi utafika katika mafanikio.Inwezekana ikawa ngumu kuwafikia uso kwa uso ambao unatamani kujifunza kwao,lakini unaweza kutumia vitabu walivyoandika CDs/DVDs walizotoa ama hata historia za maisha yao walioandika.Watu wanaofanikiwa ni wale ambao wako tayari kujifunza kwa bidii kutoka kwa waliotangulia na kuchukua mazuri wanayoona yanaendana na wanachotaka kufanya kisha wanayafanyia kazi.

Kukosa maarifa yanayotosha katika kile unachokifanya kunaweza kuwa ni kikwazo kikubwa cha kukufanya ushindwe kabisa kutimiza malengo makubwa katika maisha yako.Amua kuanzia leo kutafuta maarifa kwa bidii na kasi ambayo inatakiwa ili ujitoe katika kundi la watu wanaokwama kutimiza malengo yao.

Kumbuka kuwa ndoto Yako Inawezekana ,

Endelea kutembelea www.JoelNanauka.Com ili Kujifunza zaidi.

See You At The Top.

©JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website