Navigate / search

Matumizi makubwa serikalini chanzo cha umaskini wa kujitakia

Ripoti ya IMF-Tanzania imethibitisha hilo

Mara tu baada ya nchi za Afrika kupata uhuru katika miaka ya 1960 zilijikita katika harakati kubwa za kujikwamua kutoka katika utegemezi wa uchumi kwa wageni.Juhudi hizi ziliendeshwa na kauli mbiu maarufu ya “Africanisation”-Madaraka kwa waafrika katika kila sekta.Hii ilifanyika bila kujali utaalamu uliokuwa unahitajika na ilisababisha viwanda vingi tulivyorithi toka kwa wakoloni kufa kwa kasi na nchi za afrika zilijikuta katika hali ngumu ya uchumi tena.Nchi nyingi ziligeukia kutafuta mikopo na misaada kutoka kwa wakoloni walewale ambao iliwafukuza hapo kabla.

Mikopo na misaada hii ilitengeneza mwanya mkubwa kwa viongozi waliokuwa serikalini kujichotea mabilioni kutoka katika Benki kuu ambazo mamlaka ya uendeshaji wake ilikuwa kwa wanasiasa.”Mentality”-Fikra ya matumizi hovyo ya fedha za serikali zimeendelea hadi leo hii katika nchi nyingi za afrika,na ndio chanzo kikubwa cha upotevu wa rasilimali fedha za nchi nyingi ikiwemo Tanzania.Wengi wanaofaya hivyo husema kuwa “cha serikalli hakina mwenyewe”.

Mwezi wa pili mwaka huu,ujumbe wa IMF ulitembelea nchini ukiongozwa na mtaalamu wake bwana Paulo Mauro.Katika ripoti yake aliyoitoa ilichambua kwa undani mwelekeo wa bajeti ya Tanzania ikiwa katika robo yake ya mwisho ya mwaka wa kifedha.Ripoti hiyo ilionyesha kuwa kumekuwa na upungufu wa kibajeti kiasi cha shilingi bilioni 847,ambayo kwa maelezo ya mtaalamu huyo yametokana na kuweka malengo ya mapato yasiyo halisi kabisa.

Serikali ilikuwa inategemea mapato makubwa kutoka katika kodi ya kadi ya simu(simcard tax) ambayo ilipingwa sana na wananchi kwani ilionekana ya kinyonyaji na ni kama kurudisha kodi ya kichwa ya wakati wa mkoloni.Lakini pia ripoti imeeleza kuwa pesa nyingi za serikali zimekuwa zikiwekezwa katika maeneo ambayo hayana tija kwa uchumi mkubwa wa nchi,kwa maneno mengine imewekeza katika kuendesha shughuli za serikali zaidi-mishahara na posho (recurrent expenditures) kuliko kwenye miradi ya maendeleo(development expenditures) ambayo ingeleta tija kwa wananchi na kutengeza ajira nyingi na kuongeza pato la wananchi.

Kilichosikitisha katika ripoti hiyo sio kushindwa kwa serikali kukusanya mapato katika sekta kubwa na “kukomalia” kuwakamua zaidi walalahoi bali ni ule ukweli kuwa katika kipindi hicho mapato ya serikali yameongezeka kwa asilimia 0.2 ukilinganisha na mwaka uliopita ila matumizi yaliongezeka kwa asilimia 0.8.Hii ni kusema katika ugumu wa kukusanya mapato,bado viongozi wetu waliendelea “KUTUMIA ZAIDI,KULIKO WANACHOPATA”.

Huitaji kuwa mchumi wa kiwango cha juu kujua kuwa ukitumia zaidi ya kipato chako,utajilimbikizia madeni na utabaki kwenye dimbwi la umaskini.Nadhani katika hili hatuhitaji IMF wala Benki ya dunia kutushauri,ni kutumia akili zetu za kawaida.Kama viongozi wetu wataendelea namna hii,kujikwamua kutoka katika umaskini itakuwa bado ni safari ndefu.

TUJISAHIHISHE!!!

Leave a comment

name*

email* (not published)

website