Navigate / search

Matokeo Ya Utafiti-Jambo Kubwa Lililowasaidia Watu Wengi Kutimiza Malengo Yao

Kuna watu wengi sana huwa wanadhani kitu ambacho kitawasaidia sana kwenye maisha yao kufanikiwa ni kupewa hamasa kila wakati ili waweze kusonga mbele katika kile kitu ambacho wanakifanya.Hata hivyo kuna siri kubwa sana ambayo kama hautaijua basi kwenye maisha yako yote itakufanya ushindwe kufikia kilele cha mafanikio yako kwa wakati muafaka.Hamasa huwa inakusaidia kuanza jambo ila haina nguvu ya kukufanya uendelee kufanya jambo hilo siku zote,kwa sababu hamasa huwa ina tabia ya kupungua nguvu kadiri muda unavyozidi kwenda.
Jarida la uingereza la British Journal of Health Psychology lilijaribu kufanya utafiti ili kuona ni mara ngapi watu wanafanya mazoezi kwa muda wa wiki mbili.Katika utafiti huu walijaribu kuwachukua watu wazima 248 na wakawaweka katika makundi matatu tofauti.
Kundi la kwanza lilikuwa linaitwa “Contorl Group” na hawa waliambiwa kwa wiki mbili zijazo waandike kila siku ambayo watakuwa wanafanya mazoezi.Na kabla hawajanza waliambiwa kila mmoja asome kitabu cha hadithi(Novel) ambayo ilikuwa haihusiani kabisa na masuala ya mazoezi ama afya.
Kundi la pili liliitwa “Motivation Group” hawa waliambiwa pia waandike kila siku ambayo watafanya mazoezi katika hizo wiki mbili.Lakini pia waliambiwa kila mmoja asome kijarida kidogo kilichokuwa kinaelezea faida za kufanya mazoezi na namna unavyoweza kujiepusha na matatizo ya magonjwa ya moyo.Kundi hili pia waliambiwa,watu wengi ambao walizingatia ratiba zao za mazoezi na kufanya mazoezi mara kwa mara huwa hawapati matatizo ya magonjwa ya moyo.Kusudi kubwa lilikuwa ni kuhakikisha kuwa wanapata hamasa ya kufanya mazoezi mara kwa mara.
Kundi la tatu lilikuwa linaitwa “Intention Group” hawa walifanyiwa kwanza kama lilivyokuwa kundi la pili ili kuhakikisha kuwa na wao wana hamasa ya kufanya mazoezi.Ila kitu cha zaidi katika kundi hili ilikuwa ni kuambiwa waandike mpango wao wa wapi na saa ngapi watafanya mazoezi yao katika huo muda wa siku mbili.Walielekezwa waandike kuwa “Katika wiki mbili zijazo nitafanya mazoezi angalau kwa muda wa dakika 20 siku fulani(unazitaja) na muda fulani(Unataja) na mahali fulani(Unataja pia)”
Baada ya maelekezo haya makundi yote yaliachwa na baada ya wiki mbili yalipatikana matokeo yafuatayo kwa makundi yote matatu:
• Kundi la kwanza la “control group” 38% ya wahusika walifanikiwa kufanya mazoezi angalau mara moja kwa wiki.
• Kundi la pili la “motivation group” 35% ya wahusika walifanikiwa kufanya mazoezi angalau mara moja kwa wiki.
• Kundi la tatu la “intention group” 91% ya wahusika walifanikiwa kufanya mazoezi. Angalau mara moja kwa wiki.
Hitimisho lilikuwa ni kwamba kwa kuandika tu wapi na lini wanakusudia kufanya mazoezi washiriki wa kundi nambari tatu walifanikiwa zaidi ya makundi yote ikiwemo hata lile ambalo waliambiwa na kusisitiziwa umuhimu wa kufanya mazoezi ili kuwatia hamasa.
Matokeo ya utafiti huu ni muhimu sana kwa kila mtu ambaye anatamani kufanikiwa kutimiza malengo fulani katika maisha yake.Nguvu kubwa ambayo unayo ya kukusaidia kuweza kutimiza malengo uliyonayo katika maisha yako ni uwezo wako wa kujipangia malengo ya kitu unachotaka kufanya na usikubali kuacha tu bila kuweka mahali na muda ambao unataka kukifanya.
Kwa chochote kile ambacho unakusudia kukifanya katika maisha yako jiulize-Hivi nimeweka malengo yanayoonyesha nitakifanya wapi na muda gani?Kama unataka kufanya mazoezi basi weka muda na mahali na siku.Kama unataka kuanza kuweka akiba ya pesa zako benki,basi weka kiwango utakachoweka,muda na utaweka kila tarehe ngapi.Kama unataka kuanza kusoma vitabu basi chagua vitabu unavyotaka kusoma,utakuwa unasoma muda gani na utakuwa unasomea wapi.Kadiri ambavyo utakuwa unaweza kuchambua kwa ufasaha WAPI,LINI,na SAA NGAPI basi ndivyo utakavyozidi kuongeza uwezekano wa kufanikiwa katika lengo lako.
Leo,jaribu kupitia malengo uliyonayo na ujiulize kama yamekidhi vigezo hivi.Siku zote jitahidi kutoka katika kundi la kwanza na la pili na ujilazimishe kuwa katika kundi la tatu kwani wote ambao wamefanikiwa na kutimiza malengo makubwa katika maisha yao huwa wako kundi la tatu.
See You At The Top
@JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website