Navigate / search

MAMBO MAKUBWA 3 YALIYOMFANYA MUCHEMI AWE MILIONEA AKIWA KIJANA

danson-muchemi1

Hivi karibuni gazeti moja la nchinui Kenya lilichapisha habari ya kijana mmoja kwa jina la Danson Muchemi ambaye alizaliwa miaka ya 80 mwanzoni lakini kwa sasa ana utajiri unaokadiriwa kufikia shilingi za kikenya milioni 400.Kijana huyu ndiye anayemiliki mtandao wa JamboPay ambao unatoa huduma za malipo mtandaoni zake katika nchi za Kenya,Tanzania na Senegal zikiwahudumia zaidi ya wateja 1,500.

Muchemi ambaye amesoma shahada ya Mawasiliano na teknolojia ya habari katika chuo kikuu cha Kenyatta alianza kupenda masuala ya ujasiriamali akiwa bado yuko chuoni.Alianzisha biashara aliyoiita “Movie Library Bussiness” ambayo alichokuwa anafanya ni kurekodi lecture zote ambazo walimu wake wanafundisha na kisha kuziweka katika CDs na kuziuza kwa wanafunzi wenzake hasa wale ambao walikuwa wameshindwa kuhudhuria madarasa,na alikuwa akiuza kati ya shilingi 250 hadi 100 kulingana na uhitaji wa CD husika.
Baada ya kumaliza chuo ndipo alipoanza biashara ya malipo ya mtandao kwenye chumba kidogo  kwa miezi 6 na akawa anatumia komputa ya kukodisha ambayo alikuwa analipa Ksh 4500 kwa mwezi.Anasema alikuwa anaingia kazini kwake kila siku kabla ya saa mbili asubuhi hata kama hakukuwa na mtu wa kumsimamia.

Miaka ya mwanzoni anasema alipata shida sana kupata wateja wa huduma yake na pia hakuweza kutengeneza kipato kilichoweza kumfanya aishi maisha aliyokuwa anayatamani,kuna wakati alipata hasara ya shilingi milioni 3 kwa sababu hakuwa na uzoefu.
Aliendelea kuvumilia hadi ilipofika mwaka 2010,akiwa na miaka 25 ndipo alipopata mkataba wa kufanya huduma na benki moja na huu ndio ulikuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa katika bishara yake.

Katika mahojiano yake anasema,kitu kikubwa kilichomsadia ni nidhamu ya kazi na kutokukata tamaa.Anasema kila siku alikuwa anajiambia-Kesho nitafanikiwa,hata kama hakukuwa na dalili yoyote ile ya kuonyesha kuwa anakaribia kufanikiwa.

Kampuni yake kwa sasa ni kubwa sana na mwaka 2013 ilipata tuzo toka kampuni ya google,ikiitaja kuwa ni kampuni inayoibukia kwa ubunifu katika teknolojia.
Maisha ya Mucheni yanafanana na maisha ya watu wengi katika bara la afrika na dunia kwa ujumla.Iwapo kama angeamua kuishi maisha ya kawaida kama watu wengine basi pengine leo angebakia kuwa mtu wa kawaida sana na dunia isingemfahamu,lakini Mucheni aliamua kufanya jambo la tofauti katika maisha yake.

Kuna masomo makubwa ya kuvutia katika maisha ya Mucheni:
Kwanza ni kuwa alitumia uhitaji uliokuwa unamzunguka na kuugeuza kuwa biashara.Katika maisha yetu ya kila siku tumezungukwa na uhitaji wa aina mbalimbali ambao mtu yeyote anayeamua kutatua basi anajitengenezea fursa nzuri ya biashara katika maisha yake.Alipogundua kuwa kuna wanafunzi huwa wanakosa kuhudhuria madarasa lakini wangependa sana kupata mafunzo yaliyotolewa akaona atatue tatizo hilo.

Utajiri ni matokeo ya kutatua matatizo yanayowakabili wengine ambayo wenyewe wameshindwa/hawataki kuyatatua.Kila mtu alipo kuna uhitaji,hata wewe ulipo hapo leo kuna uhitaji-Hebu jiulize kuna uhitaji gani katika eneo lililopo ambao watu wengi wanasumbuka?Ukipata jibu basi hilo ni wazo la biashara anza kulifanyia kazi.
Pili ni kuwa Muchemi alikuwa tayari na kuanza na kidogo alichonacho.Hebu fikiria mtu ana usongo na ndoto yake hadi akaamua kukodisha kompyuta?.

Hakuwa tayari kutumia kisingizio cha kutokuwa na kompyuta kumfanye ashindwe kutimiza ndoto yake.Kuna watu wengi leo ambao wanashindwa kuanza kufanya mambo wanayotaka kuyafanya na kisingizio pekee walichonacho ni kuwa hawana pesa,hawana mtaji n.k.Hebu jiulize,katika kile unachotaka kufanya unaweza kuanza na nini?Usikubali hata kidogo uache kuanza eti kwa sababu hauna pesa au sapoti ya kutosha.Kila wakati anza na ulichonacho na anza pale ulipo vile unavyoweza.

Jambo la tatu ni kuwa Muchemi hakukata tamaa hata kidogo.Kuna wakati alilala na njaa,kuna wakati wenzake walikuwa wanapata mshahara mkubwa na kila mtu alikuwa anamwambia atafute ajira,kuna wakati alipata hasara kubwa katika biashara yake na ikaonekana kama vile hawezi tena kufanikiwa,kuna wakati alitishiwa kufungiwa ofisi kwa kushindwa kulipa kodi kwa wakati-Lakini kutokana na uvumilivu na nidhamu ya kazi leo amefanikiwa na amesahau maumivu yote.

Mucheni alikuwa anaripoti katika “kiofisi” chake kabla ya saa 2 kila siku,ndio maana leo haishangazi kumuona amefika hatua kubwa namna hii.Kuna watu wameajiriwa ama wamejiajiri hawana nidhamu kabisa ya kazi-Wanaamka muda wowote wanaotaka na wanaondoka muda wowote,halafu wanategemea watafanikiwa,Jifunze kwa Mucheni.

Kama hauwezi kuwa na nidhamu ya kazi bila mtu kukusimamia basi ujue hicho ni kikwazo kikubwa sana kukelekea mafanikio yako.

Ndivyo inavyokuwa ni lazima uamini katika kutokushindwa na ukatae kukata tamaa katika maisha yako.Kitu kimoja ambacho lazima ujue na lazima ukikubali ni kuwa kuna wakati unaweza kupata hasara,kuna wakati utaona kama vile mambo hayaendi,kuna wakati utatamani kubadilisha ndoto yako na uanze kuishi ndoto rahisi-Kumbuka,ili ufanikiwe kwa kiwango cha juu zaidi ni lazima ukubali kushinda changamoto kubwa zaidi katika maisha yako.

Sina shaka kuwa na wewe ni Muchemi ajaye katika kile unachofanya kwa sasa.Naamini sana katika uwezo ulio ndani yako,naamini sana katika ndoto yako-Naamini nitakutana na wewe siku moja ukiwa umefanikiwa sana na dunia itakutaja kama mmoja wa watu mashuhuri waliofanikiwa.Tanzania inakusubiri,Afrika Inasubiri uonyeshe uwezo wako na Dunia inasubiri uanze kuiishi ndoto yako.

Kumbuka Kuwa ndoto yako Inawezekana,
Endelea kutembelea www.JoelNanauka.Com ili kujifunza zaidi.
See You At The Top

Leave a comment

name*

email* (not published)

website