Navigate / search

MAMBO 3 YATAKAYOHARAKISHA MAFANIKIO YAKO

monitor-840624_640

Kila mtu anatamani kufanikiwa kwa kiwango cha juu sana lakini ukweli ni kuwa si kila mtu atafanikwia kama anavyotaka.Watu wengi sana hushindwa kufanikiwa katika maisha kwa sababu mbalimbali:

Wa kwanza ni wale ambao kila siku wanatamani tu kufanikiwa lakini hawajawahi kuchukua hatua,hawa huwa wanaitwa “wishers”.Ni aina ya watu ambao kila ukikutana nao watakuambia jinsi ambavyo wanatamani kuwa kama watu fulani.Mara nyingi watu hawa huwa wanatamani sana mafanikio,lakini hofu yao ya kushindwa ni kubwa kuliko shauku yao ya kufanikiwa kwa sababu hiyo huwa hawachukui hatua hata siku moja.

Watu wa namna hii huu wanajua mambo mengi sana kuhusu mafanikio,wanawea kuwa wasomaji wazuri,wanafahamu historia za matajiri na wanaweza kukueleza kinagaubaga lakini hawajaribu kufanya hata kitu kidogo.

Pili ni wale watu ambao huwa wanachukua hatua ila hawafanyi kwa nguvu zote.Aina hii ya watu ni wale ambao wako haraka sana kujiingiza katika kuanza kufanya kitu fulani lakini huwa hawaweki nguvu zao kwa 100%.Ni watu ambao huwa “wanadonoa” kidogo kila mahali na kila wakati.Kila siku utawakuta wako bize kufanya jambo fulani lakini wanafanya kizembe na matokeo yake huwa wanapata matokeo kidogo sana au huwa wanafeli mara nyingi katika kile wanachokifanya na hivyo huwa hawapigi hatua kubwa maishani na hii huwakatisha tamaa.

Tatu ni wale ambao wanaamini kufanikiwa ni bahati,na mtazamo wao ni kuwa kuna siku kitatokea kitu fulani cha ghafla katika maisha yao na watabadilika.Aina hii ya watu huwa wanasubiri kitu kisicho cha kawaida kitokee katika namna ya muujiza ili kiwafanikishe.Staili yao ya maisha ni kuwa,kama wameandikiwa kufanikiwa basi kuna namna itatokea na watafanikiwa.

Hawa ni aina ya watu ambao wanapenda kila kitu “kumsakizia” Mungu.Utasikia Mungu hajapenda niwe tajiri,Mungu akipenda nitafanikiwa asipopenda basi.Wanachosahau ni kuwa shauku ya Mungu ni kuwa kila mtu aishi maisha mazuri hapa duniani.Watu wa namna hii hujaa na visingizio kila wakati kuhalalisha kutofanikiwa kwao.

Hata hivyo ili kufanikiwa kuna kanuni mbalimbali ambazo kama ukiamua kuzizingatia basi zitakusaidia kuongeza kasi ya kufika kule ambako unataka kufika katika kutimiza malengo yako.Leo ningependa uyatambue mambo matatu ambayo ni muhimu kwako kukusaidia kufanikiwa bila kuchelewa.Mambo haya yatakusaidia kuvunja hali ya kudumaa (stagnation) katika maisha yako.Kuna watu kila siku wako vilevile na hakuna mabadiliko yoyote wanayoyapata katika maisha yao,mambo haya matatu yatakusaidia kuhakikisha kuwa hali hiyo haitakuwepo katika maisha yako:

Cha kwanza ni kuwa unatakiwa uamue kuwa bora kuliko watu wa kawaida katika kile unachokifanya.Haijalishi unajishughulisha na jambo gani katika maisha yako,mafanikio siku zote huenda kwa watu walio bora kuliko watu wa wastani katika maisha yao.Kanuni za kiuchumi zinaonyesha kuwa mara zote ni 20% ya watu katika eneo fulani/taaluma(field) ndio hupata 80% ya mapato yote yaliyopo katika eneo hilo.

Hii ni sawa na kusema kama wauzaji wote wa vifaa vya kielektroniki katika mkoa wako huwa wanaingiza milioni 100 na wako wafanya biashara 10,basi wafanyabiashara wawili katika hao ndio huingiza milioni 80 na wafanyabiashara wanane waliobaki hugawana hizo milioni 20 zilizobakia.Kanuni hii imetokana na kanuni maarufu iliyotungwa na mwanauchumi nguli wa italia,Alfred Pareto.Hivyo kwa chochote ambacho umeamua kufanya basi amua kuwa bora kupita mtu wa kawaida katika eneo hilo.Utafiti unaonyesha kuwa mtu wa kawaida husoma kitabu kimoja kwa mwaka,hivyo wewe ukiamua kusoma kitabu kimoja kila mwezi kuhusiana na eneo lako(field),ndani ya miaka kadhaa utajikuta umekuwa katika watu bora wa juu kabisa.

Cha pili ni kuwa kwa chochote unachofanya,basi fanya kwa kiwango kikubwa(Do it massively).Achana na hii tabia ya “kubeep” kila eneo na kujaribu kufanya kila kitu.Watu wengi wanafeli kwenye maisha kwa sababu huwa ni watu ambao kila siku wanafanya mambo kwa kujaribu ili waone kama watafanikiwa ama la,HAPANA.Kama kweli unataka kufanikiwa basi usiwe mtu wa kujaribu,uwe mtu wa kufanya.Kama umeamua kulima,basi uwe “serious”(ulime kama mkulima kweli),kama umeamua kufanya biashara basi ufanye kwa kumaanisha,achana na mambo ya kujaribu kila siku.Maisha si jambo la majaribio,na kila muda ambao unaupoteza basi hautarudi tena.Kama una lengo la kuwa mkulima hata kama unaanza kidogo,weka malengo yako kuja kuwa mkulima wa maelfu ya mahekari na kusafirisha nje,na kuwa na viwanda vya kuchakata bidhaa zako,kama unataka kuwa msanii jipange uwe wa kimataifa,kama unataka kuinuka katika taaluma yako jiwekee malengo ya kufanya katika makampuni ya kimataifa au kuwa na vyeo vya juu sana,kama unataka kufanya biashara jipange kwa namna ya kuja kuwa zaidi ya mabilionea waliopo sasa.

Cha muhimu hapa ni kuwa,ndoto yoyote uliyonayo basi ifanye kwa kiwango kikubwa,hata kama leo unaanza kidogo basi fanya kwa kiwango cha juu katika hicho kidogo.
Kitu cha tatu cha kuzingatia ni kuwa lazima uwe na mwendelezo (consistence) wa kile unachokifanya.Katika safari ya mafanikio kuna kitu kinaitwa “momentum of success”(Nguvu ya mwendelezo ya mafanikio).Kama umeshawahi kuendesha baiskeli hii utakuwa unaifahamu.Unapoanza kuendesha itakuwa ngumu kidogo lakini ukishachanganya vizuri basi kuna wakati unaweza kuacha kuchanganya na ikaendelea kwenda mbele.

Hiki ndicho kilichopo kwenye mafanikio,unatakiwa kufanya kitu kwa mwendelezo hadi pale ambapo utakuwa umetengeneza nguvu ya mwendelezo wa kutosha kiasi kwamba mambo yataanza kujiendesha yenyewe.Hii huja baada ya wewe kuamua kufanya jambo fulani kwa muda mrefu bila kuchoka ama kukata tamaa hata kama hauoni matokeo yake kwa wakati huo.

Kwa chochote unachofanya sasa hivi,inawezekana hakuna mtu ambaye anakusifia,au hauoni matokeo yake-Kama kweli unataka kufanikiwa usichoke na usiachie njiani.Inawezekana hauuzi kama ulivyotarajia,ama haujavuna kama ulivyokuwa umepanga,ama haupandishwi cheo kama ulivyotarajia,kanuni ni moja tu-Endelea kufanya hadi uone matokeo.
Sina shaka kuwa kuna siku utafikia malengo yako uliyojiwekewa na utafanikiwa sana katika maisha yako.Kumbuka kuwa ndoto yako inawezekana.

Kumbuka Kuwa ndoto yako Inawezekana,
Endelea kutembelea www.JoelNanauka.Com ili kujifunza zaidi.
See You At The Top

Leave a comment

name*

email* (not published)

website