Navigate / search

MAMBO 3 YALIYOMTOA J.K RAWLINGS TOKA KWENYE UMASKINI

jk

Ukitaja Harry Porter watu wengi wanajua kuhusu Movies na Vitabu maarufu sana vilivyoandikwa na Mwandishi maarufu wa uingereza J.K Rowling ambaye amefanikiwa sana kupitia kazi zake za uandishi.Lakini kitu ambacho watu wengi hawajui kuhusu J.K Rawalings ni mambo aliyoyapitia katika maisha yake hadi kufika hapo alipo sasa hivi.

Mwaka 1990 ndio kwa mara ya kwanza alipata wazo la kuandika kuhusu Harry Porter na wazo hili lilikamilika zaidi alipokuwa safarini kwenye treni akitokea Manchester kwenda London.Mara baada ya kuona ni wazo linaloweza kubadilisha maisha yake aliamua kulifanyia kazi kwa haraka na akaanza kuandika kwa bidii sana.Hata hivyo,mwaka huohuo mama yake alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Miaka miwili baadaye alihamia ureno ambako alianza kuwa mwalimu wa lugha ya kiingereza ambako pia alikutana na mwanaume ambaye alimuoa na alipata mtoto wa kike.Mwaka mmoja baadaye (1993) aliachwa na akaamua kurudi uingereza kwenye mji wa Edinburg wakati huo alikuwa tayari ameandika sura 3 za kitabu chake cha Harry Porter.Aliporudi Uingereza maisha yalikuwa magumu saidi na alijiona kama vile ndoto yake ya kuandika kitabu imeshakufa kwani alikuwa hana kazi,ameachwa na ana mtoto wa kumtunza.Ghafla akajikuta yuko kwenye msongo  mkubwa wa mawazo(stress) na mfadhaiko(depression) mkubwa sana.Hivyo aliamua kujiorodhesha katika mpango wa serikali  ambao unasaidia watu maskini(Government welfare program).

Mwaka 1995 alijaribu kupelekea kitabu chake kwa wachapishaji zaidi ya 12 na wote walikataa kuchapisha kitabu chake lakini mwaka mmoja baadaye kampuni moja ndogo(Bloomsbury) sana ikakubali na kumchapishia kopi 1000 tu na huku 500 zikagawiwa kwenye maktaba na alilipwa paundi 1500 za utangulizi.Miaka miwili baadae(1997 na 1998) kitabu chake kikashinda tuzo toka Nestle Smarties na British Book Award kama kitabu bora cha watoto cha mwaka.Baada ya hapo Rowling ameuza zaidi ya kopi milioni 400 ya kitabu chake na ndio anachukuliwa kama mwandishi mwenye mafanikio zaidi nchini Uingereza.

Ukiyachunguza maisha yake kuna mambo matatu yanyoweza kukusaidia pia kufanikisha ndoto Yako:

Moja ni kuwa alianza kubadilisha maisha yake kwa kupata wazo na kuanza kulifanyia kazi.Mafanikio yako yamefichwa katika uwezo wako wa kuwa makini na mawazo unayopata na kuanza kuyafanyia kazi.Ubongo wa mwanadamu umejaliwa nguvu ya ubunifu na kila siku utapata mawazo katika akili yako ambayo kama ukiamua kufanyia kazi angalau moja tu,utafanikiwa sana.
Watu wote ambao unaona wamefanikiwa sana ni wale ambao walipata wazo juu ya kufanya jambo fulani na kuamua kuanza kulifanya.

Najua hata wewe umekuwa ukipata mawazo fulani fulani:Pengine ni mawazo kuhusiana na aina ya biashara ya kufanya au ubunifu fulani,pengine ni wazo juu ya kuuza bidhaa fulani ama kutoa huduma.Inawezekana kwa sasa ukiangalia unaona kama vile ni wazo ambalo haliwezi kutekelezeka,jambo la msingi unalotakiwa kujua ni kuwa mawazo yako yana nguvu ya kukufanikisha.Anza kuwa na tabia ya kuwa na daftari/diary ya kuandika mawazo unayopata na kila wakati uwe unayafanyia kazi.

Pili ni kuwa Rowling hakusema angoje kusomea uandishi ama kuwa maarufu ili aanze kulitekeleza wazo lake.Alichofanya ni kuanza kuandika pamoja na kukosa sapoti yoyote kwa wakati huo.Mara nyingi wengi hutaka kusubiri hadi hatua fulani au afikie viwango vya juu zaidi ili waanze kuziishi ndoto zao.Leo,hebu fuata nyayo za Rowling,anza kuchukua hatua ndogondogo kwa kile ambacho unaamini ni wazo lako “litakalokutoa” katika maisha yako.

Usiseme hakuna anayekujua,usiseme hauwezi,usiseme unasubiri uwe na pesa nyingi:HAPANA.Kwenye kila wazo unalopata kuna mahali pa kuanzia.Jiulize,hivi kwa wazo nililonalo leo,ni wapi natakiwa kuanzia?

Jambo la tatu ni kuwa Rowling hakuruhusu kukataliwa kwa wazo lake kumfanye aache kulifuatilia ili kulifanikisha.Inashangaza sana;hivi unaweza kufikiria mtu aliyekataliwa na makampuni makubwa ya uchapishaji leo wanaomgombania wamchapishie vitabu vyake?Hebu fikiria mtu ambaye kuuza kopi 500 kwa mwaka wa kwanza wa kitabu chake kwa sasa ameuza zaidi ya kopi milioni 400?

Hapa ndipo nguvu ya kuamini ndoto yako inapotakiwa.Kila wakati utakapojaribu kutimiza na kutekeleza wazo fulani la maisha yako utakutana na vikwazo na vizuizi vya kutosha,tena sio mara moja bali mara nyingi.Unachotakiwa kujua ni kuwa kama utaendelea kung’ang’ania kidogo zaidi basi kuna mlango mkubwa sana utafunguka mbele yako siku si nyingi.

Usijali umetafuta kitu mara ngapi imeshindikana,umeomba mkopo mara ngapi imeshindikana,umewaeleza watu ndoto yako mara ngapi ili wakusaidie na hakuna anayekuunga mkono,unachotakiwa kufanya ni kuendelea kujaribu tena na tena na tena.Hakuna Kuacha hadi umefanikiwa.

Kumbuka Kuwa ndoto yako Inawezekana,
Endelea kutembelea www.JoelNanauka.Com ili kujifunza zaidi.
See You At The Top

Leave a comment

name*

email* (not published)

website