Navigate / search

Mambo 3 Ya Kuzingatia Unapokataliwa

slide-2

Ili ufanikiwe ni lazima uishinde hali ya kukataliwa pale unapokuwa unatafuta kutimiza malengo yako.Wakati fulani nilikuwa namsikiliza aliyekuwa mchezaji maarufu sana wa mpira wa kikapu nchini Marekani,Michael Jordan akiwa anahojiwa.Alipoulizwa ni kitu gani kilimfanya hadi akafikia kilele kikubwa sana cha mafanikio jibu lake lilinishangaza sana.

Jordan anasema kuna wakati akiwa chuoni alitamani sana kuchaguliwa kuwa kwenye timu ya chuo ya mpira wa kikapu.Kwa bahati mbaya sana uteuzi ulipofanyika,jina lake lilikatwa na  hivyo alishindwa kuteuliwa.Mara baada ya tukio hili alirudi nyumbani kwake na akajifungia chumbani na akaanza kulia sana kwa uchungu kwani aliona kama vile ndoto yake ya kuwa mchezaji bora imefika mwisho,lakini baadaye akapata wazo na akajiuliza-Hivi kwa nini sijachaguliwa?akajipa jibu kuwa ni kwa sababu hajawa mchezaji mzuri zaidi kuliko wale waliochaguliwa.

Baada ya kujipa jibu hili,Jordan aliamua kuanza kufanya mazoezi makali ili kuboresha uwezo wake na hatimaye aliweza kufanikiwa kufikia kilele cha malengo yake.
Kwenye kuelekea katika ndoto yako hauwezi kuepuka kukataliwa katika mambo fulani.Unaweza kukataliwa unapoenda kuomba kazi,unaweza kukataliwa unapoenda kuuza bidhaa,unaweza kukataliwa unapoenda kutafuta tenda,unaweza kukataliwa unapoenda kutafuta mkopo,inawezekana umekataliwa na wazazi wako n.k.Kiufupi ni kuwa ili uweze kufanikiwa katika malengo yako ni lazime ujiandae kukataliwa na ujue utafanya nini baada ya kukataliwa.
Kila unayemuona amefanikiwa kwa kiwango cha juu ujue kuna siku aliwahi kukataliwa,kila ambaye unatamani kuwa kama yeye ujue kuna siku aliwahi kukataliwa.Hii inamaanisha kuwa na wewe utapitia katika hali ya kukataliwa si kwa sababu haupendwi ila kwa sababu ni hatua muhimu katika kutimiza ndoto yako.

Inawezekana umeshawahi kukataliwa katika eneo fulani,swali kubwa ni je ulifanya nini?Kinachofanya watu wafeli kwenye maisha si kwa sababu wamekataliwa bali namna ambavyo wanakabiliana na hali ya kukataliwa kwao.Nakumbuka maneno ya Rais wa Zambia marehemu Michael Satta ambaye baada ya kugombea takribani mara tatu na kukosa alipoulizwa na waandishi wa habari kuwa kwa nini bado anaendelea kugombea na wazambia wameshamkataa?akasema,”wamenikataa kwa sababu hawajanielewa hivyo nagombea tena ili niwaeleweshe vizuri”.Na kweli,baada ya kugombea kwa mara nyigine alishinda uchaguzi na kuwa Rais wa Zambia.

Watu wengi wamefeli baada ya kukataliwa kwa sababu walifanya mambo yasiyo sahihi baada ya kukataliwa kwao.Kuna makosa matatu ambayo watu huyafanya wanapokutana na hali ya kukataliwa:

Moja ni kuwa hutafsiri kukataliwa kwao kama ni ujumbe kuwa wao hawafai.Watu wengi wanapokataliwa hutafsiri kuwa hiyo humaanisha kuwa wao si kitu na hawawezi lolote na hawana thamani.Hii ndio maana kuna watu wengine baada ya kukataliwa na wapenzi wao wakaamua kujinyonga,ama baada ya kufukuzwa kazi wameishia kuugua tu.Usikubali kukataliwa kwako ukutafsiri kumaanisha kuwa wewe si kitu ama hauna thamani kabisa.

Thamani yako haiko katika yule anayekukataa bali iko kwako wewe unavyojiona.Hivi kama ukichukua dhahabu na ukamtumia mbwa itakuwaje?si ataichezea tena anaweza kuweka kwenye kinyesi chake?Hii inamaanisha thamani ya dhahabu imepotea?La hasha,bado thamani ya dhahabu iko palepale.Ndivyo ilivyo,kila anayekukataa kiufupi ni kuwa hajagundua thamani uliyonayo.Hivyo kila uanpokataliwa jiambie-“Huyu amenikataa kwa sababu hajui thamani yangu”.

Hii ndio maana kuna watu walishawahi kukataliwa lakini baadaye watu walewale waliowakataa wakawataka tena .Hii ndio maana baada ya timu ya Manchester United kumuuza Paul Pogba kwa paundi milioni 1 mwaka 2012 kwa kumuona kuwa hana viwango,mchezaji huyo huyo amenunuliwa tena na timu ileile kwa paundi milioni 100 baada ya miaka 4.Hivyo basi usitafsiri kukataliwa kwako kuwa wewe haufai na hauna thamani,ni kuwa bado hawajaijua thamani yako.

Sababu ya pili inayowafanya watu wafeli mara baada ya kukataliwa ni kumchukia aliyewakataa.Ni kawaida kwa mwanadamu kuona kila anayemkataa kuwa ni adui yake.Kama unataka kufanikiwa jifunze kutomchukia mtu aliyekukataa hata kama imekuumiza kiasi gani.Kila wakati unapohamishia uchungu na hasira kwa aliyekukataa,unaendelea kupunguza nguvu zako za kufanikiwa.

Watu wengi wameshidnwa kupiga hatua kwa sababu ya kuwachukia wale ambao waliwakataa kwa namna moja ama nyingine.Unapomchukia aliyekukataa unampa mamlaka ya kuendesha maisha yako bila kujua na unauambia ubongo wako kuwa huwezi kufanikiwa hadi akukubali,kitu ambacho sio kweli.Kuna watu wameshindwa kupiga hatua kwa miaka mingi sana katika maisha yao kwa sababu tu kuna mtu aliwakataa huko nyuma na hadi leo wamebakia na uchungu wa kukataliwa.Hebu jiulize-je,kuna mtu ambaye bado umemuweka moyoni kwa sababu alikukataa huko nyuma?Kama jibu ni ndio basi chukua uamuzi wa kumsamehe na uanze hatua mpya.Naamini ukianza kufanya hivyo basi utafungua milango ya mafanikio kwenye maisha yako.

Kosa la tatu ambalo watu huwa wanalifanya wanapokuwa wamekataliwa ni ile hali ya kuamini kuwa,baada ya kukataliwa kwao basi hakuna tumaini tena.Hii huwa inatokea pale ambapo unakataliwa na mtu ambaye uliweka matumaini makubwa sana,ama kwenye kazi ambayo ulikuwa na uhakika utaipata kwa asilimia mia moja.Utajua tu kama kukataliwa kumefikisha katika hatua hii pale ambapo hutaki kuchukua tena hatua moja zaidi kuelekea katika malengo yako.Utajua kama kukataliwa kwako kumekuathiri pale ambapo mtu huyo akitajwa machozi yanakutoka kwa ndani na unasikia maumivu makali sana,utajua kuwa kukataliwa kumekuathiri pale ambapo kila ukitaka kuchukua hatua unakumbuka huko nyuma basi unaamua kughairisha.

Hali hii imewakumba watu wengi sana na imewakwamisha kuchukua hatua katika maisha yao.Watu ambao hufanikiwa siku zote huwa wanajiuliza-Hivi kwa nini nimekataliwa?Nifanye nini ili nisikataliwe tena?Huwa wanasikia maumivu ila huyatumia maumivu yao kutengeneza usongo wa mafanikio katika hatua zinazofuata.

Nawe ungana na Michael Jordan leo,usikubali kukataliwa kwao kuwe ni chanzo cha kufeli kwako.Hata kama umesikia maumivu ya kukataliwa,amua kuwa utatumia hasira na maumivu ya kukataliwa kwako kama hamasa ya kufanya bora zaidi.Kuna wengi waliokukataa watarudi na kukubali siku moja.

Endelea kutembelea www.JoelNanauka.com kujifunza zaidi.
See You At The Top
©JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website