Navigate / search

Mambo 3 Ya Kuyazingatia Ili Ufanikiwe Kazini Kwako

Ili kufanikiwa katika kazi unayoifanya unahitaji zaidi ya ujuzi wa kawaida wa kufanya kazi.Wako watu wengi sana ambao wameshindwa kuzingatia mambo muhimu yanayoonekana kuwa ni madogo lakini ambayo yanaweza kukufanya ufanikiwe ama ufeli kwenye kazi ambayo unaifanya.Leo nataka uyatambue mambo 3 muhimu ambayo kila mahala unapokuwa unaanza kufanya kazi ni lazima uyazingatie kama unatakiwa kufanikiwa katika kazi hiyo.
Jambo la kwanza kabisa ni kujifunza utamadami wa kampuni au shirika jipya ambalo unaanza kulifanyia kazi.Kila taasisi huwa ina utamadami wake ambao kwa kawaida huwa unatofautiana na wengine.Hii inamaanisha kama haujui utamaduni wa mahali husika unaweza kujikuta unafanya kitu fulani ambacho wewe unadhani kuwa ni sawa kumbe kulingana na utamaduni wa mahali husika kinakuwa sio swa kabisa.
Mkurugenzi wa Creative Group,Dona Farugia anasema aliwahi kufanya utafiti wa makampuni 250 na waliwahoji wakurugenzi wako kutaka kujua maoni yao juu ya changamoto ambayo wanafikiri waajiriwa wapya huwa wanakutana nayo.Katika utafiti huo waligundua kuwa,wakurugenzi 4 kati ya kila 10 walitaja kuwa wafanyakazi wengi wapya huwa wanashindwa kwa sababu ya kutojifunza utamaduni wa kampuni(Organization Culture).Na kutokana na hili kila ambaye anaanza kazi ofisi mpya huwa anashauriwa kuwa mchunguzi kwa kuwahi mapema asubuhi,kuchelewa kidogo kuondoka,kujifunza wanapumzika wakati gani kunywa chai,siku yao wanamalizaje,watu wa jinsia yako wanapendelea mavazi gani zaidi n.k
Kiufupi ni kuwa itatakiwa uwe mchunguzi kwa kila kitu ili uwahi haraka kuendana nao na usiendelee kuonekana mgeni ama kufanya mambo ambayo yataonekana ni ya “ajabu”.Wafanyakazi ambao huwa wako haraka kuendana na utamaduni wa kampuni yao mpya huwa wana nafasi kubwa zaidi ya kufanya vizuri katika kazi yao mpya.
Jambo la pili ni kuhakikisha kuwa unaweka sawa kila kinachotarajiwa kutoka kwako(Clarifying expectations).Mafanikio yako yatapimwa kuwa kuangalia mambo ambayo bosi wako anayaona kuwa ndiyo mambo ya msingi unayotakiwa kuyakamilisha.Moja ya sababu kubwa ya watu wengi kuonekana hawafanyi vizuri katika kazi zao ni kwa sababu huwa hawaweki bidii katika kujua haswaa wanatarajiwa kukamilisha majukumu gani na kutoa matokeo gani.
Peter Drucker mtaalamu wa management aliwahi kusema,”Hakuna kitu kisicho cha maana kama kufanya kitu fulani kwa ubora wa hali ya juu wakati hakikutakiwa kufanywa kabisa”.Hautaonekana kuwa ni mfanyakazi hodari sana kwa kufanya kazi kwa bidii na ubora tu,bali utapata fursa kubwa zaidi kwa kuonekana kuwa unatekeleza majukumu yako bila kufeli hata kidogo.Ili kujihakikishia kuwa mambo ambayo unatumia muda wako ni ya thamani sana kwa mwajiri wako-Fanya siku moja kuandika mambo yote ambayo unatarajiwa kuyakamilisha kisha yapeleke kwa mwajiri wako na muombe akupe maoni yake kuhusu vipaumbele vyako hivyo.
Hii itakusaidia kujua kama unatumia muda katika mambo yasiyo ya muhimu ama la,lakini pia itakusaidia kutokuja kulaumiwa kwa kufanya jambo ambalo baadaye linawezekana likaonekana halina umuhimu.
Jambo la tatu ni lile ambalo liliwahi kusemwa na Sue Edwards mkurugenzi wa kampuni ya Development by Design.Edward alisema sababu mojawapo ni watu wengi wanapokuwa kazini kujiona wao ni bora kuliko mtu mwingine yeyote Yule.Hii inasababisha matatizo makubwa mawili.Moja ni kuwa huwa wanataka mawazo yao tu ndio yakubalike,huwa hawako tayari kuwasikiliza wengine.Lakini pili watu wa namna hii hata wakikosea huwa hawako tayari kabisa kuomba msamaha kwa makosa ambayo wamefanya.Ukiwa na tabia hizi mbili basi kila siku wewe utakuwa mtu ambaye haupendwi na wafanyakazi wenzako lakini pia na bosi wako,na hivyo itakufanya uchelewe sana kufanikiwa katika kile unachokifanya.
Kama unataka kufanikiwa katika kazi unayofanya na ofisi uliyopo,basi kuanzia leo zingatia mambo haya matatu muhimu ili ufanikiwe.
See You At The Top
@JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website