Navigate / search

MAJARIBU MATATU YA KUYASHINDA ILI MALENGO YAKO YAFANIKIWE

nanauka-20

Kila lengo ulilonalo maishani mwako lazima litapitia wakati wa changamoto na kujaribiwa ambao utakusababishia uanze kuona kama vile kile ambacho unakiamini ama unataka kukifanya hakitaweza kufanikiwa tena.Kila mtu ambaye unamuona amefanikiwa sana katika maisha yake na pengine unatamani kuwa kama wewe,ukijaribu kuzungumza naye atakuambia mambo ambayo ameyapitia na kuyashinda katika maisha yake kabla hajafikia hapo alipo leo.Kwa maneno mengine kama kweli unatamani kuwa kama mtu fulani,ni muhimu sana pia kutafuta kujua changamoto ambazo wamezipitia na kujua namna walivyozitatua.
Kwa lugha nyepesi ningesema namna nzuri ya kutamani kufanikiwa kama wengine ni kuanza na kutamani kujua changamoto walizozipitia na namna walizvyozitatua.

Pia unatakiwa kukumbuka,mara nyingi watu huwa hawapendi kuonyesha wakati wanapopitia changamoto ila wanapenda kuonyesha mafanikio hadharani.Na kwa sababu hii,watu wengi sana wamejikuta kuwa hawajui kabisa changamoto ambazo wengine wamezipitia na kudhani kuwa yale ambayo wengine wamefanikiwa ni mambo yaliyopatikana bila kuwa na changamoto zozote.

Katika kufuatilia safari za mafanikio za watu wengi,nimegundua kuwa kuna majaribu matatu ambayo lazima yataijaribu ndoto yako.Na kila ambaye leo unamuona amefanikiwa ni lazima atakuwa amewahi kupitia katika hali hizi na akafanikiwa kuzishinda pia.

La kwanza ni jaribu la muda(Test of Time):Hii inamaanisha kuwa ndoto yako inaweza isitokee kwa kasi ya haraka kama vile ambavyo ulikuwa umepanga na umefikiria.Watu wengi wanapoanza kufanyia kazi wazo fulani huwa wanakuwa na matumaini ya kufanikiwa kwa haraka sana kwa sababu kuna watu walisikia walifanya na wakafanikiwa,kitu ambacho watu wengi waliofikia hatua za juu huwa hawaweki wazi kwa urahisi ni ile miaka waliyowekeza na nguvu walizotumia kwa muda mrefu.Kuna watu ambao nimeshakutana nao ambao walianza biashara kwa matumaini makubwa lakini baada ya muda wanagundua kuwa kile walichokuwa wanakitarajia hakiji haraka kama walivyokuwa wanafikiria.

Changamoto ya muda inamaanisha unatakiwa uwe tayari kusubiri hadi pale kitu unachotaka kitakapotokea.Kuna mambo kwenye maisha ni kama ujauzito,bila kujali unaharaka kiasi gani ya kupata mtoto ni lazima usubiri kwa miezi tisa kabla haujampata.Ili ufanikiwe ni lazima ufanye maamuzi thabiti kuwa bila kujali unachokitaka kinachukua muda mrefu kiasi gani,bado utaendelea kukifuatilia na kukifanya kwa bidii kwa sababu ni jambo linalogusa moyo wako sana.Uwezo wako wa katika kufuatilia jambo ambalo unaliamini sana katika maisha yako bila kukata tamaa pale linapochukua muda mrefu zaidi na ulivyotarajia ni sifa mojawapo muhimu sana ya watu ambao wanafanikiwa.

Hebu jaribu kufikiria mtu kama Nelson Mandela ambaye alikuwa tayari kusubiria ndoto yake kwa miaka 27 na baada ya hapo ikaja kutokea.Usiwe mwepesi wa kukata tamaa,pale ambapo jambo limechelewa kidogo kuliko ulivyotarajia.Kumbuka kuwa katika maisha kuna mambo yatachukua muda mfupi na kuna mambo mengine yatachukua muda mrefu sana hadi yamekamilika.

La pili ni Jaribu la kuachwa peke yako(Isolation):Huu ni ule wakati ambao ghafla unajikuta umebaki peke yako na wale wote ambao ulikuwa unawahesabu kuwa ni watu wako wa karibu zaidi hakuna mahali pa kuwaona kabisa.Yoyote aliyewahi kufikia kiwango cha juu cha mafanikio lazima atakusimulia wakati ambao alikuwa hakuna mtu wa karibu wa kumsaidia kumvusha.Huu ndio ule wakati ambao unampigia rafiki yako wa karibu simu na hapokei,unamtafuta kwenye watsapp na unaona “tiki mbili” kabisa ikiionyesha kuwa amesoma lakini hakujibu kabisa.Huu ndio ule wakati ambao kuna watu ambao uliwasaidia na unategemea wangekuwa msada kwako lakini cha kushangaza hawakusaidii kabisa.

Ili ufikie kilele cha mafanikio yako lazima utambue kuwa,wakati huu utafika na ni lazima uwe tayari kuukabili.Kuna watu utakuta wakati fulani ulikuwa na marafiki wengi sana lakini ghafla mambo yalipoenda kombo umebakia peke yako.Hiki ndicho kipindi unajikuta unajifungia ndani peke yako,umekuwa mpweke na unaanza kama kuona dunia haikutaki kabisa.Ili ufikie kilele cha ndoto yako ni lazima ujifunze kuukabili wakati huu na kuushinda kabisa.Kama leo uko kwenye kipindi hiki basi kumbuka kuwa ni sehemu muhimu ya kuipitia kabla haujafanikiwa katika maisha yako.

La tatu ni kuishiwa nguvu za kuendelea(Moment of Fatigue):Kuna wakati unaweza kujikuta ile hamasa yote ambayo ulikuwa nayo mwanzoni  katika kufuatilia ndoto yako imepotea ghafla.Unajikuta hupendi tena hata kuongelea kile ambacho ulikuwa unakifanya mbele ya wengine.Kati ya siku unapoanza kuamini na kufuatilia malengo yako hadi siku utakayofanikiwa,utakutana  na kipindi ambacho nguvu zitakuwa zimekuishia na utakuwa hautamani kabisa kuendelea mbele.

Hapa nazungumzia kile kipindi ambacho ukiamka asubuhi wazo linakujia la kukuambia ni bora uachane na hiki kitu.Huu ndio ule wakati kila mtu anakuambia,usiendelee kupoteza muda tafuta kitu kingine ufanye.Katika kitabu changu kipya cha TIMIZA MALENGO YAKO,nimeeleza namna watu waliofanikiwa jinsi walivyoweza kupitia hali kama hii na wakafanikiwa katika sura inayoeleza sifa na tabia za watu wanaofanikiwa.

Ni lazima siku zote ukumbuke kuwa mafanikio yako sio matokeo ya msukumo wa mambo yanayotokea nje yako bali ni yale mambo yanayotokea ndani yako.Nguvu ya kuendelea mbele lazima ianzie ndani yako.Kuna wakati hautajisikia kabisa kuendelea kusogea hatua moja,lakini kama kweli unataka kufanikiwa ni lazima ujifunze kufanya si kwa sababu unajisikia kufanya bali kwa sababu unajua umuhimu wake.

Nakumbuka siku moja nilisoma habari ya mfanyabiashara mmoja wa marekani Thom Packets,ambaye alikuwa amefanikiwa sana.Hata hivyo siku moja kuna mtu alikutwa amekufa ofisini kwake na hii ilimuingiza matatizoni hadi akafilisika.Siku moja akiwa amekunywa vidonge 35 ili ajiue akaota ndoto na sauti ikamwambia-“Bado kuna matumaini,usikate tamaa”.Alipoamka na kujikuta yuko hai bado,akaamua kutokata tamaa tena katika maisha yake.Na alianza kuishi kwa kuifuatilia ndoto yake na mwishowe aliweza kufanikiwa tena.

Bila kujali kwa leo unapitia jaribu gani kati ya haya matatu,kitu kikubwa cha kukumbuka ni kuwa ili kufanikiwa ni lazima uyashinde na uvuke upande wa pili.Ili kupata kitabu chako cha TIMIZA MALENGO YAKO(Mbinu 60 walizotumia watu maarufu kufanikiwa) popote pale ulipo kwa 15,000/- Tu,unaweza kuwasiliana kupitia:0767375474/0655720197.

See You At The Top
www.Mentorship.co.tz
©JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website