Navigate / search

Mafanikio Huanza Kuja Baada Ya Kufanya Mambo Haya 3

index

Maisha yako yanategemea sana maamuzi unayoamua kuyafanya kila siku na hatua ambazo huwa unaamua kuzichukua ili kubadilisha mwelekeo.Kati ya vitu unatakiwa kuvijua ni kuwa maisha yako hayataweza kubadilika kama hakuna hatua yoyote ambayo utaamua kuichukua katika kubadilisha hali yako ya sasa.Usikubali kuwa katika mkumbo wa watu wanaofeli ambao wao huwa na dalili zifuatazo:

Moja huwa ni watu ambao wanaamini kuna siku mambo yatabadilika tu na yatakuwa mazuri.Huwa hawachukui hatua zozote zile katika kubadilisha maisha yao.Huamini kuwa kama wameumbwa kufanikiwa basi siku itafika na watafanikiwa tu(huwa wanasema kama ipo ipo tu).Wanasahau kuwa mafanikio sio bahati,ni matokeo yanayopangwa.

Dalili ya pili watu wa namna hii hujiaminisha kuwa kila aliyefanikiwa basi ni lazima ameiba,anatumia nguvu za giza(kama vile freemason) ama alipata bahati ya kuwa na wazazi matajiri.Wanasahau kuwa Dangote na Bill Gates wote wamepata utajiri wao sio kwa kurithi ila kwa kutumia akili na vipaji vyao.

Dalili ya tatu huwa ni watu wanaojua mambo mengi ila huwa hawayafanyii kazi.Mfano rahisi itakuwa leo utakaposoma newsletter hii hadi mwisho.Jiangalie kama utafanyia kazi ama la.Ukigundua kuwa haujafanyia kazi basi jua kabisa unajiunga na wale ambao mafanikio yao yatachelewa sana katika maisha yao.

Leo ningependa kukumbusha kuwa unatakiwa uwe na nidhamu kubwa sana katika kuifuatilia na kuitekekea ndoto yako.Kuwa na nidhamu maana yake ni kuwa tayari kufanya yale mambo ambayo yana umuhimu kwako kuyafanya bila kujali kama unajisikia kuyafanya ama ala.Ili kufanikiwa unatakiwa kuwa na nidhamu ya kuyajenga mafanikio yako.leo ningependa uzijue hatua 3 zifuatazo zitakazokusaidia kufanikiwa katika maisha yako:

Amua Unataka Nini kwenye Maisha.

Hakuna kitu cha hatari kwenye maisha kama kuwa bize bila kujua unaelekea wapi.Kuna watu wengi sana wanafanya mambo mengi mazuri na kwa nje wanaonekana wamefanikiwa sana ila hawana mwelekeo.Hawawezi kusema kuwa kesho wanataka kuwa wapi na wawe wanafanya nini.

Leo ningependa utulie kidogo kabla haujaendelea kusoma na ujiulize maswali yafuatayo:
Hivi mimi nataka kuwa nani?Natafuta nini kwenye maisha?Baada ya miaka 10 nataka kuwa wapi na ninafanya nini?.Tumia muda kidogo kuandika majibu ya maswali haya na yatakusaidia kujua kama unao mwelekeo ama hauna.Utashangaa kugundua kuwa ingawa ni jambo muhimu ila pengine ulikuwa haujawahi kujiuliza kabisa katika maisha yako.
Ukishapata majibu ya maswali haya,andika kwa ufasaha mwelekeo wa mahali na vile utakavyokuwa baada ya miaka kumi kuanzia leo.Tafuta sehemu ambayo unaweza kuweka na ukawa unaiona kila siku(pengine kwenye ukuta wa chumba chako,ofisini kwako n.k)

Weka Muda wa kutimiza Kila lengo Yako

Baada ya kupata mwelekeo wa maisha yako,unatakaiwa sasa kuweka malengo makubwa kuhusu maisha yako na uyawekee muda wa kuyatimiza.Usikubali kuwa mtu mwenye malengo yasiyo na muda.Kila wakati unapoweka muda katika malengo yako unakuwa unaulazimisha ubongo wako kufanya kazi kwa bidii.Pengine unayo malengo lakini je yana muda?Sababu mojawapo ya watu kughairisha mambo mara kwa mara ni kwa sababu huwa hawana muda waliojiwekea kutimiza malengo yao.

Tumia muda kidogo-Andika malengo yako makubwa ya mwaka huu na katika kila lengo andika muda gani/lini utakuwa umelitimiza.Baada ya kuwa umefanya hivyo,tafuta mtu unayeweza kumshirikisha malengo yako na muda uliojiwekea ili aweze kukufuatilia na hii itakuongezea hamasa katika kutimiza malengo yako.Je,umeshaandika malengo yako yote na muda?

Kila siku fanya jambo kuchangia malengo yako

Kati ya kitu kinawafelisha sana ni ile hali ya kutaka kusubiri hadi siku moja itakayoweza kubadilisha maisha yao.Unachotakiwa kujua ni kuwa kila siku ni muhimu sana katika maisha yako na inatakiwa kuchangia katika kusudi kubwa ulilonalo maishani mwako.

Swali la kujiuliza-Hivi tangu siku ya leo imeanza nimefanya jambo gani linalochangia katika kusudi kubwa nililonalo maishani mwangu?Usikubali siku yoyote ile ipite bila kufanya jambo litakalokusogeza hatua moja mbele katika mafanikio yako.

Kila siku unapopanga mambo yako na ratiba ya kufanya vitu vyako-Jiulize-Katika mambo haya ninayopanga kuyafanya leo,ni mambo mangapi yanachangia katika malengo yangu makubwa ya mwaka huu?Kadiri unavyoacha kufanya mambo ambayo yana mchango mkubwa sana katika malengo yako makubwa ndivyo kadiri utakavyochelewa kufanikiwa katika malengo yako.

Hitimisho

Ili kufanikiwa ni lazima uwe mtu ambaye kila wakati ni mtu wa vitendo zaidi.Siku ya leo kabla haijaisha pata muda wa kuandika kwa ufasaha mwelekeo wa maisha yako katika kiwango ambacho hata ukiamshwa usingizini unaweza kusema bila kubabaika.Kama hautajali unaweza kushare nami malengo yako kupitia joel@joelnanauka.com na nitaweza kukusaidia kuona namna yanavyoweza kuwekwa katika mfumo ulio bora zaidi.
Huko nyuma katika mafunzo ya kila mwezi ya “Mentorship Program” tuliwahi kufundisha namna ya kuweka malengo ya maisha ya muda mfupi chini ya mwaka mmoja,ya kati chini ya miaka 5 na ya muda mrefu na tulipa nafasi kwa kila mshiriki kutengeneza “life mission statement” na kuwa na malengo ya muda mrefu ya miaka 30.

Kwa mwezi wa sita program yetu itafanyika tarehe 25 katika ukumbi wa GEPF Victoria makumbusho Dar es Salaam Kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 7 Mchana (hakuna kiingilio) na tutakuwa tukijifunza kuhusu namna ya kubadilisha kipaji na uwezo wako kuwa pesa.Kwa mlio mikoani program kwa ajili yenu zinaandaliwa.

Kama bado haujalike page yangu ya facebook(Joel Nanauka) tafadhali tembelea leo na ufanye hivyo ili upate mafunzo ya kila siku.
Kumbuka pia unaweza kupata mafundisho mbalimbali kwa njia ya CD na Vitabu kuhusu namna ya kulijua kusudi lako la kuja duniani,namna ya kufaulu mitihani yako kwa kiwango cha juu,namna ya kutoa hotuba nzuri mbele za watu n.k

Tabia ya mafanikio ni pamoja na kuweza kushirikisha wengine mambo mazuri unayojifunza.Tafadhali,watumie newletter hii watu ambao unaona inaweza kuwasaidia.

Kumbuka ndoto Yako Inawezekana.

See You At The Top.

Comments

Emmanuel
Reply

Daah
Asante sana Kaka!
Natamani kila mtu asome hii mind food!!

Doria Daniel
Reply

Very touched

Leave a comment

name*

email* (not published)

website