Navigate / search

Maambo 3 Muhimu ya Kuyafanya Jumatatu Ili Kuwa Na Wiki Ya Ushindi

Siku ya kwanza ya wiki ni muhimu sana kuhakikisha kuwa unakuwa na wiki ya mafanikio bila kupoteza muda wala kujikuta unafanya mambo ambayo siyo ya muhimu katika maisha yako.Kila aliyefanikiwa kufikia kiwango cha juu sana katika maisha yake basi huwa anatumia jumatatu kwa namna ya tofauti sana na watu wengine wa kawaida.

Kuna mambo ya msingi matatu ambayo unatakiwa kuyazingatia katika kujiandaa na jumatatu yako ili kujihakikishia wiki ya mafanikio na kuhakikiksha unatimiza kila lengo ulilonalo kwa wiki hii.

Jambo la kwanza ni kuhakikisha kuwa umeiweka ramani ya wiki yako nzima  kuanzia jumatatu hadi jumapili ya wiki hii inayoanza.Siku moja wakati nasoma sifa za watu wanaofanikiwa sana katika maisha yao na kutimiza malengo waliyonayo nilikutana na namna 7 ambazo huwa wanazitumia katika kufikiri.Njia mojawapo ambayo wote walikuwa nayo katika maisha yao ni ile tunaiita “Long-Term Perspective”: Yaani ile hali ya kuona mambo kwa upana wake na kuiishi kila dakika kwa kuilinganisha na jinsi ambavyo yanachangia malengo makubwa uliyonayo.

Mafanikio yako yamefichwa katika namna ambavyo unatumia kila siku yako.Kadiri unavyotumia siku yako vibaya basi pia utajikuta na malengo yako yanachelewa kufanikiwa,.Hivyo wiki hii amua kuwa wa tofauti na anza kujiandaa mapema kwa kuangalia katika kila siku ya wiki utakuwa na jambo gani kubwa sana ambalo utalifanya linalochangia katika malengo yako makubwa.Usikubali kuanza tu wiki bila kuandika.Chukua muda sasa andika kuanzia jumatatu hadi jumapili.

Jambo la pili ni kujitengenezea hali ya kuwa mshindi.Unachotakiwa kujua ni kuwa kushinda ni tabia kama ilivyo kushindwa na kila mshindi huwa kuna tabia amezitengeneza za kumsaidia kuwa mshindi katika mambo fulani.Sasa njia mojawapo ambayo nataka nikufundishe leo ya kukusaidia kuwa mshindi ni namna unavyoweza kutengeneza hali ya kujihisi kuwa mshindi  kwa kufanya mambo ambayo washindi wanafanya.

Ili kufanikisha hili kuna kanuni inaitwa “The Law of Reversibility”-Hii inasema kuwa kadiri unavyoshinda katika jambo fulani basi tabia yako na matendo yako huwa yanabadilika na hivyo kuna aina ya matendo na tabia ukiwa nazo zitakusaidia pia kuwa na hali ya ushindi katika kile unachokifanya.Kama haujanielewa naomba uisome tena,ni muhimu sana uweze kuielewa hii.Sasa ili kufaidika na kanuni hii,watu ambao wanashinda katika maisha huwa wanaanza siku yao kwa kufanya jambo zito na la muhimu ambalo huwapa hisia(feelings) za kuwa washindi katika maisha.Hali hii huwafanya wawe watu ambao hutaka kushinda zaidi na hivyo hujikuta wanafanya mambo makubwa na muhimu zaidi ili waendelee kujisikia kuwa ni washindi na mwisho wa siku huwa wanajikuta wamefanya mambo mengi sana na kupata matokeo makubwa zaidi katika maisha yao.

Jambo la tatu ambalo ukilikosa unaweza kujikuta umepoteza mwelekeo wa siku yako ni kuamua kutonyang’anywa furaha yako na kitu chochote.Unachotakiwa kujua ni kuwa kuna uhusiano mkubwa sana kati ya furaha yako  na nguvu za kufanya yale uliyokusudia.Watu ambao huwa  wananyang’anywa furaha zao kirahisi basi huwa wanajikuta wanakuwa na wiki mbaya sana katika maisha yao.Umeshawahi kuanza siku na uko njiani kuelekea ofisini unakutana na trafiki na anakuambia kosa fulani na unaanza kubishana?Umeshawahi kukumbuka hiyo siku iliishaje?Umeshawahi kuamka asubuhi halafu unaanza kugombana na mwenzi wako,unakumbuka hiyo siku iliendaje?Umeshawahi kuanza siku halafu umeingia kwenye daladala ukajikuta unaanza kurushiana maneno na kondakta ama abiria mwenzako?Hiyo siku iliishaje?

Kanuni ya kuwa na nguvu na uhakika wa kumaliza wiki yako ukiwa mshindi ni kuhakikisha kuwa uailinda furaha yako.Ukweli ni kuwa kuna watu wengi sana watakuwa wanajitahidi kukunyang’anya furaha yako wiki hii akiwemo bosi wako,mfanyakazi mwenzako,na hata rafiki yako.Jipange na ukusudie kuwa utaitunza furaha yako na hakuna mtu atakayekung’anya.

Ukianza kufanya mambo haya matatu kwa wiki hii sina shaka kuwa utaanza wiki yako kwa ushindi mkubwa na utapata matokeo makubwa kuliko kawaida.Unaweza kushare ujumbe huu kwa kutumia butto za hapo chini ili wengine wausome zaidi na kujifunza.

See You At The Top

@JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website