Navigate / search

Kumbukumbu ya miaka 60 ya safari ya Nyerere UN

JFKWHP-AR6696-B

BARAZA la Wazee wa TANU chini ya Mwenyekiti wake Sheikh Suleiman Takadir lilichukua mafanikio ya safari ya Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa (UN) kuwa jukumu lao binafsi. Sehemu ya kwanza ya maandalizi ilitakiwa ifanyike kwa siri sana. Uongozi wa TANU ulimkabidhi Idd Faiz kazi ya kuandaa, kukusanya na kusimamia mfuko wa safari ya Rais wa TANU kwenda Umoja wa Mataifa, New York. Safari ilikuwa ifanyike mwezi wa Februari, 1955.

Mwaka wa 1953, Faiz alikuwa na umri wa miaka arobaini na tatu, mwenye ari na nguvu tele. Alipokuwa katika Kamati Kuu ya ya TANU mwaka wa 1959, aliteuliwa kuwa Mweka Hazina wa Taifa wa TANU pamoja na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu. Alikuwa mmoja wa viongozi wa chama walioanzisha TANU Press iliyokuwa katika njia panda ya Mtaa wa Mchikichi na Livingstone mjini Dar es Salaam.

TANU Press ndiyo ilikuwa ikichapisha na kusambaza jarida la TANU, Sauti ya TANU lililohaririwa na Rais wa TANU , Julius Nyerere, na baadaye kuchapisha jarida la Mwafrika chini ya uhariri wa Rashid Heri Baghdellah na Robert Makange. Kampuni hiyo ya kupiga chapa ilimilikiwa na Mwananchi Development Corporation. TANU ilimteua Abdul Faraj kuiongoza kampuni hiyo.

TANU ilihitaji takriban shilingi elfu kumi na mbili kumwezesha Nyerere kusafiri kwenda Umoja wa Mataifa. Kamati ya Abdu Kandoro, Japhet Kirilo na Abbas Sykes ilikuwa imekusanya kiasi cha fedha kutoka majimboni ambacho kilitumika katika ile safari ya Ally Sykes na Phombeah kwenda kwenye Pan African Congress mjini Lusaka. Kilichosalia hakikutosha kumpeleka Nyerere Maekani.

Ilibidi fedha za ziada zitafutwe kutoka kwa wananchi ili kumwezesha Nyerere kufanya safari hiyo. John Rupia alichangia zaidi ya theluthi moja ya fedha zilizotakikana. Wanachama wengine walichangia kwa uwezo wao wote lakini TANU katika siku zile ikiwa bado changa ilikuwa maskini, kiasi hicho kilikuwa bado kiko nje ya uwezo wake.
Ikitambua ule upungufu wa fedha za safari ya Nyerere, Idd Faiz aliombwa na uongozi wa Al Jamiatul Islamiyya kutoa fedha katika mfuko wa Al Jamiatul Islamiyya na kuzitia katika hazina ya TANU kukiwezesha chama kumpeleka Nyerere, New York. Hata pamoja na fedha zile kutoka Al Jamiatul Islamiyya, bado hazikuweza kukidhi haja.
Al Jamiatul Islamiyya haikuwa na jingine isipokuwa kumuomba Idd Faiz asafiri kwenda Tanga na kupata fedha zaidi kutoka huko. Mwalimu Kihere alikuwa tayari amekusanya fedha hizo na alikuwa anasubiri tu zije zichukuliwe na kupelekwa makao makuu.

TANU ilipata habari kwamba yeyote ambaye angeenda Tanga kuchukua fedha hizo kwa ajili ya safari ya Nyerere angekamatwa. Kabla ya kuondoka, Oscar Kambona, Katibu Mkuu wa TANU, na John Rupia, Makamu wa Rais wa TANU, walikwenda kuonana na Idd Faiz nyumbani kwake Ilala kumuaga, kumtakia safari njema na kumpa maelezo kwa ufupi.

Safari ya kwenda Tanga haikuwa na tatizo lolote, lakini katika wakati wa kurudi basi ambalo Faiz alikuwamo lilisimamishwa njiani Turiani na makachero. Idd Faiz alikamatwa, akavuliwa nguo na kupekuliwa, lakini hakukutwa na fedha.

Hili lilimshangaza na kumchanganya yule afisa aliyemkamata kwa sababu walikuwa na taarifa Faiz alikuwa amechukua fedha kutoka kwa Mwalimu Kihere kule Tanga. Faiz aliwekwa chini ya ulinzi na kupelekwa Dar es Salaam kwa usaili zaidi wakati wote akiwa analindwa na askari wenye silaha.

Baadaye Idd Faiz aliachiliwa huru. Zile fedha za TANU zilifika makao makuu ya TANU Dar es Salaam, salama salimini. Kumbe, Faiz alikuwa amempa msichana mdogo aliyekuwa abiria ndani ya basi lile alimokuwamo kuzibeba.
Mnamo tarehe 17 Februari, 1955, Nyerere aliondoka kwenda New York kuhutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa. Nyerere aliiweka wazi nia ya TANU kuwa ametumwa na wananchi wa Tangayika kuwasilisha ujumbe ufuatao:

“Kuona kanuni ya uchaguzi ikianzishwa na Waafrika kujiwakilisha katika taasisi zote za umma… Hii tunaamini, ni kwa mujibu wa masharti ya Makubaliano ya Udhamini na Ibara ya 76 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.”
Mbele ya Umoja wa Mataifa, TANU haikuwa ikidhihirisha tamko lolote jipya, yale yote yaliyowasilishwa pale yalikuwa ni maoni ya kamati ndogo ya siasa ya TAA yaliyowakilishwa kwa Constitutional Development Committee ya Gavana Edward Twining mwaka wa 1950.

Gavana Twining aliyapuuza mapendekezo ya TAA na badala yake aliendelea na mipango yake ya kuwa na wawakilishi wa rangi zote katika Baraza la Kutunga Sheria. Ili kuupa msukumo msimamo wake huo serikali ilituma ujumbe wake Umoja wa Mataifa kuipinga TANU uliowakilishwa na I. C. Chopra, Mwasia; Sir Charles Phillips, Mzungu na Liwali Yustino Mponda, mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria wa Newala.

Nyerere alirudi kutoka New York, Jumamosi, tarehe 19 Machi, 1955 na alipokewa uwanja wa ndege na halaiki ya watu. Dossa Aziz anakumbuka kuwa aliruhusiwa pale uwanja wa ndege kuingiza gari yake hadi ndani ya uwanja chini ya ndege ili kumrahisishia Nyerere kuingia ndani ya gari na kuepuka msongamano wa watu.

Dossa Aziz anasema kama isingekuwa kwa msaada huo, Nyerere angesongwa sana na watu. Watu walikuwa kila mahali wakisukumana na kusongamana wakijaribu angalau kumtia Nyerere machoni. Watu walikuwa wakiimba na kucheza ëmgandaí, ngoma ya Kizaramo, wakiimba: ëBaba Kabwela Yunoí.

Jambo la kushangaza ni kwamba hakuna mtu aliyewahi kuusikia wimbo huu kabla ya siku ile na hakuna ajuaye lini ulitungwa. Ile gari ya Dossa Aziz aliyopanda Nyerere ilisukumwa kutoka uwanja wa ndege hadi nyumbani kwa Nyerere, Magomeni Majumba Sita, kiasi cha kama kilomita ishirini.

Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili. TANU ilifanya mkutano wa hadhara Mnazi Mmoja ambao ulihudhuriwa na umati ambao kamwe haukupata kuonekana Dar es Salaam. Inakisiwa zaidi ya watu 40,000 walikuja kutoka kila upande wa mji kumsikiliza Nyerere.

Hakuna mtu aliyekuwa na raha ya kuandika kuhusu mkutano ule na safari ya kihistoria ya Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa kuliko Mashado Plantan katika gazeti lake la Zuhra. Mtambo wa gazeti wa Mashado uliokuwa Mtaa wa Ndanda, Mission Quarters ulichapisha nakala za ziada za gazeti hilo na toleo lote liliuzika”.
(Makala hii imechukuliwa kutoka katika kitabu cha Maisha na Nyakati za Abdul Sykes kilichoandikwa na Mohamed Said)

Leave a comment

name*

email* (not published)

website