Navigate / search

Kanuni Za Kuepuka Umaskini.

Kati ya maeneo muhimu sana katika maisha yako ambayo unatakiwa kuyawekea uzito na kipaumbele katika safari yako ya kimafanikio,ni eneo la kifedha.Watu wengi wana nia na mipango mizuri ambayo imekwama na kushindwa kutekelezeka kwa sababu tu hawana pesa za kutosha kufanya wanachotaka.

Hata hivyo kwa upande mwingine kuna watu ambao kwa nje ukiwaangalia utaona wana kipato kikubwa,wana kazi nzuri,wana mshahara mzuri-Lakini ukweli ni kuwa hali yao ya kifedha ni ya kukimbizana kutoka mshahara hadi mshahara.Kwa maneno mengine,ikitokea bahati mbaya wakapoteza kazi yao wanayofanya kwa miezi mitatu tu,hawataweza kuishi kwa amani kwani hawana akiba wala vitega uchumi vya kuwapatia kipato cha ziada.

Mafanikio ya kifedha ni matokeo ya kufanya maamuzi thabiti lakini pia ni matokeo ya kuamua kuishi maisha ya nidhamu ya pesa ambayo watu wengi wameshindwa.Hivi umewahi kujiuliuza kwa nini hali yako ya kifedha,iko hivyo kwa sasa?Na je una mpango wowote wa kubadilisha hali yako ya sasa ama wewe ni aina ile ya watu ambao hutegemea bahati itatokea na kisha watafanikiwa?.Kuna watu ambao walishawahi kupata pesa nyingi sana lakini leo ni maskini,kuna wengine walishawahi kufanikiwa sana kibiashara lakini leo wamefilisika.Mafanikio ya kifedha yana kanuni ambazo ni lazima uzizingatie ili uweze kukua na kufanikiwa.Leo ningependa tuzingatie kanuni nne ambazo unatakiwa kuzizingatia katika kujenga uwezo wako wa kufanikiwa kifedha.

Kanuni ya kwanza ni kuwa na bajeti.Kanuni hii inalenga kukufanya ujiulize swali la msingi linalosema-Pesa yangu huwa inakwenda wapi?Watu wengi sana wanapata pesa ila hawawezi kabisa kueleza huwa zinatumika kwa matumizi gani.Hii ndio maana ukianza kutafakari pesa ambazo zimepita mkononi mwako tangu mwaka huu uanze na ukiangalia mambo uliyofanya utashangaa sana.Kama wewe ni mfanyakazi uliyeajiriwa hebu jiulize,tangu umeanza ajira jumla umepokea mshahara wa shilingi ngapi?Ukishapata jibu lake-Hebu angalia mambo uliyofanya hadi sasa kwa kulinganisha na pesa zilizopita mkononi mwako.

Mafanikio ya kifedha sio matokeo ya kiwango cha pesa unayopata bali ni matokeo ya kiwango cha pesa unachoweza kukibakiza mkononi mwako na jinsi utakavyoweza kukizalisha katika maisha yako.Kila mwezi hakikisha una bajeti ya matumizi yako ambayo unakusudi kuyatumia katika maeneo mbalimbali.Kwa kufanya hivyo utajijengea nidhamu ya kutotumia pesa kwa mambo ambayo sio ya muhimu.Uzuri ni kwamba hauhitaji kuwa mtaalamu ili kutengeneza bajeti,unachotakiwa kufanya ni kuorodhesha maihitaji yako na kuweka kiwango cha pesa unazotarajia kutumia.Kisha unaweka vipaumbele wa maeneo ambayo unaona ni muhimu zaidi kwanza kabla ya mengine katika kutumia pesa yako.

Ukianza kuwa makini na kufuatilia pesa zako zinaenda wapi,utagundua kuwa kuna pesa nyingi sana ambazo unazipoteza bila wewe mwenyewe kujua kwa kununua ama kutumia katika vitu visivyo vya ulazima.Kujiwekea bajeti ni pamoja na kuweka kiwango kidogo cha pesa ambacho utakuwa unakiweka kama akiba katika maisha yako kila wakati unapopata pesa.Watu wengi ukiwaambia waweke akiba huwa wanakimbilia kusema kuwa hawana kipato cha kutosha,lakini watu wanaofanikiwa kifedha huwa wanaanza kuweka akiba kwa kiwango kidogo kisha wanaendelea kuongeza kadiri kipato chao kinakuwa.Akiba hii ndio baadaye huitumia kuwekeza ama kununua vitu vitakavyowaingizia pesa zaidi katika maisha yao.

Leo,ningependa upate muda na kisha uandike kipato chako na matumizi yako ya mwezi kwa ufasaha.Hii itakupa picha kwa mwezi unatumia kiasi gani kufanyia kitu gani.Swali la muhimu hapa ni kuwa-Pesa yangu huwa inaenda wapi?Huwezi kufanikiwa kifedha kama haujui kabisa pesa yako huwa inaenda kutumika kwa mambo gani,

Kanuni ya pili ni ile ambayo ilitungwa na mwandishi nguli wa Uingereza,Bwana Cyril Northcote Parkinson ambayo ilipewa jina lake na kuitwa “Kanuni ya Parkinson”.Kanuni hii husema kuwa-Katika hali ya kawaida mwanadamu anapoona kipato chake kimeongezeka basi na yeye huongeza matumizi ili yafikie kumaliza ongezeko la kipato kipya alichokipata.Kwa sababu hiyo,hata kama mtu ataongezewa kipato mara kumi,utashangaa bado anaishi kwa shida kama vile kipato hakijaongezeka.Ili ufanikiwe kifedha ni lazima ufanye juhudi za makusudi kuikiuka kanuni hii.

Unatakiwa ufanye maamuzi katika maisha yako kuwa hautabadilisha kwa haraka aina ya maisha unayoyaishi ili ongezeko la kipato ulilolipata liwe na faida kwako.Watu wengi wakiongeza kipato/mshahara/Faida,basi haraka sana anabadilisha nguo anazovaa,anabadilisha gari,hata nyumba ghafla anaenda kuchukua ya bei ghali sana-ili mradi tu anataka kuwathibitishia watu kuwa kipato chake kimeongezeka.Kama kweli unataka kufanikiwa kifedha ni lazima uhakikishe kuwa mabadiliko ya maisha yako hayaendi kwa kasi zaidi ya kipato chako.Hii ni kusema kuwa kwa kila ongezeko ambalo unalipata kifedha hakikisha kuwa haubadilishi staili yako ya maisha itakayosababisha utumie chote kilichoongezeka-Badala yake tumia kile kinachoongezeka kuwekeza zaidi.

Watu ambao kanuni hii imewaathiri katika maisha yao ndio wale ambao kila wakati wanalazimika kuishi juu zaidi ya kipato chao.Ni rahisi sana kujua kama unaishi juu ya kipato chako kwa kuangalia aina ya madeni na mikopo uliyonayo.Kama wewe una madeni na mikopo ambayo yote imelenga kutatua shida za kila siku au kwa ajili ya fasheni basi ujue kuna tatizo katika mfumo wako wa matumizi.Hapa nazungumzia kama wewe huwa kila wakati unakopa kwa ajili ya kununua nguo,kulipa kodi ya nyumba,kununua simu ya kisasa,Viatu n.k basi ujue kuna tatizo katika mfumo wako wa kifedha na unahitaji kubalika haraka kabla umaskini wa kipato haujakuvamia.

Leo ningependa ufanye tathmini ya mikopo na madeni uliyonayo yametokana na mambo gani.Kama ukigundua madeni na mikopo yako mingi ni aina ya kuleta umaskini kama nilivyoeleza hapo juu basi mara moja amua kubadilisha mwelekeo.Kwanza amua kutojiingiza tena katika matumizi ya namna hii na pili weka mkakati kabambe wa kuanza kuyalipa bila kuchelewa.Ushauri wangu kwako ni kuwa siku zote,tumia mkopo kwa ajili ya shughuli ya kibisahara,uwekezaji ama kuzalisha zaidi na sio kununua vitu visivyozalisha.

Kitabu cha TIMIZA MALENGO YAKO kimeelezea mbinu 60 za kukusadia kufanikiwa kifedha ambazo watu waliofanikiwa wanazitumia kufikia kilele cha mafanikio yao.Unaweza kuwasiliana nasi kupitia namba 0655 720197 na tutakuelekeza kwa wakala wetu katika mkoa uliopo ama kama uko Dar Es Salaam na unahitaji kuletewa hadi pale ulipo uanweza kuwasiliana nasi kupitia 0712 224282

See You At The Top

Leave a comment

name*

email* (not published)

website