Navigate / search

Jinsi Ya Kutoka Kwenye Madeni

Mwezi Februari mwaka 2008 katika kipindi cha mtangazaji maarufu sana Oprah Winfrey alihojiwa mama mmoja ambaye alikuwa na watoto 4.Familia yake  ilizoea kuishi maisha ya hali ya juu sana.Walikuwa wanaishi katika jumba kubwa la kifahari,wana magari ya kifahari na walikuwa kila wakati wanaenda kufanya manunuzi ya vitu katika maduka makubwa sana nchini Marekani.Bila kujua kuwa pamoja na kumiliki biashara nzuri,mume wake alikuwa tayari amewaingiza katika maisha ya starehe na alikuwa ameacha kulipa madeni yao kwa wakati na tayari alikuwa anakabiliwa na madeni makubwa sana.Siku moja aliporudi nyumbani akashangaa kumkuta mume wake akiwa amejiua na ameacha karatasi aliyoandika kuwa amefanya maamuzi hayo kwa sababu anaona maisha yamembadilikia na amekuwa na madeni mengi sana ambayo hataweza kuyalipa kwani yalikuwa yamefikia dola 857,000.Mama huyu anasema hakuwahi kufikiria kuwa mume wake anapanga kujiua na yuko kwenye hali ngumu kiasi hiki.Habari hii inafanana sana na ya mwanamama Carlene Balderrama aliyejiua akiwa na miaka 53 muda mchache tu kabla ya nyumba yake kuuzwa baada ya kushindwa kulipa deni alilokuwa anadaiwa huko Marekani.

Watu wengi sana wamejikuta katika hali kama hii na imewasababishia matatizo makubwa ambayo wakati mwingine hufikiria kuwa hakuna  njia nyingine ya kuyatatua.Ningependa nianze kwa kukuambia kuwa hakuna tatizo lisilo na suluhisho na hata kama ukijikuta kwenye deni kubwa kiasi gani,ipo njia ya kutumia ili uweze kutoka kwenye tatizo hilo.Inawezekana leo umejikuta katika hali kama hii na unaona kama vile hakuna namna unaweza kutoka,ila utakaposoma makala hii hadi mwisho naamini utapata mwanga wa mahali pa kuanzia ili uweze kujikwamua.

Kwanza ningependa ujue kuwa athari kubwa ya kuwa na madeni yanayoonekana hayalipiki haitokani na kiwango cha pesa chenyewe bali athari kubwa hutokana na mambo ambayo unakabiliana nayo kisaikolojia.Ningependa kukuonyesha athari za kisaikolojia za madeni yaliyofikia kiwango hiki kwanza kabla hatujaangalia hatua za kuchukua.

Moja itakusababishia msongo mkubwa sana wa mawazo katika maisha yako.Mtaalamu wa saikolojia na mkurugenzi mtendaji wa Taasisi inayojihusisha na kupambana na vifo vinavyotokana na kujiua(suicide) nchini marekani anasema,madeni ni moja ya sababu kubwa inayowafanya watu wajiue.Hii hutokana na watu wengi kukumbwa na msongo mkubwa wa mawazo ambao inaonekana kabisa hakuna jibu la tatizo lao.Kama unataka usiishie wengine walikoishia ni lazima uamue kuamini kuwa kuna njia ya kutoka hapo ulipo.Wakati mwingine inaweza isikupelekee kufikiria kujiua bali inaweza kukuletea magonjwa ya moyo ambayo yatakusababishia matatizo makubwa ya kiafya,usikubali kuamini kuwa hakuna njia ya kutoka hapo ulipo,njia ipo.

Jambo la pili linalotokea watu wanapojikuta katika hali kama hii,ni ile hali ya kutokujiamini tena katika uwezo wao.Mara nyingi madeni huwa yanasababisha watu kupoteza mali zao ama kubadilisha “status” zao za maisha na kulazimika kuishi maisha ya chini kidogo,wengine huwasababishia kupoteza marafiki n.k.Haya yote huwapelekea watu kuanza kupoteza hali ya kujiamini katika maisha yao.Hata hivyo madeni huambatana na watu wengine kuamua kutokukuamini tena na wapo ambao watakusemea maneno makali utakaposhindwa kuwalipa na maneno ya kukatisha tamaa na wengine wanaweza hata kuamua kukuharibia sifa yako.Haya yote huwa yanasababisha watu wengi sana kupoteza uwezo wa kujiamini.Siku zote kumbuka kuwa uwezo wako hauondolewi na uwepo wa madeni katika maisha yako.Usikubali pia kujiingiza katika mkumbo wa watu wanaoishi kwa kujilaumu kwa sabbau madeni waliyonayo yamesabaishwa na maamuzi mabaya ama matumizi mabaya ya pesa ambayo waliwahi kuipata.Usikubali madeni yapoteze ndoto zako kubwa,kujiamini kwako ama kujiona mtu wa maana.Bado una nafasi ya kufanikiwa tena.

Hatua ya kwanza unayotakiwa kuichukua ni kukubali kwamba una tatizo la madeni.Hii itakusaidia kuanza kutafuta suluhisho mapema.Watu ambao bado hawajakubali kuwa wako kwenye tatizo la madeni hujaribu kuficha na kujaribu kutumia nguvu lii kuendelea kuishi maisha ya hali ya juu ambayo hawayawezi tena.Matokeo yake huwa ni ni nini?Huwa ni kuendelea kukopa zaidi na kujiingiza katika madeni makubwa zaidi.

Kukubali kuwa uko kwenye tatizo la madeni ni pamoja na kuchukua hatua za kuwaambia watu wako wa karibu ili upate mawazo kwao ama kutafuta wataalamu wa ushauri kuhusu maisha na tutakusaidia namna ya kuanza kujitoa katika shimo hilo.Usijaribu kuendelea kuishi ili kuwaridhisha watu wengine kuwa bado mambo yako yako safi huku wewe mwenyewe unajua kuwa unaumia ndani kwa ndani.

Hatua ya pili inayofuata ni kujaribu kuyatathmini madeni yako yote uliyonayo,asilimia ya riba,dhamana uliyoweka kwenye kila deni,madhara ya kutolipa kila deni n.k Hii itakusaidia kujua ni madeni gani yana athari kubwa zaidi kwa kutoyalipa ama kwa kiwango cha riba,au dhamana uliyoweka n.k.Orodhesha madeni haya katika karatasi ukizingatia yote haya na kisha yaweke katika orodha ya umuhimu wa kuyalipa kulingana na vigezo hivyo hapo juu.

Hatua ya tatu ni kuzungumza na wadeni wako.Watu wengi sana wakiwa kwenye hali ya madeni mengi huwa hawataki kuzungumza na wadeni wao na huwa wanawakimbia na hata kubadilisha namba zao za simu,hii itakuletea matatizo zaidi.Pamoja na kuwa wanakudai na wanataka pesa zao kumbuka kuwa watakuwa tayari kukusikiliza kama uan mpango mzuri.Pata muda wa kuzungumza nao,omba muda wa ziada ama kupunguza kiwango cha kila mwezi unacholipa n.k Ukionyesha kuwa una nia ya dhati ya kulipa,una mpango thabiti na unawajibika,wengi huwa wanakuwa tayari kukusikiliza na kukukubaliana na mapendekezo yako.

Hatua ya nne ni kuhakikisha kuwa unabadilisha mtindo wa maisha yako.Jitahidi kupunguza gharama za maisha ili upate pesa ya ziada kuanza kulipa.Pengine itakulazimu kuhamia nyumba nafuu,kuuza gari yako ya sasa na kununua isiyotumia mafuta mengi na inayohitaji vifaa vye bei nafuu,kubadilisha shule ya watoto waende yenye ada nafuu n.k Kumbuka kuwa hatua hizi zote ni za muda huku ukijenga uwezo mkubwa na utarudia maisha unayotaka hapo baadae.Inawezekana kutoka kwenye madeni.

Kitabu cha TIMIZA MALENGO YAKO kimechambua mbinu mbalimbali ambazo watu waliofanikiwa wamekuwa wanazitumia ili kufikia kilele cha mafanikio.Unaweza kukipata katika mkoa wowote ulipo,wasiliana nasi kupitia 0655 720 197 na kwa walioko Dar es Salaam unaweza kukipata katika maduka ya vitabu ama ukaletewa pale ulipo kwa bei ileile kupitia namba 0762 224 282.

 

Leave a comment

name*

email* (not published)

website