Navigate / search

Jinsi Ya Kutimiza Ndoto Yako Katika Mazingira Magumu

1

Samuel Walton alizaliwa na kukulia katika kipindi kigumu sana cha uchumi nchini marekani(Great Depression),na kwa kuwa familia yake haikuwa ya kitajiri alijikuta anapitia changamoto nyingi sana katika maisha yake ya kila siku.Ili aweze kufanikiwa kuendelea kuishi na kuwasaidia familia yake katika kuongeza kipato alilazimika kufanya kazi za hali ya chini ambazo zinadharauliwa na watu wengi.

Samuel alikuwa kila siku anaamka asubuhi na kukamua maziwa toka kwa ng’ombe mmoja aliyekuwa anamilikiwa na wazazi wake.Baada ya kukamua maziwa aliyaweka katika chupa ndogondogo na kisha akatumia baiskeli yake kuanza kutembeza na kuuza mitaani.Mara baada ya kumaliza kuuza maziwa asubuhi sana,aliendelea na kazi ya kusambaza magazeti ya  Tribune  yaliyokuwa yanatoka kila siku.

Wakati akiwa anasoma chuoni Samuel alifanya kazi mbalimbali ili kuweza kupata pesa za chakula na matumizi mbalimbali aliyokuwa anayahitaji.Kuna wakati alikuwa anafanya kazi kama mhudumu wa mgahawa na kisha mshahara wake ulikuwa ni kupewa chakula ambacho hakuwa na pesa yoyote ya kuweza kununua.Samuel alianza biashara ya kuuza duka la vitu mbalimbali akiwa na umri wa miaka 26 mara baada ya kutoka jeshini baada ya vita ya pili ya dunia.

Baada ya kuendelea kwa muda na biashara ya maduka madogomadogo baadaye alianzisha maduka makubwa ya kisasa(Supermarkets) na akayapa jina la WalMart.Samuel aliwahi kueleza kuwa mtaji wa duka lake la kwanza aliupata kwa kuchukua mkopo na baadaye akaendelea kufungua la pili na ndani ya miaka mitatu alikuwa amefikia kuwa na mauzo ya dola 225,000.Duka kubwa la WallMart alilifungua  July 2, 1962 eneo la Rogers, Arkansas.Baada ya hapo aliendelea kuwa tajiri mkubwa sana nchini marekani na kati ya mwaka 1982 hadi 1986 aliongoza katika orodha ya matajiri wa marekani kwa mujibu wa jarida la Forbes.

Hadi wakati Samuel anafariki mwaka 1992 alikuwa na matawi 1960 ya Supermarket za Wallmart na alikuwa ameaajiri watu takribani 380,000 na mauzo yake yalikuwa yamefikia dola bilioni 50 kwa mwaka;Je kwa mwaka huu itakuwa imefikia kiasi gani na kutakuwa na matawi mangapi ya WalMart duniani?

Hakuna mtu ambaye hana hatima kubwa katika maisha yake,hata wewe unayesoma Makala hii leo ningependa kukukumbusha kuwa unayo hatima kubwa sana inayokungojea mbele yako kama tu utafanya maamuzi yasiyoyumbishwa ya kuanza kufuatilia malengo yako na kuamini bila shaka kuwa utafanikiwa.Kupitia maisha ya Samuel kuna mambo mawili ambayo unatakiwa ujifunze kuhusiana na suala la mafanikio ya maisha yako.

Jambo la kwanza ni kuwa usikubali hali yako ngumu ya sasa ikukatishe tamaa kuendelea kuamini ndoto kubwa ya mafanikio iliyo mbele yako.Hakuna ubishi kuwa Samuel alikulia katika mazingira magumu sana yenye kukatisha tamaa katika maisha yake.Hebu fikiria maisha ya kukamua maziwa kisha kuzunguka na baiskeli kuyauza mitaani?

Hebu fikiria kuzunguka na magazeti na kupigwa na jua ukiyauza mitaani huku ukiambulia faida ndogo sana kwa kila kopi unayoiuza.Pamoja na hali hii ngumu ambayo kwa namna yoyote ile ilikuwa inatakiwa kumkatisha tamaa,Samueli aliamua kutokata tamaa na aliendelea kuamini kuwa kupitia bidii aliyokuwa nayo basi ni lazima kuna siku atafanikiwa.Hata wewe inawezekana umepitia,unapitia ama utapitia mazingira kama haya.Huu ni wakati ambao mtu yoyote yule ukimwambia kuhusu ndoto yako na akilinganisha na maisha unayoishi sasa hivi,unaonekana kama kituko kabisa.

Ni kama wakati Samueli anafanya “deiwaka”(dailyworker) katika migahawa ili tu aweze kupata chakula halafu mtu anakuja anamuuliza-“Hivi Samuel una ndoto ya kufanya nini kwenye maisha yako hapo baadaye?”,halafu Samuel anasema-“Mimi nataka kuja kumiliki maduka makubwa yenye matawi dunia nzima”-Bila shaka hata ungekuwa wewe ungeona anachekesha.Kama kweli ndoto yako ni kubwa basi lazima ukiisema kuna watu wataona unachekesha ama umechanganyikiwa katika maisha yako.Kwa namna yoyote ile usikate tamaa eti kwa sababu mazingira yako ya sasa hayafanani na kule unakotaka kwenda ama kuna watu wakisikia unachosema na ulivyo wanaona havifanani-Songa mbele,kumbuka kuwa kila aliyefanikiwa alikutana na hali hiyo katika maisha yake.

Jambo la pili la kujifunza kutoka  kwa Samuel ni kutumia kila fursa uliyonayo kwa sasa bila kujali ni ndogo ama haina hadhi kiasi gani.Kabla haujafikia kiwango cha kuiishi ndoto yako na kuanza kufaidi matunda ya bidii yako,kuna wakati utalazimika kufanya kazi au shughuli ambayo inaweza ikaonekana kama umefeli.Jambo kubwa unalotakiwa kuwa nalo ni kutopoteza picha yako kubwa ndani ya moyo wako wakati ukiwa unafanya jambo dogo leo.

Kati ya misemo muhimu ambayo uantakiwa kuikumbuka katika majira kama haya ni “Dream Big but Start Small” yaani uwe na ndoto kubwa lakini uwe tayari kuanza kidogo.Haijalishi ndoto yako ni kubwa kiasi gani ni lazima uanze mahali fulani,na mara nyingi mahali pa kuanzia patakuwa padogo sana.Leo Jiulize,katika ndoto kubwa niliyonayo ninaweza kuanzia wapi?Usikubali wazo la kukuambia kuwa utaanza ukishapata mtaji mkubwa ama ukishafanikiwa kiwango fulani,ukiwa mtu wa kusubiri huo utakuwa ni mwanzo wa kufeli-Kwa chochote unachotaka kufanya lazima kuna hatua ndogo ya kuchukua.Leo usikubali kumaliza siku yako kabla haujaanza hatua ndogo itakayokusaidia kuelekea katika lengo lako.

Naamini wewe ni Samueli ajaye katika kile unachotaka kufanya,Usikubali uishie njiani.Dunia inasubiri ndoto yako itimie,kuna watu wengi hatima zao zinategemea mafanikio ya ndoto yako,kuna watu ajira zao ziko mikononi mwako-Hakikisha hauwaangushi.
Kumbuka kuwa ndoto yako Inawezekana.

Endelea kutembelea www.JoelNanauka.Com ili kujifunza zaidi.
Ndoto Yako Inaezekana.
See You At The Top.

Leave a comment

name*

email* (not published)

website