Navigate / search

Jinsi ya Kupata Fursa Kubwa Ya Mafanikio

Kwenye maisha fursa moja tu inatosha kabisa kubadilisha hali yako ya sasa na kukuweka kwenye kiwango kingine kabisa cha mafanikio.Kuna watu wengi sana ambao waliwahi kufikiria kuwa maisha yao yatachukua miaka mingi sana kabla hayajabadilika na kwa mshangao wao walipoanza kufanya vitu sahihi wakakutana na mabadiliko makubwa sana katika maisha yao kwa kupitia fursa moja tu.

Kufanikiwa kwenye maisha ni matokeo ya kujua mambo sahihi ya kuyafanya.Ni kama ilivyo wakati unapotaka kufungua mlango uliofungwa,unachohitaji ni ufunguo sahihi wa kutumia na sio vinginevyo.

Ili ufanikiwe lazima uwe mtu mwenye bidii na ambaye unawathamini watu bila kujali hali zao za sasa.Ili kutoka hapo ulipo na kwenda kule unakotaka unahitaji watu wa kukuunganisha na fursa mpya,kukuonyesha njia nzuri ya kufanya mambo,wa kukurekebisha  na watu ambao unaweza kujifunza kwao.

Mwaka 2012 mmiliki wa kampuni kubwa ya vifaa vya michezo ya Modell nchini marekani,bwana Mitchell Modell alifanya tukio la ajabu sana lililotoa funzo kubwa la mafanikio katika maisha yetu ya kila siku.Aliamua kujibadilisha mwonekano wake kwa kunyoa nywele zake zote na kuweka ndevu nyingi sana za bandia na pia kuvaa hereni sikio moja.Kisha baada ya hapo alienda kuomba kazi kwenye kampuni yake na akaanza kufanya kazi ya daraja la chini kabisa.

Akiwa ameajiriwa bila watu kujua kuwa ndiye mmiliki alikutana na wafanyakazi wengi sana wa aina mbalimbali.Kati ya wafanyakazi katika tawi lile alikuwepo dada mmoja anayeitwa Angel ambaye alikuwa ana watoto 3 ila hakuwa anakaa na mume wake na kwa muda wa miaka 2.Lakini pia,Angel na watoto wake wamekuwa wanaishi kwenye vibanda kwani hakuweza kulipia pango kwenye nyumba nzuri ya kuishi.Gharama zote za chakula,ada,matibabu na mavazi ya watoto yote ilikuwa juu yake.

Pamoja na hali yake hiyo,Angel alikuwa ni mfanyakazi anayewahi kazini kila siku na alikuwa anafanya kazi kwa bidii sana.Hata wakati wengine walikuwa wanalamika juu ya mshahara,yeye kazi yake ilikuwa ni kuwatia moyo na kuwahamasisha wafanye kazi kwa bidii sana akiamini ipo siku mambo yatakuwa mazuri.Kila wakati Bwana Mitchell alipokuwa anamkuta Angel,alikuta anafanya kazi zake kwa umakini na hata akikuta anaongea na wenzake basi itakuwa ni kuwatia moyo na kuwapa hamasa na kuwataka waaache kulalamika.

Wakati Bwana Mitchell akiwa kama mfanyakazi mpya alihitaji sana msaada wa kufundishwa jinsi mfumo unavyofanya kazi na mambo mengine.Kila mmoja alikuwa hayuko tayari kumfundisha,ila Angel alikuwa tayari kumfundisha na kumsaidia hata na kazi ambazo alikuwa hawezi kuzifanya kutokana na ugeni wake.Na kwa sababu ya ukaribu wake ndipo alipoweza kumfahamu Angel na kuyajua maisha yake kwa undani.

Baada ya siku kadhaa za kufanya kazi bila mtu yoyote kujua kuwa ndiye mmiliki,ndipo alipoamua kufanya kitu kikubwa kwa Angel.Kwanza alimpandisha cheo na kumfanya kuwa meneja msaidizi na kisha alimpa zawadi ya dola laki mbili na hamsini(Takribani shilingi milioni 500 za kitanzania) ili aweze kupata nyumba nzuri ya kuishi.

Baada ya tukio hili kutokea wafanyakazi wengi sana walijilaumu na walitamani sana kupata fursa upya kama wangejua kuwa yule alikuwa ni mmiliki.

Ndivyo maisha yalivyo na ndivyo safari ya mafanikio ilivyo.mara zote huwezi kujua ni wakati gani fursa kubwa inayohusu maisha yako itakutokea.Kilichomfanya Angel kufanikiwa ni ile hali ya kuwa ni mtu ambaye hakuruhusu jambo lolote limzuie kufanya kazi kwa bidii na kwa ufanisi kila wakati hata kipindi ambacho maisha yake yalikuwa magumu.

Mara nyingi unaweza kujikuta katika hali ambazo zinakatisha tamaa na zinakupa uhalali wa kila namna wa wewe kuwa mtu wa kulalamika na kukata tamaa.Hebu fikiria mama wa watoto watatu,analipwa mshahara mdogo lakini bado anawahi ofisini na huwa halalamiki.Kuna fursa nyingi kwenye maisha unazikosa kwa sababu ya malalamiko juu ya hali inayokuzunguka.Kitu cha msingi unachotakiwa kujua ni kuwa kulalamikia kitu au mtu hakuwezi kubadilisha hali yako ya sasa lakini kufanya kwa bidii kunaweza kufungua fursa nyingi kubwa katika maisha yako.

Inawezekana kazi unayoifanya ni ndogo ukilinganisha na ndoto kubwa uliyonayo,inawezekana mshahara unaolipwa sio mkubwa kama unavyotaka,inawezekana biashara yako bado haifanyi vizuri kama mipango yako ilivyo ama hauna mtaji kiwango unachotaka.Katikati ya hali hii unachotakiwa kufanya sio kuanza kulalamika na kukata tamaa,unatakiwa kuwa kama Angel,weka kiwango kikubwa cha bidii kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unajifungulia milango mikubwa zaidi katika maisha yako.

Kuanzia leo fanya maazimio katika maisha yako kuwa utakuwa mtu wa kufanya kwa bidii kile ambacho unakifanya hata kama itakuwa kwenye mazingira magumu,kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unajitengenezea fursa kubwa sana mbele yako.Ukiamua kuishi kwa mtazamo huu,muda mfupi sana ujao utafanikiwa.

Kitu kingine cha msingi cha kukizingatia hapa ni kuwa usidharau watu katika maisha yako.Kati ya mafumbo makubwa ambayo Mungu ameyafumba ni kuhusu hatima za watu ambao tunakutana nao kila siku katika maisha yetu.Hakuna kitu kibaya kama kumdharau mtu eti kwa sababu anaonekana kwa wakati huo hawezi kukusaidia chochote.Jifunze kumuheshimu na kumthamini kila mtu.

Ilil ufanikiwe katika maisha yako jifunze kuishi kama Angel,jifunze kuwa na bidii ya kazi hata katika mazingira magumu lakini pia jifunze kuthamini kila mtu ambaye unakutana naye-Kuanzia mdada wa kazi nyumbani,mlinzi,mfagizi,kondakta wa daladala hadi dereva wako.Kila mtu ni muhimu na ana mchango katika maisha yako.Kanuni ya maisha inasema-“Husiana na watu kama wewe unavyotaka watu wengine wahusiane na wewe pia”.Kuanzia leo ishi na kila mtu kama “Mitshell wako” wa kukuunganisha na fursa kubwa uliyokuwa unaisubiria.

Sina shaka kuwa fursa yako kubwa iko njiani inakuja,usikate tamaa.

Kumbuka kuwa ndoto Yako Inawezekana,

See You AT The Top.

©Joel Nanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website