Navigate / search

Jinsi Ya Kujenga Msingi Wa Mafanikio

Siku moja mwandishi mmoja wa habari alikuwa akimhoji Muhamadi Ali,bingwa wa ngumi za uzito wa juu wa wakati huo na akamuuliza kutaka kujua nini huwa kinamtia hamasa zaidi katika kufanya mazoezi kwa bidii.Jibu lake lilikuwa linafurahisha sana pale aliposema-“Kila siku huwa nikitaka kwenda kufanya mazoezi huwa nasikia uchovu na natamani kuendelea kulala,ila huwa najiambia,ni bora niishi kwa sasa kama mtumwa ili nije kuishi kama mfalme hapo baadaye”.Fikra ya namna hii ndio ilimsaidia kufika kule ambako alikuwa anataka kwenda.

Tunaishi katika kizazi ambacho uvumilivu unazidi kupungua sana kwenye maisha ya watu wengi,na hii inawasabishia watu wengi wakate tamaa kwa haraka kuliko kawaida.Katika ulimwengu wa sasa,watu wameaminishwa kuwa kila kitu ni lazima kitokee kwa haraka kama wanavyoataka wao na hakuna mtu ambaye yuko tayari kusubiri.Hii ndio maana makampuni mengi kwa kugundua hila kila kitu wanachofanya huwa wanaweka na maneno ya kuonyesha kuwa utapata kwa haraka.Ni kama vile kila mtu anaaminishwa kuwa atapata anachotaka bila kuchelewa-Hii ndio maana leo tuna internet ya kasi,fast food,fast jet,mabasi ya mwendokasi n.k

Mtazamo huu wa maisha umewafanya watu wengi sana washindwe kufika wanakokwenda kwani kila wakati huwa wanaamini kila wanachotaka wanataka wapate papo kwa hapo.Kuna watu wanataka kuwa kama Aliko Dangote ila wanasahau kuwa Dangote ana miaka zaidi ya 30 kwenye biashara anayofanya na anaamka kabla yao hadi leo na wanapoenda kulala yeye bado anaendelea kufanya kazi.

Siku moja nilimsikia mtu anamzunguzia mchungaji mkubwa sana wa Nigeria anaitwa Dr.David Oyedepo ambaye wakati huo alikuwa ndiye mchungaji tajiri zaidi duniani na alikuwa na ndege nne na vyuo vikuu 2.Huyo mtu akasema,huyu mtu ana bahati sana,yaani amekua kwa kasi kuliko kawaida.Baada ya muda mfupi nilibahatika kusoma moja ya kitabu chake kianchoitwa “The Pillars of Destiny”(Nguzo zinazojenga Hatima)-Na nikakutana sehemu anayosema-“Sishangai kwamba niko tajiri hivi leo,ila ningeshangaa kama nisingekuwa tajiri hivi.Kuna watu wanasema nina bahati.Ni kweli nina bahati kwani tangu mwaka 1980 nafanya kazi masaa 16-18 kila siku,nimesoma maelfu ya vitabu,sifanyi kitu kingine isipokuwa kimoja nilichochagua,sijawahi kukatishwa tamaa na maneno ya watu-Hiyo ndio bahati yangu”

Watu wengi sana waliofanikiwa ukiowaona huwa unafikiri  wamefika hapo kwa haraka sana mara moja,sio kweli.Kuna mambo mengi sana ambayo hauyajui ambayo wameyapitia,wameyavumilia na kuyashinda hadi wamefanikiwa kufika hapo walipofika leo.Na wewe ili ufike unakotaka ni lazima uwe mtu ambaye uko tayari kuvumilia changamoto zote ambazo zinakukabili.Kuna mambo mawili ya kuyazingatia hapa:

Moja ni kuwa ili upate unachokitaka kwa kiwango cha juu ni lazima uamue kuachana na mambo mengi ambayo wengine wanayafanya.Hakuna namna unaweza kuishi maisha kama ya watu wengine na wewe usifanane nao.Ukiona kila kitu unachofanya,maisha unayoishi,ratiba yako ya kila siku,matumizi yako,unachoangalia na kusoma kinafafana na wengine basi ujue ni lazima utafanana nao kwenye matokeo.Kama unataka kufanikiwa zaidi ya watu wa kawaida ni lazima uchague maisha ambayo sio ya kawaida.Amua kuanza kuwekeza leo katika ndoto yako-Tumia pesa kununua vitabu,jinyime baadhi ya vitu na uwekeze,tumia muda wako kujifunza vitu vya kukusaidia n.k.Utakapokuwa unafanya hivyo kuna watu wengi sana ambao hawatakuelewa kabisa lakini uwe na uhakika kuwa hicho ndicho kitakachokutofautisha na wengine.Leo jaribu kujichunguza-Unavyoishi kuna tofatui na wafanyakazi wenzako hapo kazini?Kuna tofauti na wafanyabiashara wenzako wanaokuzunguka-Kama hauoni tofauti ina maana hautatofautiana nao kabisa katika matokeo yako.Kumbuka mafanikio yako ni matokeo ya uwekezaji wako;je unawekeza nini LEO ili uvune mambo Makubwa KESHO?

Mbili ni lazima uwe tayari kusimama peke yako.Kuna watu wengi ni waoga sana kusimamia wanachokiamini peke yao.huwa wanatamani kila wakati kuwe na watu ambao wanawaunga mkono.Siku zote kumbuka kuwa unapokuwa na ndoto kubwa sio kila mtu ataiamini na sio kila mtu ataona kama wewe unavyoona.Ukishapata uhakika wa ndoto yako ambayo unaifuatilia kwenye maisha yako,weka msimamo kuwa bila kujali ni nani yuko upande wako na ni nani hayuko na wewe bado utaisimamia ndoto yako kwa nguvu.

Mara nyingi watu wako tayari kukupa sapoti pale ambapo unafanya mambo ya kawaida,lakini mara utakapoanza kufanya mambo ambayo ni zaidi ya ilivyozoeleka utashangaa kuona hakuna mtu anasimama na wewe tena.Ikifika wakati huu usiogope kuendelea eti kwa sababu hakuna mtu yuko upande wako.Kama una ndoto kubwa,basi jiandae kusimama peke yako.

Ni kweli utasikia maumivu,ni kweli utasikia upweke,ni kweli utasikia umeachwa peke yako,ni kweli utaonekana wa ajabu,ni kweli watakusema vibaya-Ila kumbuka,kuwekeza kwenye ndoto yako kunalipa sana.

See You At The Top

@JoelNanauka

#TIMIZAMALENGOYAKO

Leave a comment

name*

email* (not published)

website