Navigate / search

Jinsi ya Kuishinda Hofu Inayowafanya Wengi Wasifanikiwe

maxresdefault

Bill Cosby siku moja aliwahi kusema “In order to succeed, your desire for success should be greater than your fear of failure”(Ili ufanikiwe,ni lazima shauku yako ya kufanikiwa iwe kubwa kuliko hofu yako ya kufeli).Watu wengi sana hivi leo wamebakia kuwa watu wa kawaida sana katika maisha yao kwa sababu wanaogopa kufanya kitu kipya ambacho hawajawahi kufanya hapo kabla.Watu wengi hawajui wanaweza kufanikiwa kiwango gani kama wakiamua kutoogopa kufeli katika kuelekea malengo yao.Kwa sababu ya hofu ya kufeli watu wengi wameendelea kufanya mambo ambayo kiukweli ni kuwa hawayapendi na hawayafurahii,kwa sababu ya kuogopa kushindwa katika maisha watu wengi wamebakia katika kiwango kimoja cha maisha yao bila kupiga hatua kwa muda mrefu.

Hata wewe ukijichunguza leo,unaweza kugundua ni mara ngapi umekosa fursa katika maisha yako kwa sababu tu uliogopa kuchukua hatua fulani ya muhimu.Kuna watu wakiona kazi wanaacha kuapply eti kwa sababu tu wanaogopa hawataitwa kwenye usahili.Kila malengo uliyonayo katika maisha yako lazima utakutana na hofu ya kutofanikiwa.Kumbuka kuwa ujasiri sio hali ya kutohisi hofu kabisa katika maisha yako bali uwezo wa kuikabili.Kuna watu wengi hawataki kufanya biashara kwa sababu wanahofu ya kupata hasara,kuna watu wengi wanaogopa kilimo kwa sababu wanahisi hawatafanikiwa,kuna wengi ambao wanaogopa kuanza upya kwa sababu hawana uhakika kama watafanikiwa n.k.Kiufupi ni kuwa kuna uwezo unashindwa kutumika ndani yako kwa sababu ya hofu yako ya kufeli.

Hofu ya kufeli mara zote inaambatana na hali ya kuona aibu kama ikitokea umeshindwa kufanikiwa.Watu wengi kama wangepelekwa kwenye kisiwa ambacho wanaishi wao peke yao na hakuna mtu mwingine ambaye yuko pamoja nao basi wangekuwa tayari kujaribu mambo mapya na kuchukua hatua bila hofu ya kufeli.Mara nyingi kinachowafanya watu washindwe kuchukua hatua katika maisha yao ni ile hali ya kuogopa kuwa kufeli kwao kutawaletea aibu.Hii imejengwa tangu utotoni na shuleni.Hata wewe hebu jiulize,kinachokufanya hasa usifanye kile unachokipenda/usichukue hatua inayotakiwa katika maisha yako ni nini?Hofu inakuandama.

Nakumbuka tukiwa tunasoma shule ya msingi mwisho wa muhula kulikuwa na utaratibu wa kutaja kumi bora na wanapigiwa makofi na kupewa zawadi na wale kumi wa mwisho wallikuwa wanaitwa kumi dhaifu na tulikuwa tunawazomea.Hali hii ilitengeneza hisia ndani ya mioyo ya wengi kuwa ukifeli basi wewe utakuwa mtu wa kuzomewa maishani na ikasababisha kuona kama hakuna kitu unaweza kujifunza katika kufeli kwao.Kwa upande mwingine kilichokuwa kinawafanya watu wapende kufaulu sio ile ile shauku ya kufanya vizuri bali hofu ya kuzomewa.

Kuna watu wengi sana leo,wanaishi maisha ambayo hayaongozwi na shauku ya kitu fulani bali yanaongozwa na hofu ya kufeli.Kuna watu wako kwenye kazi wasizozipenda sio kwa sababu wanashauku ya kufanikiwa katika kazi hivyo bali kwa sababu wanahofu ya kutafuta kazi mpya ama wana hofu ya kuanza kujiajiri.
Kwa upande mwingine hofu ya kutofanikiwa imesababishwa na ile hali ya kuonekana hauko sahihi katika kile unachokifanya.Siku zote mafanikio huambatana na kuchukua hatua zisizo za kawaida na ambazo hazijazoeleka.Watu wengi wamekulia katika mazingira ya kuambiwa na kuonyeshwa kuwa hawako sahihi kwa kile wanachokifanya.

Utakumbuka hata ulipokuwa mtoto mdogo kila kitu ulikuwa ukigusa badala ya kuelekezwa ulikuwa unaambiwa-“Acha hivyo”,ukijaribu kufanya kitu utaambiwa-“Usifanye hivyo,huwezi” n.k.Maneno haya yote yametengeneza hali katika ufahamu wetu wa kujiona kuwa sisi ni watu ambao hatuwezi kufanikiwa kwa namna yoyote ile.Hivyo mara nyingi huwa kabla hatujachukua hatua swali la kwanza huwa haliwi-“Hivi hii ni hatua sahihi?” bali swali la kwanza huwa-“Hivi watu hawatasema nimekosea?”.Ni rahisi sana kujua hili kwani hata inawezekana wewe ni mmoja wa wale watu ambao ukivaa nguo asubuhi huwa cha kwanza kujiuliza ni,”Hivi watu watasemaje?”.Hii imesababisha watu wengi waishi kwa kutegemea mawazo na maoni ya wengine na wameshindwa kuamini katika kuchukua hatua muhimu zitakazobadilisha maisha yao.Kama umeamua kufanikiwa usiwe mtu mwenye hofu ya kuogopa kuonekana umekosea.

Confucious aliwahi kusema kuwa “Our greatest glory is not in never falling, but in rising every time we fall.” (Utukufu wetu mkubwa haupo kweny kutokuanguka bali upo kwenye kuinuka kila mara tunapokuwa tumeanguka).Leo amua kujaribu na kuchukua hatua muhimu katika maisha yako bila hofu ya kuonekana umekosea.

Ili uishinde hofu yako ya kufeli ni lazima uwe mtu ambaye uko tayari kukubali kwamba kuna hofu inakusumbua katika maisha yako.Kama wewe ni mtu ambaye unajua kabisa unasumbuliwa na hofu ya namna hii,hatua ya kwanza ni wewe kukiri kwanza na kutafuta kusaidiwa.Tafuta mtu unayemwamini na anayeweza kukushauri na umwambie kuwa unasumbuliwa na hofu ya kuogopa kufeli katika kufanya mambo.Hofu hii inaweza kuwa imetokana na historia yako huko nyuma ama mambo uliyowahi kuyashuhudia.
Baada ya kutambua hofu zako na kisha kushirikisha mtu mwingine andaa mkakati wa kuishinda hofu inayokusumbua mapema iwezekanavyo na wala usisubiri siku moja zaidi ipite.Namna nzuri ya kuishinda hofu ni kufanya kile unachokiogopa.

Hii ndio maana Eleanor Roosevelt aliwahi kusema-“Do one thing every day that scares you.” (Kila siku fanya kitu kimoja ambacho unakihofia).

Ili ufanikiwe ni lazima uwe tayari kuishinda hofu inayozuia mafanikio yako,ni lazima uishinde hofu ya kuogopa kufeli.Leo Anza kuchukua hatua ya kuelekea katika mafanikio yako makubwa kwa kuanza kufanya kile ambacho kimekuwa kinakutia hofu.
Kumbuka kuwa Ndoto Yako Inawezekana.
Endelea kutembelea www.JoelNanauka.Com na www.Mentorship.co.tz ili kujifunza zaidi.Kwa ushauri na mafunzo zaidi tuwasiliane.
See You At The Top.
©JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website