Navigate / search

Jinsi Ya Kuharakisha Mafanikio Yako

Kwa mwanadamu yoyote yule wa kawaida ni lazima siku zote huwa anatamani kutoka hatua moja kwenda nyingine.Ingawa hii ni shauku ya kila mtu na ninaamini na wewe ni shauku yako pia,swali kubwa ni kuwa kwa nini watu wengi huwa maisha yao hayabadiliki?. Nimeshawahi kukutana na watu wengi sana ambao kila siku wana mawazo mapya tena ni mawazo mazuri sana ila tatizo lao ni kuwa huwa hawachukui hatua kabisa hata kama wanajua wanachotakiwa kukifanya ili waweze kufanikiwa.

Pengine hata wewe unaposoma makala hii leo, una mawazo mengi sana tena makubwa ambayo yakifanikiwa basi utabadilisha maisha yako kwa kiwango kikubwa.Wakati tunauanza mwaka huu nakumbuka jinsi ambavyo watu wangu wa karibu kila mmoja alikuwa amejiwekea malengo yake ya jinsi ambavyo anataka mwaka huu uwe ni wa kubadilika kabisa.Kuna baadhi yao walijiwekea malengo kuwa mwaka huu lazima waache kazi mahali walipoajiriwa na waanze kujiajiri,wako wengine walidhamiria kuanzisha biashara zao mpya,wapo wengine walisema watajenga nyumba na wengine pia waliweka malengo ya kuingia katika ndoa.

Wengi wa wale ambao nimefanikiwa kuwauliza tukiwa tayari tumeshavuka nusu ya mwaka wanaonekana bado hawajaweza kufikia hata robo ya malengo yao na wengine hawajaanza kabisa.Sina uhakika kwa upande wako,je-Malengo yako ya mwaka huu umeyafanikisha kwa kiwango gani hadi sasa?

Jambo la Kujiuliza ni kwa nini watu wengi huwa hawafanikiwi katika kutekeleza mawazo yao.Ukweli ni kuwa pamoja na kila mtu kuwa na shauku ya mafanikio na kutimiza malengo yake,kuna mambo mawili ambayo ukiyafahamu na kuyafanyia kazi kuanzia leo basi utajitoa katika kundi ambalo kila mwaka huwa wanashindwa kufikia malengo yao.

Kwanza kabisa,Usijipe jibu la hapana kabla haujafanya.

Miaka kadhaa iliyopita mwandishi maarufu wa vitabu Dr.Myles Munroe kutoka nchini Bahamas aliwahi kushauriwa na rafiki yake amtafute mtu maarufu sana anayeishi Marekani ili amwandikie neno la utangulizi katika kitabu chake kipya.Baada ya kuambiwa hivyo jibu lake likawa,“Hata nikumuomba hatakubali kwani hanifahamu kabisa” .Rafiki yake akamwambia “Usijiambie hapana kabla haujajaribu kufanya”.Cha ajabu ni kuwa baada ya kumuomba huyo mtu,alikubaliwa bila matatizo yoyote ndani ya muda mfupi sana.

Nimekutana na watu wengi sana ambao mawazo yao yanahitaji msaada wa mtu, kampuni au taasisi fulani ili waweze kupiga hatua ya mbele zaidi.Cha ajabu nikiwauliza kwa nini hawajachukua hatua huwa wanasema, “najua hatakubali nikimwambia.”Kuna watu wengi sana ambao ndoto zao zimeshindwa kufanikiwa na malengo yao yameishia njiani kwa sababu tu wamejipa majibu ya kutokuwezekana kabla hata hawajajaribu kufanya.

Ili ufanikiwe maishani, usiwe mtu wa kujipa jibu la hapana kabla haujajaribu. Utashangaa sana mambo mengi na watu wengi ambao unadhani watakuambia hapana siku ukija kuwashirikisha wanakubali ama wanakuunganisha mahali sahihi pa kukusaidia kufanikiwa.Je kuna wazo umeshawahi kuwa nalo katika maisha yako lakini umeshindwa kulifanyia kazi kwa sababu kila wakati ukifikiria unajipa jibu la hapana na haiwezekani?Kuna biashara ambayo umeshawahi kuifikiria kuifanya mwaka huu lakini kila wakati ukiifikiria huwa unajipa jibu kuwa haitawezekana?Au kuna mtu umetamani kumpigia simu au kuonana naye tangu muda mrefu kwa ajili ya kukusaidia katika jambo fulani kwenye maisha yako lakini kila wakati ukifikiria unaogopa kuwa atakataa?

Watu wengi sana wmeshidnwa kufanikiwa kwenye maisha kwa tabia ya kujipa jibu la hapana na kuogopa kukataliwa kabla hawajajaribu.Ili ufanikiwe ni lazima uwe tayari kuchukua hatua na kamwe usijipe jibu la hapana.

Leo, chukua hatua kuelekea katika kufanyia kazi mipango yako. Mpigie simu unayehitaji akusaidie, nenda ofisini kwake, andika barua pepe n.k. Chukua hatua bila woga nawe utashangaa.Mambo mengine ni kama milango inayofunguka yenyewe,huwa haifunguki hadi uisogelee.Mambo makubwa kwenye maisha huwa hayaji kwa sababu unayasubiria bali kwa sababu unayafuata.

Pili anza na Kidogo ulichonacho

Kuna watu wengi sana huwa wanachelewa kufanikiwa kwa sababu mara zote huwa wanajiona hawana vya kutosha kufanya walichokusudia.Wengine watakuambia elimu yao ndogo,wengine watakuambia mtaji wao mdogo na wengine watasema uzoefu wao mdogo;ili mradi tu wanaona bado hawajajitosheleza kufanya kile wanachotamani katika maisha yao.Lakini wakati wanatoa visingizio vya namna hiyo kuna watu kama

Mara nyingi watu wa namna hii huwa wanajifariji kuwa wataanza kesho tutakapokuwa na vitu tunavyovihitaji.Ila cha kushangaza ni kuwa hata kesho ikifika wanajikuta wanasubiria kesho nyingine.Ukweli ni kuwa watu wanaosubiria kesho kukamilisha jambo fulani huwa hawafanikiwi kwa sababu kesho huwa haifiki

Badala ya kusubiria kesho ifike utakapokuwa umekamilisha kila unachotaka nakushauri anza na hatua iliyo katika uwezo wako kwa leo wakati unaendelea kutumaini kuifikia hatua ambayo iko juu ya uwezo wako kwa kesho.

Kuna kanuni katika kuelekea mafanikio inaitwa “kanuni ya kulimbikiza nguvu”, kanuni hii inazungumzia nguvu ya mkusanyiko wa mambo mengi unayofanya ili kutimiza jambo fulani. Mfano rahisi ni pale unapoamua kuvunja ukuta kwa kutumia nyundo yako. Unaweza ukapiga sana hadi nyundo ya mia mbili ndio ukuta ukaanguka. Lakini swali ni je, ni nguvu ya nyundo ya mia mbili ndio iliyoangusha ukuta? HAPANA. Ukuta umeanguka sio kwa nyundo moja ya mwisho bali kwa mkusanyiko wa kila pigo la nyundo ulilopiga hata kama ilikuwa haionyeshi dalili yoyote ile.

Katika safari ya mafanikio ndio vivyo hivyo, kila unachofanya kuelekea mwelekeo wa ndoto yako kina faida. Siku inakuja ambapo utashangaa ghafla “ukuta umeanguka”-Umepata kile unachotaka.

Watu wote waliofanikiwa hakuna aliyeanza na vingi ama aliyeanza juu,walianza na kidogo walivyonavyo na waianza pale walipo.

Leo,unapoanza siku yako orodhesha mambo ambayo unatakiwa kuyafanya katika kuchukua hatua ya kuelekea mafanikio yako.Usikubali kuwa mtu unayesubiria vingi ili uanze kufanya,anza na kidogo ulichonacho leo.

See You At The Top

Joel Nanauka

 

Leave a comment

name*

email* (not published)

website