Navigate / search

Jinsi Unavyoweza Kufanikiwa Ndani ya Muda Mfupi Kama Lufefe

saouth

Leo ukibahatika kufika mitaa ya jiji la Capetown nchini Afrika Kusini na ukaulizia “Mfalme wa Spinachi” basi hakuna shaka utapelekwa moja kwa moja nyumbani kwa Lufefe Nomjana,kijana mwenye umri wa miaka 28 anayemiliki kampuni ya Espinaca Innovations ambayo ni maarufu kwa kutengeneza mikate yenye spinachi na bidhaa zingine zinazotokana na spinachi.

Mwezi huu amefungua ofisi yake nyingine kupitia ufadhili wa Helath Club Group,Virgin Active,na pia ana mpango wa kuanzisha kiwanda chake ifikapo mwezi wa Agosti baadae mwaka huu.Ila swali kubwa ambalo kila mtu anajiuliza,Hivi amewezaje kufikia hatua hii kubwa kwa muda mfupi?

Mwaka 2012 akiwa alikuwa anajitolea katika bustani moja ya jumuiya ya mtaani kwao ambapo walikuwa wanalima spinachi nyingi sana na kisha kuziuza.Baadae anasema aliamua kutafuta kwenye mtandao na “aka-google” ili kutafuta namna ya kutumia zao la spinach kwa namna mbalimbali na akakuta kumbe unaweza kutengeneza mkate mtamu sana kwa kutumia spinachi.Mara baada ya kujifunza aliamua kwenda kwa jirani yao mmoja ambaye alikuwa na oven ili aweze kuanza kutengenza mkate.Alianza biashara kwa kununua vitu vya kwanza vilivyohitajika kutengenezea mkate kwa kututmia randi 40(dola 2.6) aliyokuwa nayo wakati huo.

Baada ya kuanza kutengeneza,jirani yake alimwambia atatakiwa awe anatumia oven wakati wa usikua ambao wao watakuwa wamelala na hawatahiitaji na atatakiwa kulipia gharama za umeme na akakubali.Baada ya kuanza kutengeneza mikate minne kila usiku na kisha minane,kisha 16 ambayo ndio ilikuwa idadi kubwa ambayo angeweza kuitengeneza kwa usiku mmoja.Anasema kila siku idadi iliongezeka ya watu waliokuwa wanahitaji mikate yake na ukweli ni kuwa hakuwa anatengeneza faida ya kutosha kwani gharama ya mkate ilikuwa ni randi 9.8 na yeye ilibidi auze kwa randi 10.Anachosema ni kuwa suala la muhimu katika hatua hiyo ilikuwa ni kutengeneza jina kwa wateja wake na kujifunza zaidi.

Mwaka 2013 alienda kuongea na meneja wa kampuni ya Spa na akamuomba amruhusu awe anatumia oven zake kuokea mikate wakati zinapokuwa hazitumiki na pia atumie baraza la nje ili auzie mikate.Baada ya kukubaliwa na kuanza,alijikuta anauza mikate 200 kwa siku.Aliamua kuajiri vijana wachache ambao walikuwa pia wanazungusha mikate na kupewa kamisheni kwa kila mkate wanaouza.Baadaye aliwanunulia baisikeli na pia akawatengenezea matsheti ya kuvaa wanapokuwa wanaenda kuuza.Lufefe pia aliomba kontena kutoka kampuni moja mjini CapeTown na akaanza kuitumia kama ofisi yake ya mauzo baada ya kuikarabati.Leo hii kampuni yake inazalisha zaidi ya mikate 500 kwa siku na lengo lake ni kuwa kabla mwaka huu haujaisha basi awe anazalisha mikate isiyopungua 2000 kupitia kiwanda chake kidogo ambacho atakuwa amekianzisha.

Hivi unajua kuwa fursa za mafanikio zimetuzunguka kila siku?Kila Mahali tulipo kuna fursa lukuki kama tukiamua kuishughulisha akili yetu kutafuta mbinu mpya za kufanya mambo.Kuna mambo ya msingi sana ya kujifunza kuhusu lufefe.

Moja ni kuwa alikuwa mtu anayependa kudadisi na kutafuta taarifa.Hakuna shaka kuwa lufefe ni mtu alliyekuwa kila wakati anataka kuongeza maarifa juu ya kile alichokuwa anafanya ama anatamani kufanya.Uzuri wa nyakati tunazoiishi ni kuwa kila taarifa unayoitaka inaweza kupatikana kirahisi sana.Inategemea wewe unataka kufanya nini,basi chukua hatua kutafuta taarifa ambazo zinaweza kukusaidia kufanikisha kile ambacho unataka kufanya.Kwenye mitandao kumejaa mambo mengi sana,mengine ya kuburudisha na mengine ya kufurahisha na yapo mengi ya kufundisha.Jiwekee nidhamu katika maisha yako kila siku kutafuta taarifa mpya na muhimu inayohusiana na kile ambacho unataka kufanya katika maisha yako.Hebu fikiria kwa kile unachotaka kufanya,kwa ile ndoto yako,umeshajifunza mambo mangapi kuhusiana na ndoto yako?Usichokijua ni kuwa taarifa moja tu ambayo unaweza kuipata leo inawezekana kuwa ndiyo unayoihitaji kufikia mafanikio yako.Usiwe mvivu,tafuta taarifa-Soma vitabu,Makala,CDs,DVds zinazofundisha mambo ambayo unataka kuyafanya katika maisha yako.

Jambo la pili ni kuwa tafuta kila njia ya kutimiza kile ambacho unataka kukifanya katika maisha yako.Usiogope kuwaambia watu kuwa unahitaji kitu fulani.Lufefe hakusubiri hadi awe na uwezo wa kununua oven yake mwenyewe,alichofanya ni kuangalia nani anaweza kumtumia ili afanikishe ndoto yake.Katika kila unachotaka kufanya kuna mtu mahali ana fursa unayoweza kuitumia.Kitu kikubwa ni kuwa na ujasiri wa kwenda na kuongea na mtu huyo,usiogope na usijiambie hapana/haiwezekani kabla haujachukua hatua.Unachotakiwa kuzingatia ni kuwa na uwezo wa kueleza kwa ufasaha kile unachotaka kukifanya na pia kuwa mwaminifu kwa makubaliano yoyote ambayo mtakubaliana.Jiulize,katika kile unachotaka  kukifanya,nani anaweza kuwa msaada kwa namna moja ama nyingine.Andika orodha na kisha jiulize wanaweza kuwa msaada katika jambo gani.UKishajiridhisha,basi bila kuogopa chochote,chukua hatua na uwaendee ama uwasiliane nao.Utashangaa ukichukua hatua ya ujasiri watakukubalia ombi lako na utaanza kuiishi ndoto yako.

Jambo la tatu na muhimu sana kuhusiana na mafanikio ya biashara yake ni kuwa alikuwa tayari kufanya kwa muda kidogo kabla hajaanza kutengeneza faida kubwa.Hii ni hatua ambayo lazima kila mmoja wetu ambaye anataka kufanikiwa katika ndoto yake lazima aipitie.Kuna wakati itabidi ukubali kufanya mambo aidha kwa faida ndogo ama hata kwa hasara,sio kwa sababu unapenda,la hasha bali kwa sababu inabidi ujenge jina kwa wateja wako na wakati huohuo unajenga uzoefu wa kutosha katika kile unachokifanya kwa wakati huo.Usiwe mtu ambaye kila wakati unapoanza kufanya jambo basi kinachokusukuma ni faida tu,hapana-Uwe tayari kwa muda fulani kujenga msingi imara kwa kile unachokifanya kwa kuwa tayari kupata faida ndogo ama kutopata faida kabisa lakini ukitumia muda huo kujenga jina lako na kupata uzoefu unaouhitaji.

Sina shaka kuwa kwa chochote ambacho unachokifanya kwa wakati huu,utatumia kanuni kama alizozitumia lufefe katika kufanikisha ndoto yake,na wewe utakuwa mmoja wa watu ambao siku si nyingi utafanikiwa kwa kiwango cha juu sana katika maisha yako.
Kumbuka kuwa ndoto yako Inawezekana.Kama ujumbe huu umekuwa na msaada kwako,unaweza kuutuma kwa wengine ili nao pia waweze kujifunza.

Endelea kutembelea www.JoelNanauka.com ili kujifunza zaidi.
See You At The Top.
©JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website