Navigate / search

Jinsi Mafanikio Yako Yanavyohusiana na Uwezo Wako Wa Kusamehe

images

Katika kuhusiana na watu mbalimbali katika maisha yetu ya kila siku huwa mara moja au zaidi tunajikuta tuko katika mtego wa kukosewa na watu katika mambo mbalimbali.Kati ya changamoto kubwa unayoweza kukutana nayo ni uwezo wako wa kusamehe waliokukosea.Kuna watu wameshikilia watu waliowakosea mioyoni mwao kwa miaka mingi sasa na maumivu ya makosa waliyofanyiwa yanakua mapya kila siku.Cha muhimu ni kutambua kuwa kuna mahusiano makubwa sana kati ya uwezo wako wa kusamehe na mafanikio yako.

Ni rahisi sana kudhani kuwa umesamehe hadi pale aliyekukosea atakapokutana na wewe au utakapokutana na mtu anamzungumzia,hisia utakazokuwa nazo ndizo zitakujulisha kuwa umemsamehe kwelikweli ama la.Kuna watu wamekosewa na wazazi wao,pengine walikanwa ama walifukuzwa;kuna watu wamekosewa na wenzi wao kwa mambo makubwa yasiyoelezeka,kuna watu wamekosewa na wafanyakazi wenzao kwa mambo yaliyopelekea maisha yao kuharibika,kuna watu wamekosewa na mabosi wao n.k

Ukweli ni kuwa kusamehe kunakuwa kugumu zaidi pale kosa linapofanywa na mtu wa karibu yetu zaidi na yule ambaye hatukumtarajia kabisa.Ila swali ni kwamba,je utaendelea kushikilia maumivu ya kutokusamehe hadi lini?Ukweli ni kwamba uchungu wa kutomsamehe mtu hufanya furaha yako ipungue bila kujua na hukusababisha uwa na reactions za hasira zisizo na sababu ambazo zitawafukuza watu wengi kutoka kwenye maisha yako na kukukosesha fursa muhimu maishani.Kuna mambo kadhaa unatakiwa kuyafahamu kuhusu kusamehe:

Moja ni kuwa kusamehe ni kwa faida yako zaidi kuliko ya wale waliokukosea.Kuna watu wanadhani kutomsamehe aliyewakosea ni kumuadhibu bali ukweli ni kuwa tafiti za kisaikolojia huonyesha kuwa wasiosamehe wanateseka zaidi kuliko wasiosamehewa kwa sababu wakati wewe unasikia hasira na maumivu mwenzako hajali na alishasahau kilichotokea.Kanuni ni kuwa Usisubiri waombe msamaha,amua kuwasamehe kwa faida yako mwenyewe.Siku ukiamua kufanya hivyo utagundua umejitoa katika jela ambayo ulijifungia kwa muda mrefu.Ndio maana Lewis B.smedes alisema” To forgive is to set a prisoner free and discover that the prisoner was you” yaani kusamehe ni kumuweka huru mfungwa na utagundua mfungwa huyo alikuwa ni wewe.Wakati mwingine ili ujiweke huru kabisa utalazimika kumtaarifu aliyekukosea kwa kukutanana naye,kumpigia simu au kumwandikia ujumbe wa sms na kumwambia “nimekusamehe”..Ukifanya hivyo utashangaa utakavyojisikia na mambo yatakavyoanza kubadilika maishani mwako.

Pili ni kuwa kila unapoamua kusamehe Unajipa fursa ya kuanza upya,.Duniani huwa tunakutana na changamoto za kila wakati,na changamoto hizi wakati mwingine hutusababisha tuone kama vile maisha hayawezi kuendelea mbele tena.Kati ya vitu huwafanya watu wasisogee hatua ni pale wanapoapa kuwa hawawezi kumsamehe mtu Fulani.Kila wakati ukikutana nao wanamsema vibaya mtu huyo na kumlalamikia,ni kama wanataka kila mtu amchukie.Watu wengi wamekwama katika maisha yao kwa sababu wameshikilia maumivu ya nyuma na wameshindwa kujipa nafasi ya kuanza upya.Amua leo kuwa hautaendelea kukaa katika maumivu ya kutokusamehe waliokukosea-Amini kwamba unayo fursa ya kuanza upya na ukafanikiwa katika biashara,kazi yako,mahusiano ama masomo yako.Amua kuanza upya leo.

Jambo la tatu ni kufikiri juu ya maisha yako mwenyewe.Wakati mwingine tunaishi kama vile hatujawahi kukosea.Hivi ni mara ngapi umefanya vitu vibaya sana na umesamehewa?Je,unegependa ukikosea tena usisamehewe na wengine?.Kuna kanuni ya ajabu sana maishani inayoonyesha kuwa kadiri unavyokuwa mgumu kusamehe wengine basi na wewe kuna siku utafanya jambo na utatafuta msamaha hadi kwa machozi lakini hautasamehewa.Kusamehe wengine bila masharti ni kujifungulia mlango wa kusamehewa mbeleni utakapokosea.Usimfanye aliyekukosea akose raha kwa kila wakati kumkumbushia aliyoyakosea.Ukishaamua kusamehe mweke huru na usimkumbushekumbushe kila wakati makaosa yake.Kusamehe ni kuachilia moja kwa moja.
Kama unapenda kusamehewa,uwe tayari kuwasamehe wengine pia.

Watu ambao wanasamehe wengine ni watu wenye furaha na huwa na nguvu za ziada kusonga mbele haraka kila magumu yanapowatokea.Kusamehe sio hisia,bali ni maamuzi unayotakiwa kuyafanya kuanzia leo bila kusita.Kumbuka kuwa,kuna mahusiano ya karibu sana kati ya mafanikio yako na uwezo wako wa kusamehe.kama unahitaji msaada zaidi,tafadhali tuwasiliane.
Endelea kutembelea ukurasa wangu wa facebook ili Kujifunza Zaidi.

See You At the Top

Comments

Justina Msidada
Reply

Barikiwa Mtumishi kwa somo hili, ni kweli kukosewa na mtu wa karibu zaid huwa inakuwa ngumu kwa kiasi kusamehe, lakini ukiamua kuachia inawezekana

Leave a comment

name*

email* (not published)

website