Navigate / search

Jinsi Kukosolewa Kunavyoweza Kukusaidia Kufanikiwa Kwa Haraka.

mobbing

Jack Rosenblum aliwahi kusema “If one person tells you you are a horse,he is crazy.If three people tell you,you are a horse there’s a conspiracy afoot. If ten people tell you you’re a horse,it’s time to buy a saddle”(Kama mtu mmoja akikuambia wewe ni farasi atakuwa amechanganyikiwa,watu watatu wakikuambia wewe ni farasi itakuwa ni mbinu wamepanga kukufanyia,ikiwa watu kumi watakuambia wewe ni farasi basi hapo kanunue vile vifaa vinavyotumika kuendeshea farasi kwa sababu utakuwa kweli ni farasi).

Ili uweze kufikia kilele cha ndoto yako na uyafikie mafanikio yako ni lazima uwe na uwezo na utayari wa kukubali kupokea mrejesho(feedback) toka kwa watu wengine.
Mara nyingi sana kama binadamu huwa tunapenda sana kuambiwa vitu ambavyo tungependa kuvisikia na ambavyo vinatufurahisha.Labda tuseme umetoka kuongea mbele ya watu,basi pale watu watakapokuja na kuanza kukuambia “aisee umeonge vizuri sana”-Hao ndio watu utakaowapenda zaidi.Na akitokea mtu akakuambia “Mambo uliyokuwa unaongea yalikuwa mazuri sana ila ulionekana kama hauongei kwa hamasa,wakati mwingine jitahidi katika hilo”-Hata kama hatutaonyesha palepale lakini mara nyingi ndani yetu hatupendi kusikia hivyo.

Katika kuelekea mafanikio kuna aina mbili za mrejesho ambazo zote ni za muhimu sana kwa ajili ya mafanikio yako.Moja ni mrejesho chanya(positive feedback)-Huu unaelezea nguvu tulizonazo na maeneo ambayo kwa sasa tunafanya vizuri zaidi.Mrejesho chanya unakupa hamasa ya kuendelea kufanya mambo,unakupa ujasiri na pia unakusaidia kujua maeneo gani unatakiwa kuendelea kuyafanya.Watu wengi wako tayari kutoa aina hii ya mrejesho na watu wengi wako tayari kupokea aina hii ya mrejesho.

Aina ya pili ya mrejesho ni mrejesho hasi(negative feedback).Huu ni mrejesho unaoeleza wapi tumekosea,hatujafanya vizuri na pia unaonyesha madhaifu yetu.Watu wengi hatupendi kupata mrejesho wa namna hii na watu wengi pia hawapendi kutoa mrejesho huu.Inawezekana hata wewe kuna watu wako wa karibu huwa wanakosea mara nyingi tu ila unakosa ujasiri wa kuwakosoa kwa sababu unaogopa watachukia.

Ni mara ngapi umekaa sehemu na ukasikia watu wanasema-“Nilijua tu,kwa jinsi alivyokuwa anaendelea lazima angefikia hapo tu,sishangai”.Ila watu hao hao ukiwauliza kama walishawahi kumwambia mtu huyo utashangaa kujua kwamba hawajawahi kumwambia hata kama kila siku walikuwa naye.Ili ufanikiwe ni lazime ukubali kukosolewa hapa na pale ili uongeze ubora wako.Na kwa sababu watu wengi huwa hawako tayari kukosoa,itahitajika mara nyingine uulize wewe mwenyewe na kuwapa fursa ya kufanya hivyo kwa uhuru zaidi ili wasiogope kuwa wakikukosoa basi utakasirika ama watakuudhi.

Kwa mfano umemaliza kufanya kitu au uko kwenye ofisi moja na mtu au ni rafiki yako;kila akikusifia kuhusu jambo fulani unaweza kumwambia-“Ahsante sana,ila unafikiri nifanye nini ili niweze kuwa bora zaidi katika hili?,ni kitu gani natakiwa kukiboresha?”.Ukiwa tayari kuuliza swali hili utashangaa jinsi utakavyopata mambo mengi ya kukusaidia.

Hata hivyo kulingana  na Jack Rosenblum ni kuwa mara kadhaa tunaweza kukutana na watu zaidi ya mmoja wanatuambia jambo hilohilo kuhusu maisha yetu.Kwa mfano,kama kuna watu kadhaa wanakuambia una kiburi,usiseme tu hawakupendi hebu jichunguze,kama kuna watu kadhaa wanakuambia unapenda kujidekeza,hebu lifanyie kazi,kama kuna watu kadhaa wameshawahi kuwa unakasirika haraka usipuuzie hilo lifanyie kazi.Watu wengi sana huwa wanakwama kuwa bora zaidi katika maisha yao wanapopata mrejesho wasioupenda(negative feedback) kwa sababu kuu 3:

Moja ni kuwa huwa wakikosolewa wanakata tamaa kabisa.Kuna watu baada ya kukoselewa huwa hawachukui somo la kujifunza ili wawe bora zaidi badala yake wanakatishwa tamaa na kile walichoambiwa.Kama ni waimbaji wakiambiwa leo uliimba nje ya sauti inayotakiwa basi kesho wanaacha kuimba kwaya kabisa.Ili ufanikiwe ni lazima ukatae kukatishwa tamaa na mrejesho hasi.Kama bosi wako amekuambia kuna kazi hukufanya vizuri usikate tamaa na kutaka kuacha kazi,jiulize namna gani unaweza kuwa bora zaidi.

Pili ni kuwa kuna watu ambao wanachukia watu ambao huwa wanawapa mrejesho hasi.Historia zinaonyesha kuwa viongozi wengi ambao hawana watu wa kuwaambia wanapofanya vibaya ama kwa kuwaogopa ama kwa hofu ya kuwa wataharibu mahusiano yao huwa wanaishia kuboronga.Katika maisha ni hivyo hivyo,katika watu wa karibu yako lazima wawepo watu ambao wanaweza kuwa na ujasiri na uwezo wa kukuambia ulipokosea na usiwachukie.Kama umezungukwa na watu wanaokusifia tu kila siku basi ujue utakuwa mtu wa kurudia makosa mengi sana na utachelewesha safari yako ya mafanikio.Siku zote katika maisha yako,usijiruhusu kumchukia anayekurekebisha badala yake chukua funzo analokupa na lifanyie kazi.Najua kuwa kuna watu ambao ni wakosoaji kila wakati,hata ukifanya zuri huwa hawalioni-Siwazungumzii watu wa namna hii,nawazungumzia wale ambao huwa wanakukosoa ili uweze kuwa bora zaidi katika kile uanchofanya.

Kila wakati utakapoonyesha kuwa unamchukia anayekupa mrejesho hasi basi hatafanya hivyo tena na matokeo yake utabakia kuwa mtu ambaye huwa unakosea kila siku.

Tatu ni kupuuzia unayoambiwa.Kuna watu wamepata bahati ya kuwa na watu wanaowapenda na kila wakati huwa wanawapa mrejesho kuhusiana na maeneo ya maisha yao wanayoweza kuyaboresha zaidi lakini huwa hawazingatii kabisa,wanayapuuza.Kila wakati unapopuuza mrejesho unaokutaka uboreshe eneo fulani la maisha yako ni kuwa unajinyima fursa ya kufanya vizuri zaidi wakati unaofuata.

Kila wakati ukisikia mtu amekupa mrejesho fulani katika maisha yako kuanzia leo,upokee na uwekee mkakati wa namna ya kuwa bora zaidi wakati unaofuata.
Kumbuka kuwa ndoto yako Inawezekana,

Endelea kutembelea
 www.JoelNanauka.Com
See You At The Top.
©JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website