Navigate / search

Jina Tanzania lilipatikanaje?

IMG-20150426-WA0059

 Mohamed Iqbal Dar ni mtanzania mwenye asili ya kiasia. Mzaliwa wa Tabora ambaye kwa sasa anaishi katika jiji la Burmingham nchini Uingereza.Huyu ndiye aliyebuni jina TANZANIA ambalo ndilo linatumika hadi leo likimaanisha Jamuhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Ni bahati mbaya historia kumuhusu mtu huyu haitajwi na wala kufundishwa mahala popote lakini ukweli unabaki kuwa Mohamed Iqbal Dar ndiye shujaa mbunifu wa jina TANZANIA ambalo leo kama nchi limetupa utambulisho dunia nzima.

Anasimulia kisa chake mpaka kubuni jina TANZANIA.

Akiwa na umri wa miaka 18 mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Agha Khan H. H Secondary School ya mjini Morogoro, siku moja akiwa katika mapumziko ya muhula wa masomo yake, alikwenda Maktaba Kuu ya Taifa jijini Dar es Salaam ambako alikuwa na tabia ya kwenda kujisomea nyakati za likizo.

Alipofika hapo aliamua kusoma gazeti la Serikali la Tanganyika Standard ambalo kwa sasa linaitwa DAILY NEWS ambako alikuta tangazo la shindano la kubuni jina litakalotumika kuiita Jamuhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar jina lililoonekana kuwa refu sana.

Mohamed ambaye nimuumini wa madhheb ya Ahmadiyat Muslim Jamaat alichukua karatasi na kuandika;
– “Kwa Jina la Mwenyezi Mungu”

– “Tanganyika”

– “Zanzibar”

– “Mohamed Iqbal Dar”

Kisha akamuomba Mwenyezi Mungu amsaidie kupata jina zuri.Ndipo akaandika;

TAN (kwa maana Tanganyika)
ZAN (kwa maana Zanzibar)
akapata neno TANZAN akaamua kumalizia IA baada ya kufikiria majina mengi ya nchi yanavyoishia na IA(Somal-ia,Ethiopia,Zamb-ia,Niger-ia,Alger-ia etc) na kupata jina TANZANIA.

Akalituma katika Wizara iliyoagiza shindano hilo na kusubiri matokeo.

Hakujua lolote mpaka siku aliporudi nyumbani kwao akapokelewa na baba yake mzazi ambaye alikuwa Daktari wa hospitali na kumuonesha barua kutoka Serikalini ikimpongeza kuwa jina alililobuni TANZANIA ndio limepitishwa kutumika badala ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Hivyo ndivyo jina TANZANIA lilivyobuniwa na huyo ndie Mohamed Iqbal Dar mbunifu wa jina TANZANIA.

Imenakiliwa toka makala ya gazetini

Leave a comment

name*

email* (not published)

website