Navigate / search

Huyu ndiye Sokoine, tutampata lini mwingine?

“Ole wake kiongozi mzembe na asiye na nidhamu nitakayemkuta: Kiongozi wa siasa hana usalama wa aina yoyote. Usalama wake ni kudra ya Mungu na Wananchi peke yake. Viongozi wazembe na wabadhirifu wahesabu siku zao. Labda tusiwajue. Hawa hatuna sababu ya kuwapa imani, kuwa tutawalinda kama vitendo vyao viovu”
Edward Moringe Sokoine, 26 Machi 1983

April 12 mwaka 1984 ni siku ambayo Tanzania ilimpoteza kati ya viongozi wake mahiri kuwahi kutokea katika kizazi cha kwanza baada ya uhuru.Sauti iliyojaa huzuni ya mwalimu Nyerere ilisikika ikitangaza pigo kubwa ambalo nchi yetu ilikuwa imelipata,kupitia radio Tanzania(RTD) Mwalimu alisema kwa huzuni:

“NDUGU wananchi, leo saa saba mchana; ndugu yetu na kijana wetu. Ndugu Edward Moringe Sokoine; alipokuwa safarini kutoka Dodoma kuja Dar es Salaam, gari yake ilipata ajali. Amefariki dunia.”

Hayati Sokoine alipata ajali hiyo baada ya gari lake kugongana uso kwa uso na Toyota Land Cruiser maeneo ya Dakawa Morogoro.Mengi sana yamesemwa kuhusiana na ajali hiyo na baadhi ya watu walisadiki kusema kuwa ilipangwa na waliokuwa wanahofia kasi yake ya kupambana na wala rushwa nchini lakini kwa kuwa hakuna ushahidi wowote si vyema kulizungumzia hili kwa undani.

Edward Moringe Sokoine alizaliwa tarehe 1 Agosti 1938 Monduli Mkoani Arusha Tanzania,  alipata elimu ya msingi na sekondari katika miji ya Monduli na Umbwe toka mwaka 1948 hadi 1958. Mwaka 1961 alijiunga na chama cha TANU baadaye alichukua masomo ya Uongozi nchini Ujerumani 1962 hadi mwaka 1963. Aliporudi kutoka Ujerumani alikuwa afisa Mtendaji wa Wilaya ya Masai.Baadaye alichaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo la Masai. Mwaka 1967 alikuwa naibu waziri wa mawasiliano, usafiri na kazi. Mwaka 1975 alichaguliwa kwenye Bunge tena wakati huu kupitia Monduli. Miaka miwili baadaye akawa mjumbe wa Kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), 1977 alianza muhula wa kwanza ofisini akiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania tarehe 13 Februari 1977 hadi tarehe 7 Novemba1980.Akawa Waziri mkuu tena toka tarehe 24 February hadi tarehe 12 Aprili 1984.

Yako mambo mengi yanayomfanya hayati Sokoine akumbukwe na watanzania hasa wanyonge.Nakumbuka simulizi niliyopewa ya kisa cha mama mmoja aliyelia sana baada ya kifo cha sokoine kutangazwa kwa kiwango ambacho watu walifikiri kuwa ni ndugu yake.Alipoulizwa alijibu huku akilia..“Nani atatutetea sisi wanyonge?”

Sokoine alikuwa ni mchapa kazi,watu waliokuwa wanafanya kazi naye walisema kuwa alikuwa ni mtu asiyechoka katika majukumu yake.Alikuwa ni mtu anayefuatilia kazi alizoagiza kipengele kwa kipengele.Hakuwa mtu wa kupenda starehe kama ilivyo baadhi ya viongozi wa leo.Alihimiza kutumia rasilimali za umma kwa faida ya wananchi hasa wanyonge.Na hii ndio sababu ilimfanya asitake kusafiri kwa ndege kutoka Dodoma hadi Dar Es Salaam,badala yake alitaka kusafiri kwa gari kwa kutoa sababu kuwa anataka kukagua miradi ya maendeleo atakapokuwa anapita katika maeneo ya njiani.Hii ilisababishwa wakandarasi wafanye kazi kwa viwago vya juu kwani walijua siku usiyodhani Sokoine anaweza kutokea.

Hayati Sokoine alihimiza serikali kuhamia Dodoma kama ilivyokuwa imependekezwa na serikali na Chama na kuundiwa tume maalumu(CDA) ya kuendeleza mji huo kwa ajili ya kuhamishia makao ya serikali yetu.Sababu ilikuw mji wa Dodoma uko katikati ya nchi itakuwa rahisi kwa wananchi kufuata huduma huko na si lazima tujaze kila ofisi Dar Es Salaam.Hadi leo miaka 20 ya kuenziwa kwake viongozi wetu wamen’gan’gania Dar Es Salaam na huku shuleni watoto wakifundishwa mji mkuu ni Dodoma wakati kila kitu kinafanyika Dar Es Salaam.Natamani tunapomuenzi Sokoine katika mwaka 2014,aidha Serikali itangaze kuhamia Dodoma ama itangaze rasmi kuwa Dodoma si mji mkuu bali ni Dar Es Salaam,kuliko kuendele kujidanganya.

Hakuna anayeweza kusahau huruma yake kwa wanyonge.Kuna wakati alitembelea Kibaha katika ziara zake za kukagua miradi.Baada ya Ziara ya masaa kadhaa kama ilivyo ada alipelekwa kwenye ukumbi wa kula chakula huku njiani kukiwa kumejaa wanafunzi waliojipanga kumsubiri.Alipofika kwenye ukumbi wa chakula swali lake la kwanza kwa wenyeji wake lilikuwa-“wanafunzi hawa wamenisubiri tangu saa ngapi” viongozi kwa kufikiri watasifiwa wakasema tangu saa tatu asubuhi.Ndipo Sokoine akasema chakula chote mlichoniandadalia na mssafara wangu wapewe hawa na mimi na wenzangu tutarudi Dar Es Salaam.Kiongozi gani leo atawaza juu ya walimu wanaopata mishahara midogo na kufanya kazi katika maeneo magumu?Si ndio hawa walituambi ndege ya Rais Lazima inunuliwe hata kama tutakula nyasi?.Tunahitaji viongozi kama sokoine wanaoguswa na mateso ya wananchi na kuwa tayari kujinyima ili wananchi waondokane na mateso yao ya kila siku.

Hayati Sokoine kama alivyokuwa Nyerere,alikataa kabisa kuitwa mheshimiwa katika mazingira yoyote,alitaka aitwe ndugu.Alitoa sababu rahisi sana ya kuwa kama kuna “Mheshimiwa” basi pia lazima kuna “mdharauliwa”.Siku hizi ni tofauti,ukitaka ufukuzwe kazi kirahisi acha kumuita kiongozi wa kisiasa mheshimiwa.Wanataka kujenga matabaka kwa maneno na kwa vitendo pia.

Hayati Sokoine alikuwa ni jasiri wa kuchukua hatua kali kwa wote waliokuwa wabadhirifu wa mali za Umma bila kujali vyeo vyao au ukoo wanaotokea.Kila mtu anaikumbuka operesheni Tokomeza wahujumu uchumi,iliyolenga kuwafuatilia wote waliokuwa wanajipatia mali kwa njia zisizo halali.Watu walijikuta wakifukia pesa chini ya ardhi na wakimwaga sukari na bidhaa zingine baharini,mitoni na kwenye maziwa.Nakumbuka kisa nilichosimuliwa cha watu waliotupa pesa kwenye makaburi ya kisutu na watu kuogopa kuziokota kwa kuhofia kuwa ni pesa za “Majini”.Alikuwa si mla Rushwa hivyo hakuona hofu kuwakemea wala rushwa.Hivi leo inachekesha kusikia eti walioiba pesa Benki kuu wanaombwa warudishe,tena wakizirudisha hawachukuliwi hatua yoyote.Hakuruhusu watu wajikwapulie pesa za umma na kuendelea “kutesa” mtaani.

Nyerere alilazimika kukatisha mapumziko yake Butiama baada ya ndugu wa karibu wa Paul Rupia Kukamatwa katika sekeseke la wahujumu uchumi.Rupia alikuwa ni mtu mwenye heshima katika nchi na katika chama,alichangia theluthi ya pesa zilizompeleka Nyerere UN.Hii yote haikumzia Sokoine kuchukua hatua eti kwa sababu yuko karibu na Mkuu wa Nch,alitaka uwajibikaji kwa kila mtu bila kujali ni nani na ana cheo gani.

Bado namtafuta Sokoine atakayewawajibisha watendaji wa serikali wanaofuja pesa za umma na kutuingiza katika mikataba inayotutia hasara.

Bado namtafuta Sokoine atakayekuwa na ujasiri wa kukemea rushwa bila kujali cheo cha mtu wala familia anayotoka.

Bado namtafuta Sokoine wa kizazi chetu atakayekuwa yuko tayari kukaa na njaa ili wanyonge anaowaongoza waweze kula.

Yuko wapi Sokoine aliye msafi asiyeogopa kukemea uchafu wa aina yoyote ile.

Kizazi chetu kina deni cha kumpata Sokoine wake…swali ni kuwa TUTAMPATA LINI???

Leave a comment

name*

email* (not published)

website