Navigate / search

Hotuba yangu kwa Vijana wa Tanzania iliyokuwa niitoe Chuo Kikuu cha Dar 06/june/2015

k1

Jumamosi iliyopita nilialikwa niwe mnenaji pamoja na David Kafulila chuo kikuu cha Dar es Salaam katika Kongamano la Uongozi la vijana la mwka 2015.Bahati mbaya sana siku moja kabla;tukio lilighairishwa kwa maelezo toka kwa waandalizi kuwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wao.Watu wengi walikusudia kuja kusikiliza na wengine hawakupata taarifa za kughairishwa na walijitokeza ukumbini.Nimeona ni vyema niwashirikishe hotuba hiyo kwa leo:

Ilipofika miaka ya 1970 migomo ya wanafunzi ilianza kushamiri nchini Afrika migomo iliyoongozwa na chama cha wanafunzi(SASO-South African Student Oganisation) kilichokuwa kimejitoa toka kwenye chama cha wanafunzi kilichokuwa kinapendelea maslahi ya weupe Zaidi cha National Union of South African Students.Tarehe 16 June,1968 kamati ya wanafunzi wa shule za Soweto iiandaa maandamano yaliyosababisha vuguvugu la mabadiliko lilipolekea wananchi wengine wengi kuanza kukataa ukandamizaji kwa vitendo.

Maandamano yaliyoonekana ni ya wanafunzi wenye umri mdogo na wasio na uzoefu wowote wa kisiasa,ndiyo yalikuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya kifikra na kusababisha kila mtu awe jasiri katika kupinga unyonyaji na ukandamizaji wa watu weusi.

Tukio hili linanikumbusha maneno ya Barack Obama wakati anagombea Urais wa Marekani pale aliposema—“In the face of impossible odds, people who love this country can change it.”.Yes,Bila kujali kuwa hali iliyopo inakatisha tamaa ama kuonyesha haiwezekani kubadilika;watu wanaopenda Tanzania wanaweza kuleta Mabadiliko.Na tuko hapa Leo kuyaleta mabadiliko hayo kwa sababu tunaipenda nchi Yetu.

Kama vile wanafunzi wadogo wa Soweto walivyoanzisha vuguvugu la mabadiliko lililoleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa nchi,ndivyo itakavyokuwa kwa Tanzania baada ya sisi wote kutoka katika Ukumbi huu hivi leo.

Katika dunia ya watu bilioni 7,kundi la vijana chini ya miaka 30 wanafikia bilioni 3.5 yaani 50% ya idadi ya watu wote duniani.Hata hivyo changamoto ni kubwa Zaidi katika nchi zilizoendelea ambapo idadi ya vijana imefikia kiwango cha asilimia 89 ya wananchi wote.Tanzania ni kati ya nchi 10 duniani zenye idadi kubwa ya vijana na mji wa Dar es salaam umeingia katika rekodi hivi karibuni kwa kuwa na idadi kubwa ya vijana duniani.

Katika bara la Afrika Zaidi ya 60% ni vijana chini ya umri wa miaka 25,hata hivyo nusu ya vijana wote wa afrika bado hawajui kusoma na kuandika.

Uwingi huu wa vijana umewafanya vijana wengi si tuu kukosa kazi(unemployment) Ukosefu huu wa ajira umewafanya vijana wengi kufanya kazi za kiwango cha chini ukilinganisha na uwezo wao(Underemployed) na inakisiwa Zaidi ya 70% ya vijana Afrika wananishi chini ya dola mbili kwa siku takribani 20% ya vijana chini ya jangwa la sahara hawana ajira kabisa.Changamoto hii inaelekea kuongezeka mara mbili Zaidi itakapofika mwaka 2045 kwa kuzingatia kuwa katika bara la Afrika takribani vijana milioni 10-12 wanatoka vyuoni na kuingia mtaani kutafuta ajira.

Wakati hayo yanaendelea ,nchi za Afrika zimeendelea kushangilia ukuaji wa uchumi wao kwenye makaratasi na uvumbuzi wa rasilimali za madini,mafuta na gesi.Takwimu za ukuaji wa kiuchumi zinazotolewa na benki ya dunia na mashirika ya Kimataifa zimeendelea kukatisha tamaa kwani wakati uchumi wa afrika unasema kuimarika kwa takribani ukuaji wa 7% bado hali za vijana zimeendelea kudhoofika kwani kiuhalisia uchumi uliokua ni katika akaunti za wanasiasa,mifuko ya wafanyakazi wabadhirifu wa umma na tabaka la wachache lililojipa mamlaka juu ya rasilimali zetu.

Nchini Nigeria inaonyesha kuwa 98% ya mapato yanayotokana na mafuta inaishia kwa 2% ya wanasiasa na wafanyabiashara nchini Nigeria.Ni vyema kukumbuka kuwa,Kila wakati vijana wanapokuja pamoja katika kujaribu kuleta mabadiliko katika jamii na mataifa yao wengi wanaanza kuwabeza ama kwa kuwakosoa hawana uzoefu ama wanachojaribu kufanya ni kigumu na hawataweza kufanikiwa kabisa.Ingawa ujana si kigezo pekee kinachotosha kumfanya mtu alete mabadiliko katika nchi yake,pia si sahihi kudhani kuwa mtu atashindwa kuleta mabadiliko kwa sababu ni kijana.

Bado najiuliza,hivi ni kweli hatuna tena Vijana wanaoweza kuleta mabadiliko katika Afrika?

Ni Kweli kuwa hatuna vijana wanaoweza kuleta mabadiliko katika Nchi yetu ya Tanzania?

Ni kweli kuwa tumeamua kukata tamaa na kuacha mambo yanaenda mrama?

Kila siku najiuliza kiko wapi kizazi kipya cha Afrika kitakacholeta Mabadiliko ya kifikra na Kiuchumi katika Taifa Letu.Wako wapi Vijana hawa?Wako Wapi Mashujaa wa kiazi chetu?.

Wakati Steven Bikko anaanza harakati za kuchochea waafrika kujitambua miaka ya 60 baada ya viongozi wa ANC na Pan Africanist congress kufungwa, wengi walidharau na waliona ni hekaheka za ujana.Baada ya muda mchache kijana huyu aliyekuwa na miak 28 wakati huo alikuwa tayari ni tishio kwa utawala dhalimu hadi kufikia uamuzi wa kupitisha sharia ya kumzuia kutoongea na mtu Zaidi ya mmoja ama watu kunukuu maneno yake.Ingawa aliuawawa baada ya muda mfupi,hakika mabadiliko aliyokuwa ameyaleta bado yanadumu na maneno yake yametimia pale aliposema-“It is better to die for an idea that will live, than to live for an idea that will die””Ni bora kufa kwa mawazo yatakayoishi kuliko kuishi kwa mawazo yatakayokufa”-

Wako wapi akina steven Bikko wa leo katika nchi yetu?Vijana wanaoamini kuwa wajibu wao wa kwanza ni kuwasaidia wanyonge walioonewa na kupuuzwa.Wako wapi wasomi walio tayari kuwa watetezi wa maskini wanaonyan’ganywa ardhi na kuporwa rasilimali zao.
Steven Bikko alikuwa ni mtu anayejitegemea kimawazo katika kuendesha harakati zake;hakukubali tamaa ya pesa na tamaa ya vyeo imfanye asaliti kizazi chake na kuwa mfuasi wa wanasiasa wasioamini katika utu.Hii ndio aina ya vijana tunayohiitaji katika Taifa letu.

Namkumbuka Sekou Toure alivyoonyesha ujasiri wake dhidi ya mamlaka ya wakoloni wa wafaransa na hata walipoamua kumkomoa kwa kubomoa kila kitu walichokuwa wamejenga kabla ya uhuru na hata kuvunja taa za Ikulu.Nguvu ya ujana na uzalendo wake ilimfanya asimame tena na kulitetea Taifa lake.

Leo naikumbuka Damu ya Kijana Mzalendo,Patrice Lumumba;Patrice Lumumba ambaye hakuwa tayari kuwa kibaraka wa wabelgiji na akakubali kifo badala ya kukandamiza wakongo wenzake,hii ndio aina ya vijana tunawatafuta.Katika changamoto zote ndoto yake haikuwa kuhusu kuitajirisha familia yake bali kulitetea taifa lake hata akaandika barua wakati anakaribia kuuwawa na kusema;”Siku itakuja ambapo wananchi wa Kongo wataandika historia yao wenyewe,nami niko tayari kufa kifahari kwa ajili ya nchi yangu kuliko kukubali ukandamizi wa nchi za magharibi”Leo hatutawaliwi kwa bendera lakini nani anabisha kuwa tunatawaliwa kifikra.Wako wapi vijana watakaosema badala ya kuchukua madini yetu na kutuachia mashimo huku wakituletea vyandarua,watadai uwazi Zaidi katika mikataba ya rasilimali zetu?Wako wapi vijana watakaosema maneno haya bila woga.

Wazalendo kama Thomas sankara ambao kwa ndani ya miaka 4 aliifanya Burkina Faso ijitegemee kiuchumi na chakula bila msaada wa nchi za nje.Leo wako viongozi wanaosema miaka waliyokaa madarakani ni michache tuwape miaka Zaidi,na vijana tumekaa kimya.Ni vijana gani leo wanaweza kuwa viongozi wakaamini katika kujitegemea na kuchukia kuwa ombaomba katika nchi za watu?.

Vijana kama akina Thomas Sankara ambao waliamua kukata mishahara ya wanasiasa nusu,kuzuia kuendesha magari ya kifahari na hata kuzuia kusafiri kwa viongozi wa serikali katika daraja la Kwanza kwenye ndege.Wako wapi?

Tunapozungumzia Rushwa na Ufisadi tunatakiwa kumaanisha.Tunatakiwa kuchukia kama jerry Rawlings ambaye akiwa na miaka 32 alishughulikia mafisadi na wabadhirifu nchini Ghana katika kampeni ya “Safisha nyumba” ambapo hakuna aliyeachwa kwa sababu ama ya cheo chake serikalini ama jeshini.Ni mara ngapi tumesikia vijana wakisema ukipata nafasi ya kula kula haswaa kwa sababu usipokula wenzako watakula.

Hawa ndio vijana tunaotaka waikomboe nchi hii;je wataweza?Ni kama vile wengi wanachukia rushwa kwa sababu hawajapata nafasi ya kula rushwa lakini wakiipata wanaweza kuwa wabaya kuliko walioko madarakani.

Je,tunaweza kuwapata akina Jerry Rawlings leo ?ambao hata kama hawataua lakini watachukua hatua zisizo na shaka kwa kila mbadhirifu.

Ingawa ni ukweli kuwa hatukupigana vita ili kupata uhuru wa nchi hii lakini ni lazima tujue kuwa kuna watu walijitoa muhanga kupitia muda wao,mali zao na wengine uhai wao ili kutufanya tuwe huru kisiasa.Na ningependa kusema kuwa yako mambo matatu ambayo tunayweza kuyanya ili kuleta mabadiliko katika nchi yetu:

1)Ni Lazima Vijana Tuongoze njia
Ni lazima tutambue kuwa hakuna atakayekuja kuibadilisha nchi hii isipokuwa vijana wa nchi hii.Tukikaa pembeni,yale tunayoyachukia yataendelea kuwepo.Ni lazima tufanye uamuzi LEO,tuamue kufa kishujaa ama tuishi kitumwa.
Nayakumbuka maneno Matatu ya Martin Luther King Junior:SASA,HAPA na SEKTA ZOTE

Neno la Kwanza-Tunahitaji kufanya Mabadiliko SASA-Tusikubali kuambiwa tusubiri kesho;Tusikubali kuambiwa tusubiri tukue;Tusikubali tuambiwe tusubiri uchaguzi Ujao:Tufanye mabadiliko SASA.

Neno la Pili-Mabadiliko yanatakiwa kuanzia PALE TULIPO;Wako wanaosema tusubiri tupate ubunge ili tubadilishe nchi yetu;wapo wanaosema tusubiri tuwe matajiri tuweze kusaidia wananchi wenzetu maskini;wapo wanaosema tusubiri tuwe na Phd tulete mabadiliko.HAPANA-Tuanze kuleta mabadiliko pale tulipo na kwa kile tulichonacho.

Neno la Tatu-Tunahitaji Kufanya mabadiliko KILA SEKTA;Kuna watu wanalalama kuwa kila msomi anaenda kwenye siasa,ni kweli kuwa siungi mkono wasomi wote kwenda kwenye siasa lakini pia siungi mkono siasa kuwa dhamana ya mtu yoyote yule bila kuajali uwezo alionao.Ni vizuri wasomi tuenedelee kujenga kutoa mchango wetu katika sekta mbalimbali lakini ukweli ni kwamba kama tutaiacha siasa mikononi mwa wasio na uwezo mchango wetu hautakuwa na maana kabisa.

Naungana na maneno ya Plato aliposema-“One of the penalties for refusing to participate in politics is that you end up being governed by your inferiors.”-(Moja ya adhabu uanyopata kwa kukataa kushiriki kwenye siasa ni kuishia kutawaliwa na watu wasio na uwezo kabisa)-Na matokeo utaishia kulalamika.Si kila mmoja ana wito kwenye siasa,lakini kila mwenye wito kwenye siasa aingie kuleta mabadiliko.Ni hatari kuachia mambo ya siasa yaendeshwe na wanasiasa wasio na uwezo wa kutosha na Zaidi wasio na uzalendo kwa Nchi yetu.

Ni lazima kila asubuhi tukumbuke maneno ya Che GuevaraNi bora kufa ukiwa umesimama,kuliko kuishi kwa karne nzima ukiwa umepiga magoti”
Ni lazima vijana waseme yale wanayoyaamini bila kujali yamefanywa na chama chako ama na chama cha wengine.Kama hatuwezi kutetea wanyonge tukiwa hatuna madaraka tujue fika hatutaweza kufanya hivyo hata tukipewa madaraka.Ni lazima tuanze pale tulipo kwa vile tulivyonavyo.

2)Inatupasa tuamini katika mabadiliko:

Nilipokuwa nahutubia vijana wakati Fulani kuhusu mabadiliko mmoja akanyooosha mkono akasema;Nchi hii haiwezi kubadilika kwani kila mtu ameoza.Nikamwambia si kweli-Wapo wengi ni wazalendo na wanaipeanda nchi hii.Naamini hata hapa wapo kwa sababu katika kila nchi Mungu huacha masalia ya kuleta ukombozi.Samaki mmoja ndani ya kapu akioza wengine wote ndani ya kapu wataoza;ila samaki walioko nje ya kapu watabaki Salama.Naamini hata hapa wako vijana wengi walioko nje la kapu la samaki waliooza.

Ni lazima nikiri kuwa si rahisi kuleta mabadiliko lakini si jambo linaloshindikana.Kila mtu aliamini kuwa hakuna anayeweza kuwashinda makaburu katika siasa kandamizi nchini Afrika Kusini.Lakini kama mandela alivyosema”It always look impossible until it is done”-Siku zote itaonekana haiwezekani hadi utakapoamua kufanya.
Dhambi kubwa ni kukata tamaa maishani-Wakati Orvile na Wilbur wanatengeneza ndege yao kila mmoja aliona ni jambo haliwezani na hata kamati ya kisayansi ikatoa tamko rasmi juu ya kutokuwezekana kwa teknolojia hiyo.Kinyume na matarajio ya wengi Wrights Brothers waliirusha ndege yao ya kwanza 1903.

Wakati wa mabadiliko wengi wasio amini hupenda kuwakatisha tamaa wanaoamini mabadiliko,vijana lazima waamini katika mabadiliko bila kukata tamaa.Habari njema ni kuwa siku mabadiliko yakitokea hata wale wanaoyapinga watashangilia.

3)Tuwe tayari kujitoa kwa ajili ya nchi yetu

Tarehe 5 January,2011 Zaidi ya watu 5,000 waliandamana kwenda kuhudhuria mazishi ya kijana aliyekuwa amefariki baada ya kujichoma moto na kwa mujibu wa madaktari 90% ya mwili wake iliharibika kwa kuungua.Aliamua kujiua mbele ya ofisi za serikali ili kuonyesha hasira zake na jinsi alivyokatishwa tamaa na serikali iliyochukula bidhaa na vifaaa vyake alivyovipata kwa shida baada ya kuhangaika kwa muda mrefu kutafuta kazi.Siku chache zilizofuata kifo cha Mohamed Bouaziz kilisababisha maandamnao makubwa yaliyopelekea Rais wa Tunisia wa wakati huo Zine El Abidine Ben Ali kukimbia nchi.

Hakuna Taifa linalobadiliko bila watu kusacrifice kwa Taifa hilo,hakuna mabadiliko yasiyo na gharama.Na ni lazima kutambua kuwa mtu mmoja kama alivyokuwa Bouaziz anaweza kuwa chanzo cha mabadiliko katika nchi hii.Mtu huyo unaweza kuwa wewe.Usikae kusubiri Mwingine,Tanzania inakusubiri uweze kuibadilisha.
Mwaka 2007 usiku wa manane nilijikuta katikati ya pori kubwa sana lililokuwa na giza totoro,wakati naendelea kushangaa na kutafuta nini cha kufanya nilianza kusikia sauti nyingi kwa mbali ambazo sikuweza kuzitambua mara moja.Katika hali ya hofu,kukiwa na ukimya usio wa kawaida, umande ukinilowesha huku nikiwa peku,mwili ulisisimka,moyo ukaenda mbio,nywele zikanisimama-na ingawa kulikuwa na baridi jasho lilianza kunitoka.
Nikaamua kuchukua hatua kuzifuata kelele zilikokuwa zinatokea;kadiri nilivyosogea ndivyo niilvyoendelea kutambua kuwa kelele zile zilikuwa ni za wanadamu na sio wanyama ama ndege.

Nilipokuwa nimetembea takribani mita 100 nilifika mahali ambapo kelele hizi zilitokea.Ukweli ni kuwa hazikuwa kelele za shangwe bali zilkuwa kelele za kilio na kuomba msaada.
Katika hali ya kupigwa butwaa na hofu nyingi nilijikuta nimesimama mbele ya shimo kubwa lenye watu wa kila aina,wengine walemavu,wengine wanavuja damu,wajawazito nawatoto.

Nilishindwa kujizuia nafsi yangu na nikaanza kutoa machozi.Ghafla nikasikia sauti ikiniambia USILIE KAMA WAO,WALA USIWALAUMU,BALI WASAIDIE UWATOE SHIMONI.Ghafla nikashtuka na nikagundua nilikuwa ndotoni!

Nilipoamka ni kama ndoto ilendelea nikiwa macho sasa kwani nilianza kupata maana na ujumbe uliopo katika ndoto ile:

-Wakati hospitali ya Apolo India inaidai serikali yetu bilioni 16 za matibabu hususani viongozi wa serikali na wanasiasa bado Maskini wa kitanzania wanakufa kwa kasi kwa kukosa huduma bora za matibabu na kushindwa kununua dawa kutokana na gharama za juu za dawa hizo.Tukumbuke kuwa tusipofanya kitu leo tutakuwa wahanga kesho. MABADILIKO YANAWEZEKANA, TUKIAMUA TUNAWEZA.

-Nchi hii leo imegeuka kuwa ya wachuuzi;Unapopita na kukuta vijana wenzako wanauza pipi ambazo mtaji wake haufiki hata shilingi 2,000 na anaanza kukueleza kuwa ni siku ya pili hajala.. Tusifunge masikio yetu na macho yetu.Tuje na miradi ya kuongeza ajira na tuendelea kuwasadia kwa kidogo tulichonacho.Tukumbuke,MABADILIKO YANAWEZEKANA,NA TUKIAMUA TUNAWEZA.

-Ukishuka mabonde kuelekea Kusini wakulima wa Korosho wanalia,wanapaza sauti kueleza kuwa miaka 50 sasa hawajapata Faida yoyote ya kulima korosho.Walipoona kuna Tumaoni la Gesi walianza kupaza sauti ili waelezwe watanufaikaje na rasilimali gesi sisi kama vijana TUSIWALAUMU na TUSIWAACHE PEKE YAO.Tukumbuke;MABADILIKO YANAWEZEKANA,TUKIAMUA TUNAWEZA.

-Ukipanda milima kuelekea Kaskazini MINOFU YA SAMAKI inaendeea kusafirishwa kulekea nje ya nchi na mapanki yanaendelea kubaki nchini kwa ajili ya watanzania.Viwanda vimekufa na ajira zinazidi kupungua.Tunapokutaka na vijana waliokata tamaa na hawajui wafanye nini tuwakumbushe.MABADILIKO YANAWEZEKANA,NA TUKIAMUA TUNAWEZA.

Tunapoondoka Hapa Leo,kila mmoja wetu awe ni Kijana Mjumbe wa Mabadiliko.Kelele za vilio ziko Kaskazaini,Kusini,Magaharini na Mashariki.Huko kote wanatusubiri tuwasaidie.

Nchi hii Inasubiri Uchukue Hatua,Inasubiri Ufanye Kitu,Wakati Umefika,Wakati Ndio Sasa.TUSILAUMU BALI TULETE MABADILIKO.

TUKUMBUKE-Mabadiliko hayawezi Kuja kama Tunamsubiri mwingine ayalete,Mabadiliko hayawezi kuja kama tunasubiri wakati Mwingine.Wanaoweza Kuleta Mabadiliko ni Sisi,na Wakati wa Mabadiliko ni LEO.

Ni vyema tukumbuke “If we don’t do it today, it might be too late to be done Tommorow”

Mungu Ibariki Afrika,

Mungu Ibariki Tanzania,

Ahsanteni kwa Kunisikiliza.

Joel Arthur Nanauka
jnanauka@gmail.com;0688-677968

Comments

Patroba Bwire
Reply

Hongera sana kaka Joel, Hotuba yako ni nzuri na yenye kuwafanya vijana wanaojitambua kuchukua hatua mathubuti kwa ajili ya kuleta mapinduzi ya Fikra katika nchi yetu, Africa na duniani kwa ujmla, naaamini ujumbe umefika na mimi kama kijana mwenye kuitaji mabadiliko ya fikra yakinifu kwa Taifa langu, Africa na hata kuona dunia ikiishi katika speed inayoendana na mabadiliko ya siasa makini, uchumi shirikishi na imara na uhuru wa kushiriki katika mabadiliko yenye tija kwa kufuata utu na uzalendo asilia. BE BLESSED SIR JOEL.

nanauka
Reply

Ahsante patroba,ubarikiwe sana pia.Tuendelee kuombeana.

esnath
Reply

Mungu akutunze vyemaaaa

Bellet
Reply

My friend Nanauka….

What a wisdom????

You are a great seed of this beautiful NATION….. Keep it on my bro….

Ipo wiki hii mbegu itaota…

God bless u…

Hamidun
Reply

Mzee wa Asali BIG UP SANA.
It is nice presentation. i wish they didn’t postpone it , so many could hear it and may be act on it.

Keep it up bro.

julius
Reply

Br Nanauka, asante saaana kwa hotuba yako nzuri yenye dira kwa ustawi WA kweli juu ya Tz,,
Ni dhahiri tunahitaji kuwa chachu ya mabadiliko..zamu imetufikia,,tutatoa ripot gan jua likizama kipindi chetu!!! Nakupenda br.

Leave a comment

name*

email* (not published)

website