Navigate / search

Hatua Tatu Za Kubadilisha Wazo Kuwa Uhalisia

 

Kama kweli unataka kufanikiwa katika maisha yako ni lazima ujijengee uwezo wa kubadilisha mawazo yako kuwa vitendo.Kati ya vitu ambavyo vinawakwamisha watu wengi sana ni udhaifu wa kubadilisha mawazo yaliyoko kichwani kwao kuwa vitendo katika mikono yao.Jambo mojawapo muhimu sana ambalo unatakiwa kulitambua katika maisha yako ni kuwa,mawazo mazuri ambayo hayafanyiwi kazi hayawezi kukusaidia kubadilisha maisha yako kwani unakuwa hauna tofauti na mtu ambaye hawazi kabisa.

Ndani ya ubongo wako kuna eneo linalohusika na mawazo na pia kuna eneo linalohusika na maamuzi.Ili ufanikiwe lazima uwe na uwezo wa aina zote mbili;wa kuwaza na pia kutendea kazi mawazo yako.Watu wanaowaza tu bila kuwa na uwezo wa kutenda huwa na tabia ya kujua mambo mengi sana lakini huwa wanafanya machache sana ukilinganisha na vile vitu ambavyo wanavijua.

Hawa ni aina ya watu ambao ukianza kuzungumzia kilimo watakueleza jinsi ilivyo rahisi kutajirika kupitia kilimo;watakuiambia mtaji unaohitaji,gharama ya kukodisha mashamba,aina za mbegu,mavuno na utakavyotengeneza pesa kwa muda mfupi sana.Ukizungumzia fursa zozote za biashara au ajira,huwa wako mstari wa mbele kutoa maelezo marefu yenye kushawihsi akili,lakini ukichunguza maisha yao utagundua kuwa hakuna kitu wanachofanya miaka nenda rudi.Ukitaka kujua kama wewe ni mmoja wao jipime kiwango cha maarifa uliyonayo kuhusu mambo mbalimbali na angalia kiwango cha mambo unayofanya.Kama mambo unayoyajua na kuyasema ni mengi sana na hayafanani kabisa na unayoyatenda basi ujue uko kwenye mwelekeo wa aina ya watu ambao huwa hawafanikiwi.

Miaka minne iliyopita nilisikia habari za binti mmoja mnaijeria anayeitwa Kasope Ladipo-Ajai amabaye alikuwa na umri wa miaka 27 kwa wakati huo.Binti huyu alikuwa anafanya kazi katika kampuni ya usafirishaji wa ndege ya Nigeria.Kwa sababu ya kusafiri mara kwa mara katika nchi za ulaya na marekani,kila wakati alipokuwa anaingia katika maduka alikutana na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa  nchini Nigeria lakini zilizoonyehswa kuwa zimewekwa kwenye vifurushi zikitokea nchini Ghana.Hapo ndipo alipoanza kupata wazo la kuanza kusafirisha bidhaa kutoka Nigeria moja kwa moja na kusafirisha kwenda katika masoko haya ya ulaya na marekani.

Baada ya kufanya utafiti wake kwa muda wa miaka minne,Kasope aliamua kuacha kazi na akajiunga na mwenzake na wakafungua kampuni ya kuuza vyakula na viungo nchini Nigeria waliyoipa jina la OmoAlata Food Services.Walipoanza kampuni yao hawakuanza na bidhaa ghali na adimu,waliamua kuanza kununua pilipili,kuziweka kwenye vifurushi na kuziuza.Baada ya muda mfupi walianza kuwa na wateja wengi sana yakiwemo maduka makubwa maarufu sana (Supermarkets) nchini Nigeria.Na ndani ya muda mfupi walianza kuwa na wateja wakubwa kama 25 waliokuwa wananunua bidhaa zao.Kwa sasa kiwanda chao kinazalisha bidhaa nyingi sana na kina wateja wengi wanaowapatia faida ya kutosha kujilipa mishahara minono na wanaendelea kukua wakijiandaa kuanza kusafirisha nje ya nchi.

Wakati binti huyu anahojiwa ili kueleza safari yake ya mafanikio,alielezea mambo matatu muhimu katika kulifanya wazo lako likuletee mafanikio:

Jambo la kwanza ni uwezo wako wa kugundua fursa za kukutengenezea pesa.Kila siku tumezungukwa na fursa ambazo kama tukiamua kuzitumia na kuzifanyia kazi basi zitatusaidia sana.Hakuna mahali ambapo hakuna fursa za mafanikio,hata hapo ulipo leo kuna fursa ambayo kama ukiamua kuifanyia kazi itakuletea tofauti kubwa sana.Usikubali kuamini kuwa hakuna fursa kwani kwa kufanya hivyo unajiwekea hali ya upofu wa mafanikio katika maisha yako.Siku moja nilishangaa sana nilipokutana na binti mmoja ambaye kwa sasa anafanya kilimo cha bamia mto Ruvu ambaye kwa taaluma ni daktari pia,lakini mapato yake yanayotokana na kilimo cha bamia ni makubwa kuliko mshahara anaoupata kama daktari.Usikubali hata siku moja kuamini kuwa kiwango chako cha sasa ndio kiwango cha juu zaidi cha mafanikio,siku zote kumbuka kuwa unayo nafasi ya kuona fursa zaidi na ukizifanyia kazi zitakusaidia sana.

Jambo la pili la muhimu sana kuhusiana na mafanikio ni kuchukua hatua za kujifunza kwa bidii kile kitu ambacho hasa ndicho unataka kukifanya katika maisha yako.Tunaishi katika ulimwengu ambao taarifa na maarifa ndio zimeshika hatamu na ndio nguvu inayobeba mafanikio ya kila mmoja wetu.Ukweli ni kuwa kasi yako ya kupata maarifa ndiyo itajulisha kasi yako ya kufanikiwa katika kile ambacho unakifanya katika maisha yako.Kuanzisha kiwanda kidogo cha kuweka pilipili katika vifungashio na kuchanganya viungo mbalimbali ili kuleta ladha nzuri kwa wateja sio jambo ambalo binti huyu alikuwa analifahamu hapo kabla.Kitu alichoamua kukifanya ni kutumia maarifa ya yanayopatikana katika mtandao na kujifunza mambo mbalimbali kuhusiana na biashara anayotaka kuifanya.Badala ya kutumia muda wake mwingi katika kusoma stori za wasanii au michezo kwenye mitandao ya kijamii ama kuangalia video mpya za wasanii alimua kununu vifurushi vya intaneti na kisha kuviweka kuanza kutafuta maarifa mbalimbali kuhusiana na kile kitu ambacho alikuwa anakusudia kukifanya.

Usiwe mtu ambaye unazungumzia wazo lako tu bila kuchukua hatua za kujijenga zaidi ili upate uwezo wa kulifanyia kazi bila kushindwa.Kitaalamu inasemwa kuwa ili uwe na maarifa ya kutosha katika kile uanchotaka kukifanya unatakiwa angalau kwa kila siku uwekeze dakika zisizopungua 30 kupata maarifa mapya na yanayotakiwa katika jambo hilo.Kuanzia leo hebu jichunguze mwenyewe ili uone uwe unatumia muda gani kila siku kupata maarifa juu ya kile unachokifanya/unataka kukifanya.Kama hauna uwezo wa kupata taarifa katika mitandao basi unaweza kununua kitabu,kuhudhuria semina,kufuataliia Makala kama hizi ama kutafuta mtu ambaye tayari anafanya kile unachotaka kukifanya na amefanikiwa ili upate maarifa kutoka kwake.

Kitu cha tatu cha muhimu kujifunza toka kwa binti huyu ni jinsi ambavyo aliweza kutumia mtandao alionao na kile alichonacho huku akiendelea kutafuta kile ambacho hakuwa nacho.Anasema kitu cha kwanza alihitaji ardhi na akagundua kuwa kuna baadhi ya ndugu zake wana ardhi ambayo hawaitumii hivyo aliamua kuwaomba aitumie na alikubaliwa bila gharama yoyote kwa kuanzia.Unapotaka kuanza kufanya jambo lolote ni muhimu sana ukajiuliza,hivi kuna nini ambacho ninakihitaji na naweza kukipata kwa watu wangu walio karibu kabla sijaenda kukitafuta mbali?Usianze kusema kuwa hawatakubali kabla haujajaribu kuwaomba.Chukua hatua!

Siku zote usiache kulitendea kazi wazo lako kwa kukosa  kitu ambacho unakihitaji.Kama unataka kufanikiwa na kutimiza malengo uliyonayo katika maisha yako-ANZA NA KILE ULICHONACHO NA ANZA PALE ULIPO.Usisubiri,Anza sasa.

Kitabu cha TIMIZA MALENGO YAKO kimeelezea mbinu 60 ambazo watu waliofanikiwa wanazitumia kufikia kilele cha mafanikio yao.Unaweza kuwasiliana nasi kupitia namba 0655 720197 na tutakuelekeza kwa wakala wetu katika mkoa uliopo ama kama uko Dar Es Salaam na unahitaji kuletewa hadi pale ulipo uanweza kuwasiliana nasi kupitia 0712 224282

See You At The Top

 

Leave a comment

name*

email* (not published)

website