Navigate / search

Hatua 3 za Kufanya Maamuzi Ambayo Yatakuletea MAFANIKIO.

mentorship tz

Mwaka 1973 Profesa Walter Kaufmann wa chuo kikuu cha Princeton aligundua tatizo moja kubwa sana ambalo huwa linachangia watu wengi wasiweze kufanikiwa katika maisha yao.Tatizo hili linaitwa kwa jina la kitaalamu “decidophobia” ikimaanisha hali ya kushindwa/kuwa hofu ya kufanya maamuzi katika maisha.Kwa sababu ya kushindwa kufanya maamuzi watu wengi sana wamejikuta wakiwa katika hali zilezile bila kupiga hatua kwa muda mrefu sana katika maisha yao.Ukweli ni kuwa hali yako uliyonayo leo ni matokeo ya maamuzi ambayo uliyafanya huko nyuma,hivyo kama hautaki kubakia pale ulipo leo ni lazima uamue kufanya aina ya maamuzi ambayo haujawahi kuyafanya kabisa katika maisha yako.

Kazi uliyonayo leo,biashara uliyonayo leo,maisha unayoishi leo ni matokeo ya maamuzi ambayo uliyafanya huko nyuma katika maisha yako.Hivyo basi kama ambavyo uliamua kuchagua maisha unayoishi sasa hivi,ndivyo ambavyo unaweza kuamua kuyabadilisha maisha unayoishi leo.Hebu jichunguze katika maisha yako,kuna jambo ambalo hauridhiki nalo kabisa?Kuna kitu ambacho ungependa kibadilike?Kuna aina ya maisha ambayo unayapenda kuyaishi?Kama jibu lako ni ndio basi jua kuwa uwezo huo unao kama utakuwa tayari kufanya maamuzi bila uwoga wowote.

Watu ambao wamebakia katika hali zao bila kubadilika kabisa ni wale ambao kila wakati wanaishia kulalamika kuhusiana na aina ya maisha wanayoyaishi lakini hawako tayari kufanya maamuzi yoyote kuhusiana na maisha yao,ni kama vile wanamsubiri mtu mahali fulani aweze kuwabadilishia maisha yao.Kuna mambo katika maisha yako huwa yanaweza kubadilika kwa sababu muda umepita (kama ilivyo usiku lazima utaingia hata bila wewe kufanya maamuzi yoyote),lakini kuna mambo ambayo hayataweza kubadilika katika maisha yako hadi wewe mwenyewe uchukue hatua ya kufanya mabadiliko.

Kati ya vitu ambavyo ni lazima ufanyie maamuzi katika maisha yako ni kuamua kuwa hautakubali kushindwa katika maisha yako.Jim Cantrel ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya SpaceX inayojisghulisha na kupeleka vifaa vya kiteknolojia mwezini alipoulizwa siri ya mafanikio yake alisema-Ni Uamuzi ambao aliwahi kuufanya katika maisha yake kuwa hata iweje,hatakubali kushindwa katika maisha yake.Na kwa sababu hiyo kila wakati alipojikuta ameshindwa kufanikiwa katika jambo fulani basi alitafuta njia nyingine ya kulifanya.

Ni lazima ifike hatua katika maisha yako ufanye maamuzi ya kufanikiwa;Mafanikio huwa hayaji kwa bahati katika maisha ya mtu,ni matokeo ya maamuzi ambayo mtu huyafanya.kila unayemuona amefanikiwa katika maisha,jua kwamba kuna siku alifanya maamuzi ya kufanikiwa na hakukubali jambo lolote limkwamishe ama lifupishe safari yake.Je,wewe umeshawahi kufanya maamuzi ya namna hii.Mara nyingi maamuzi haya hutakiwi kusubiri hadi uone dalili za mafanikio,unatakiwa kuyafanya wakati hata kukiwa hakuna dalili yoyote ya mafanikio.Hata kama leo maisha yako yanaoenekana kuwa hayana matumaini yoyote yale,hata kama inaonekana kama vile hautaweza kufikia lengo ulilojiwekea-Fanya jambo moja la muhimu leo:Amua kuwa lazima utafanikiwa bila kujali chochote kile kitakachotokea katika maisha yako.

Ili kufanya maamuzi yatakayokusaidia katika maisha yako kuna hatua TATU unapaswa kuzichukua:

Moja ni ile hali ya kutambua na kukubali kwamba kuna uhitaji wa wewe kufanya maamuzi fulani.Watu wengi wanajikuta wamekwama mahali pamoja  katika maisha yao kwa muda mrefu kwa sababu huwa hawataki kukubali kuwa wanamatatizo.Kukataa tatizo hakufanyi tatizo kuondoka bali kunafanya ugumu wa kutatua tatizo uongezeke.Wengi ambao wamekata tamaa huamua kusema kuwa “mimi nimeridhika na maisha yangu au mimi nimeridhika na kazi yangu” lakini ukweli wa ndani ya moyo wao huwa wanatamani sana kubadilika na kuwa na maisha mazuri zaidi.Ili ufanye maamuzi yatakayoleta matokeo ni lazima ukubali kuwa una tatizo unalohitaji kulitatua.Hebu chunguza maisha yak oleo,je kuna maeneo ambayo unahitaji kuyafanyia maamuzi.

Pili ni kutambua ni maamuzi gani unatakiwa kuyafanya.Kama umegundua kuwa kipato chako ni kidogo na matumizi yako nin makubwa,pengine utahitaji kufanya maamuzi ya kupunguza idadi ya ngu unazonunua kwa mwezi ama kuamua kutafuta kazi nyingine ya ziada.Kwa kila eneo la maisha yako ambalo umeona kuna uhitaji basi jitahidi kujiuliza hapa natakiwa kufanya uamuzi gani?-Mwingine itakuwa ni kutafuta kazi mpya,mwingine itakuwa ni kuvunja uhusiano,mwingine ni kumwambia mtu ukweli badala ya kuendelea kuumia,mwingine ni kuchukua mkopo n.k.Hebu tafakari katika maeneo uliyotaja hapo juu ni maamuzi gani unapaswa kuyachukua?

Tatu ni kuchukua hatua ya kufanyia kazi maamuzi uliyoyaamua.Haitakusaidia chochote kama utaamua na kisha hautachukua hatua yoyote ile.Kuna watu wengi walishaamua kufanya biashara siku nyingi sana lakini hadi leo hawajaanza,kuna watu walishaamua kuanza upya maisha yao lakini kila siku wanarudi tena kwenye mahusiano ya zamani,kuna watu walishaamua kulima shamba lakini hadi leo hawana hata robo heka,wako mijini wanazurura tu,kuna watu kila ukikutana nao watakuambia kuwa wanataka kuwa wafugaji wa kuku lakini hata hawajaanza kufuga kuku mmoja n.k

Maamuzi bila hatua thabiti hayatakusaidia kabisa,chochote ambacho umekifanyia mamuzi leo tafadhali chukua hatua na ukifanyie kazi bila kuchelewa.Natamani sana pia kujua maamuzi gani ya muhimu ambayo umeyachukua leo,tuwasiliane tafadhali.
Kumbuka kuwa kadiri unavyochelewa kufanya maamuzi ndivyo kadiri utakavyochelewa kufanikiwa.

Kumbuka kuwa ndoto Yako Inawezekana,
Endelea kutembelea www.JoelNanauka.Com na www.mentorship.co.tz ili kujifunza zaidi.
See You At The Top.

@JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website