Navigate / search

Hatua 3 Ambazo WAZO Lazima Lipitie Kabla Haujafanikiwa

22

Kuna nyakati katika maisha yetu ambazo huwa tunapitia na ghafla kujikuta imani yetu kubwa tuliyowahi kuwa nayo juu ya mafanikio yetu imekufa.Hivi umeshawahi kuamini katika wazo fulani kwenye maisha yako na mara  baada ya muda fulani unakuta ile nguvu ya kuendelea kuliamini wazo lilelile inazidi kupungua na hatimaye inakufa kabisa?Kuna watu walishawahi kuamini katika wazo fulani la biashara na wakaweka nguvu zao zote katika wazo hilo na wakafanya kila kila kitu ili kufanikiwa walipokuwa wanaanza lakini kwa leo ukikutana nao tena ile hamasa ya kufanya jambo lilelile imeshakufa na wameacha kabisa.

Aliyewahi kuwa Rais wa India Abdul Kalam aliwahi kusema — “Ndoto sio kile kitu ambacho huwa unakiona unapokuwa usingizini bali ni kile kitu ambacho huwa kinakukosesha usingizi”.Mawazo yanayosisimua na kuonekana yanaweza kukufanikisha kwa haraka hayawezi kuwa ndio chachu ya mafanikio peke yako-Mafanikio ni zaidi ya hapo.Kufanikiwa kwenye maisha yako kunatokana na ile hali ya kuamini jambo fulani na kutoruhusu kitu au mtu yoyote yule akukatishe tamaa ama akuaminishe vinginevyo.

Kila wazo ulilonalo lazima lipitie hatua kadhaa kabla halijaweza kufanikiwa.Hatua ya kwanza ni ile ya kukupa hamasa na kuonekana inawezekana bila shaka.Katika hatua hii mtu anakuwa “hasikii wala haoni”-hapa ndipo hutokea kitu kinaitwa upofu wa mafanikio.Hata kama kuna hatari ya waziwazi katika kile kitu mtu anataka kukifanya lakini si rahisi yeye mwenyewe kukiona.Hata utakapojaribu kumuonyesha pia,haitakuwa rahisi kwake kukubali.Katika hatua hii ya wazo,mtu huwa tayari kufanya chochote ili kuhakikisha wazo lake limefanikiwa.Watu wengi huwa na nguvu za kufuatilia na kufanya mambo kwa kiwango cha juu sana kwa sababu ya tumaini kubwa ambalo wanakuwa nalo.

Hatua ya pili huitwa uhalisia wa wazo.Hapa ni pale ambapo mtu huanza kulifanyia kazi wazo kwa katika matendo.Kumbuka siku zote wazo litaonekana ni rahisi kwa maneno lakini mara utakapoanza kulitekeleza ndipo utakapoanza kugundua changamoto mbalimbali katika uhalisia.Hapa ndipo mtu anapogundua kuwa nia peke yake haitoshi inahitajika uvumilivu.Katika hatua hii ndio watu hujikuta wako peke yao katika kutekeleza wazo lao na ni kama hakuna mtu ambaye yuko tayari kuwaunga mkono.Hii ndio pale wale uliowategemea wawe msaada wa karibu sana hawaonekanai tena na kila ukijaribu kuwapigia simu hawaonyehsi ushirikiano kabisa.

Hatua ya tatu ni ya kufanya maamuzi ya kuendelea ama kuacha.Wazo lolote lile ambalo ni muhimu kwenye maisha yako ni lazima likufikishe katika hatua hii.Unajaribu kuangalia mbele unaona giza,unajaribu kupiga hatua unaona nguvu zote ni kama zimeisha,unajaribu kutafuta msaada ni kama milango yote imefungwa,unasikia maumivu na hakuna anayeonekana kujali kabisa.Ili ufanikiwe ni lazima uvuke katika hatua hii.Huu ndio ule wakati ambao unaona kama hakuna umuhimu wowote wa kuendelea kuishi na unaona kama vile thamani yako hakuna tena.Ili ufanikiwe ni lazima uamue kuwa hautakubali kuliacha wazo lako njiani,utalifikisha mwisho.

Katika hatua hizi tatu,kuna watu huwa wanaishia hatua ya kwanza,wengine wanaishia hatua ya pili,wengine wanaishia hatua ya tatu na wengine huvuka na kufanikiwa.Hata hivyo swali la msingi la kujiuliza ni kuwa “Kwa nini wengine wanaweza kufanikiwa na kuvuka hatua zote hizi na wengine huishia njiani?”.Kuna mambo ambayo ukiyajua na kuyafanya basi na wewe yatakusaidia sana usiwe mtu wa kuishia njiani wakati wowote ule.Kila ambaye amefanikiwa kuvuka vikwazo vyote hivi ni lazima alifanya jambo moja la muhimu sana:Alijiwekea mpango wa muda mrefu wa maisha yake.

Kati ya vitu ambavyo usipokuwa navyo katika maisha yako vitakufanya ushindwe kila wakati ni ile hali ya kutokuwa na mpango wa muda mrefu kuhusiana na maisha yako.Inashauriwa kila mtu awe na mpango wa muda mrefu wa angalau miaka 10 lakini kama ukiweza basi unaweza kuweka wa miaka mingi zaidi ya hapo.Mpango wa muda mrefu ni chachu ya mafanikio yako na hukupa nguvu ya kufanya mambo ukijua fika kuwa mbele yako kuna jambo kubwa sana ambalo unalitarajia.

Kuwa na mpango wa muda mrefu ni sawa na kukata tiketi ya basi kwenda safari ya mbali.Hata ikitokea basi limeharibika njiani ama kuna tatizo limetokea,utakubali kuvumilia na kusubiria kwa sababu tayari unajua unakoelekea,hautakubali kuishia njiani.Unapokuwa hauna mpango wa muda mrefu kuhusu maisha yako  ni rahisi sana kupoteza mwelekeo wa maisha yako na ni rahisi sana kukata tamaa.Kuna watu wengi sana ambao hawajawahi kufikiria miaka kumi ijayo watakuwa wapi,wanafanya nini na watakuwa ni nani?Kama wewe ni mmoja wao ningekushauri leo ufanye zoezi hilo la kupanga kuhusiana na maisha yako ya muda mrefu ujao.

Watu ambao huwa wanajua wanakoelekea sio rahisi kukata tamaa na kuishia njiani.Ni kama wewe tuseme uko kwenye kituo cha daladala unataka kwenda nyumbani na ghafla mvua ikaanza kunyesha:Hivi utaamua kughairisha kwenda nyumbani na ukalala kituoni kwa sababu ya mvua?Bila shaka jibu ni hapana.Lakini mtu ambaye ni mwendawazimu anaweza kuamua kulala kwa sababu hana mpango wa mahali anapoelekea.Kama unataka kuwa mtu ambaye unafanikisha wazo lako hadi mwisho basi ni lazima uwe na mpango wa muda mrefu kuhusiana na maisha yako.

Hebu leo pata muda na ujiulize hivi mpango wangu wa muda mrefu kuhusu maisha yangu ni upi?Ninataka kumiliki fedha kiasi gani baada ya miaka 10?Ninapanga kuwa na familia ya namna gani?Nitakuwa nafanya kazi gani baada ya miaka 10?Je nitakuwa na elimu/ujuzi upi baada ya miaka 10?n.k Jiulize na ukishapata majibu weka katika maandishi kuwa ndio ramani ya maisha yako.Baharia mwenye ramani ya anakokwenda hata mawimbi yakiwa makali namna gani ni lazima ataendelea na safari yake hadi anakokwenda.Usiwe mtu ambaye unaishi duniani bila kujua mwelekeo wako.
Share na wengine na endelea kutembelea www.JoelNanauka.com/www.mentorship.co.tz  ili kujifunza zaidi.
See You At The Top.

Leave a comment

name*

email* (not published)

website